WAYEMEN WAANDAMANA KUPINGA VITA DHIDI YA SYRIA.


Raia wa Yemen wamefanya maandamano ya kupinga aina yoyote ya vita tarajiwa vya Marekani dhidi ya Syria. Maandamano hayo yamefanyika leo katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa na kulaani vikali aina yoyote ya mashambulizi hayo ya Washington na waitifaki wake dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu na kutangaza rasmi kuungana na serikali na taifa la Syria. Washiriki wa maandamano hayo yaliyoanzia katika medani ya al-Taghyiir kuelekea chuo kikuu cha Sanaa, walibeba bendera ya taifa la Syria na picha za Rais wake Bashar al-Asad, huku wakitoa nara za kuunga mkono taifa hilo. Hayo yanajiri katika hali ambayo, ulimwengu umeendelea kulaani vikali hatua hiyo ya kijuba inayoweza kuchukuliwa na Marekani. Mapema leo mfalme wa Jordan ambaye ni mshirika wa karibu wa Marekani ametangaza kupinga vita hivyo tarajiwa huku akisisitiza juu ya kutatuliwa mgogoro wa Syria kwa njia za kidiplomasia. Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan amesema kuwa, mashambulizi yoyote dhidi ya Syria, yatawasha moto katika eneo zima la Mashariki ya Kati sambamba na kuzisukuma nchi nyingi kuingia katika mgogoro huo. Aidha hapo jana Nouri al-Maliki Waziri Mkuu wa Iraq alitangaza rasmi upinzani wa nchi yake kwa mashambulizi hayo tarajiwa dhidi ya taifa jirani la Syria huku akisema kuwa, hatua hiyo inaenda kinyume na sheria za kimataifa. Mbali na hapo nchi za Iran, Russia na China zimetangaza pia kupinga aina yoyote ya uvamizi huo wa kijeshi dhidi ya Syria huku zikiionya Marekani na waitifaki wake juu ya kile zilichokitaja kuwa ni kujizamisha kwenye kinamasi huko Syria.