Rais Hassan Rohani wa Iran na mwenzake wa Russia Vladimir Putin wameafiki kuimarisha jitihada za kuzuia uvamizi wowote wa kijeshi dhidi ya Syria.
Katika mazungumzo yao ya simu Jumatano usiku, marais hao wawili walisisitiza kuwa utumizi wa nguvu za kijeshi dhidi ya nchi yoyote pasina kuwepo idhini ya Umoja wa Mataifa ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa.
Matamshi hayo yalikuija punde baada ya nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Umoja wa Mataifa kufanya kikao cha faragha ambapo zilishindwa kuafikiana kuhusu pendekezo la Uingereza la kutaka Syria ishambuliwe kijeshi. Rais Putin amepinga madai ya Marekani na waitifaki wao kuwa Syria ilihusika na hujuma ya silaha za kemikali. Amesema jeshi la Syria lilikuwa limefanikiwa kukabiliana na waasi wanaopata himaya ya kigeni na hivyo halikuhitaji kutumia silaha za kemikali. Naye Rais Rohani ameonya kuwa uvamizi wowote wa kijeshi utavuruga eneo zima la Mashariki ya Kati. Wakati huo huo Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran Mohammad Ali Ja’afari ameionya vikali Marekani kuwa itakumbwa na hatima sawa na ya Vitenam iwapo itavamia Syria. Naye Mkuu wa Majeshi Yote ya Iran Meja Jenerali Hassan Firouzabadi ameonya kuwa hujuma yoyote ya kijeshi dhidi ya Syria itauteketeza utawala haramu wa Israel.