WAMAGHARIBI WASHINDWA KUPATA INDHINI YA BARAZA LA USALAMA YA KUISHAMBULIA KIJESHI SYRIA.


Kikao cha jana Jumatano cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilimalizika bila ya kukidhi matakwa ya Magharibi. Wawakilishi wa China na Russia, nchi mbili wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama ambazo zina haki ya kura ya turufu walitoka nje ya kikao hicho na kutoruhusu kupigiwa kura rasimu ya azimio lililokuwa limetayarishwa na Uingereza. Kama alivyosema Mkuu wa Kamisheni ya Masuala ya Kimataifa ya Bunge la Russia “Duma” ni kuwa, lengo la mpango wa Uingereza lilikuwa ni kuanzishwa operesheni ya kijeshi dhidi ya Syria. Uingereza imewasilisha rasimu ya azimio hilo hata kabla ya timu ya uchunguzi ya watu 11 ya Umoja wa Mataifa kumaliza kazi yake ya kuchunguza matumizi ya silaha za kemikali huko Syria. Kama rasimu ya azimio hilo ingepasishwa, Syria ingeanza kukabiliwa na operesheni ya kigeni ya kijeshi. Agosti 21 maroketi 29 yaliyokuwa na silaha za kemikali yalishambulia maeneo ya viunga vya Damascus na kusababisha watu 350 kuuawa na wengine 3000 kujeruhiwa. Madola ya Magharibi yalitangaza kwamba, jeshi la Syria limetumia silaha za kemikali dhidi ya makundi yanayobeba silaha, ilhali hata hakukuwa na uchunguzi wowote wa kitaalamu uliokuwa umefanyika kuhusiana na suala hilo. Serikali ya Syria imekanusha vikali madai hayo na kusisitiza kwamba, ni magaidi ndio waliofanya mashambulio ya silaha za kemikali huko al-Ghouta Mashariki. Kufanywa mashambulio ya silaha za kemikali katika ardhi ya Syria, kumeufanya mgogoro wa nchi hiyo pamoja na juhudi za kimataifa za kuutatua kuwa tata zaidi. Huko nyuma Wamagharibi walikuwa wametangaza kwamba, hawatanyamazia kimya utumiaji silaha za kemikali utakaofanywa na jeshi la Syria na kwamba, kufanya hivyo ni kuvuka mstari mwekundu na natija yake ni kukabiliwa na mashambulio ya kijeshi. Kwa kuzingatia matukio hayo, ni jambo lililo mbali sana kwamba, jeshi la Syria ndilo lililotumia silaha za kemikali. Serikali ya Syria ambayo daima imekuwa ikisema ni jambo baya kutumia silaha hizo imekanusha vikali tuhuma hizo; kwani kutumia silaha hizo ni tishio kwake hasa kwa kutilia maanani kwamba, kufanya hivyo ni kuwapa Wamagharibi kisingizio cha bure cha kuanzisha mashambulio ya kijeshi. Katika upande mwingine, wale ambao wanaunga mkono kushambuliwa kijeshi Syria, ndio wenye msukumo zaidi wa kutaka kutokea maafa ya silaha za kemikali katika nchi hiyo. Inaonekana kuwa, hilo ndilo jambo lililoashiriwa na Sergei Lavrov, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia katika mazungumzo yake na William Hague, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza na kusisitiza kwamba, madai ya Syria kutumia silaha za kemikali si ya kimantiki. Aidha Lavrov amemwambia John Kerry Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kwamba, hakupaswi kuchukuliwa hatua yoyote ile isiyo ya kimantiki kabla ya kutolewa ripoti ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na shambulio la silaha za kemikali nchini Syria. Inaonekana kuwa, hatua za pupa za Uingereza za kuwasilisha rasimu ya azimio katika Baraza la Usalama inatokana na wasi wasi wa nchi hiyo na natija tarajiwa ya wachunguzi hao. Uingereza ina wasi wasi kwamba, huenda ikashindwa kutumia matokeo ya ripoti hiyo kama fursa ya kuishambulia kijeshi Syria. Inasemekana kwamba, silaha za kemikali zilizotumika katika viunga vya mji mkuu Damascus ni gesi aina ya sarin. Gesi aina ya sarin haina rangi wala harufu na ni vigumu kuweza kuigundua. Fauka ya hayo, Carla Del Ponte, mmoja wa maafisa wa ngazi za juu na mtajika wa Umoja wa Mataifa ambaye anaunda timu ya watu 11 iliyotumwa nchini Syria kuchunguza matumizi ya silaha za kemikali ametangaza kwamba, waasi wa Syria wametumia silaha hizo dhidi ya vikosi vitiifu kwa Rais Bashar al-Assad. Katika mazingira kama haya, Uingereza haiwezi kuhalalisha kwamba, inataka kukabiliana na Rais Bashar kwa ajili ya kutoa himaya na uungaji mkono kwa wananchi wa Syria. Kwa hakika Wamagharibi wameingiwa na kiwewe kwani wanaona mambo hayaendi kwa maslahi yao hasa kwa kutilia maanani kwamba, ripoti ya wachunguzi hao huenda ikatikisa nguzo za madai yao ya uongo kwamba, serikali ya Syria imetekeleza jinai za kivita. Hivyo basi tunaweza kusema kuwa, hofu ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza ya kukabiliwa na taathira hasi mpango wa Magharibi katika kipindi hiki, ndio iliyomfanya achukue hatua za pupa za kuwasilisha katika Baraza la Usalama rasimu ya azimio la uingiliaji wa kijeshi huko Syria. Habari kutoka http://kiswahili.irib.ir/uchambuzi/item/34335-wamagharibi-washindwa-kupata-idhini-ya-baraza-la-usalama-ya-kuishambulia-kijeshi-syria