Katika kuonyesha mshikamano wao kwa mwanamke wa Kiislamu aliyeshambuliwa mjini Stockholm kwa sababu ya kuvaa vazi la hijab, makumi ya wanawake nchini Sweden wameamua kusambaza picha zao wakiwa wamevaa hijab. Msemaji wa Polisi ya Sweden amesema kuwa, siku ya Ijumaa mtu asiyejulikana alimshambuliwa mwanamke mjamzito aliyekuwa amevaa vazi la stara la Kiislamu la hijab, na kumtukuna. Kama hilo halitoshi, mtu huyo pia alimchania hijabu yake mwanamke huyo wa Kiislamu na kumpigiza kichwa chake kwenye gari. Ushahidi uliopo unaonesha kwamba, itikadi za kidini ndio sababu kuu iliyopelekea mwanamke huyoashambuliwe. Katika radiamali dhidi ya kitendo hicho kisicho cha kibinadamu, kundi la wanawake wa Sweden ili kuonyesha mshikamano wao kwa mwanamke huyo Muislamu, Jumatatu walisambaza picha zao katika mtandao wa kijamii wa twitter, huku wote wakiwa wamevaa vazi la hijab. Miongoni mwa wanawake hao waliopinga kitendo hicho, ni wanasiasa na watangazaji maarufu wa televisheni, akiwemo Asa Romson kiongozi wa chama cha 'Green Party' pamoja na Veronica Palm mwakilishi wa chama cha kidemokrasia katika Bunge la Sweden. Kundi hili la wanawake pia linafanya jitihada za kuzidi kuandaa mazingira ya kuwaamsha watu ili wajue mashinikizo yanayowakabiliwa wanawake wa Kiislamu kutokana na kuvaa vazi la stara la hijab. Harakati iliyopewa jina la 'Sauti ya Hijab" imeitaka serikali ya Sweden kuwahakikishiwa wanawake wa Kiislamu wa nchi hiyo kuw, haki yao ya uhuru wa kidini inaheshimiwa. Inaonekana kuwa, kuenea kwa chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya ambako hivi sasa ni makaazi ya mamilioni ya wahajiri wa Kiislamu, kila siku kunachukua sura mpya. Jambo jipya kuhusiana na hilo ni kuwa, vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu hivi sasa vinashuhudiwa katika nchi za Ulaya ambazo huko nyuma zilikuwa zinaonekana kama vile zina hali ya kuvumiliana na kustahmiliana kidini na asili za watu. Nchi za Scandinavia ikiwemo Sweden, Norway na Denmark ni eneo lenye wahajiri wengi wa Kiislamu, na kuongezeka mashambulizi dhidi ya Waislamu katika nchi hizo kunahesabiwa kuwa ni dalili za kubadilika taratibu hali ya kijamii na kuongezeka propaganda sumu za kuufanya Uislamu uonekane tishio. Hata hivyo hatua hizo zilizoanzishwa na wanawake wa Sweden za kuunga mkono kinembo vazi la hijab la Kiislamu pamoja na wanawake wanaojisitiri kwa vazi hilo, zinaweza kuchukuliwa kuwa ni radiamali ya kukabiliana na vitendo na propaganda za chuki dhidi ya Uislamu, kuongezeka kushambuliwa Waislamu hasa wanawake wanaovaa hijabu na kwa ujumla kuwaunga mkono Waislamu wa Sweden. Hii ni katika hali ambayo, propaganda sumu za kuonesha kuwa Uislamu ni tishio, ambazo kila uchao zinazidi kuakisiwa katika vyombo vya habari vya Ulaya, zina nafasi kubwa katika kuzidisha mashambulizi dhidi ya Waislamu katika baadhi ya nchi kama vile Ufaransa, Ujerumani, Uingereza na Sweden, ambako kuna idadi kubwa ya Waislamu wahajiri. Kwa upande mwingine, baadhi ya matukio yanayofanywa na makundi yaliyofurutu ada, yanapelekea makundi ya mrengo wa kulia yenye misimamo mikali na serikali za Ulaya zizidi kuwashinikiza Waislamu na kuwawekea vipingamizi zaidi. Ushahidi unaonesha kuwa, vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu vinazidi kuongezeka barani Ulaya huku Waislamu wakinyanyaswa, kutishwa, kubaguliwa kwa njia mbalimbali, kufunguliwa kesi tofauti halikadhalika kuvunjiwa heshima matukufu ya kiislamu na propaganda kubwa dhidi Uislamu na Waislamu kukiongezeka. Licha ya hayo yote, Waislamu wanaendelea kulinda utambulisho wao wa kidini hali inayopelekea hata waungwe mkono na Wakristo ambao wanapinga kukiukwa haki za raia. Mwenendo huo huenda mwishowe ukaleta matokeo tofauti katika njama za kuufanya Uislamu uonekane tishio katika nchi za Magharibi.