Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (bunge) Ali Larijani amesema Marekani na madola mengine yenye kiburi ndio waungaji mkono wakuu wa Ugaidi unaotekelezwa na makundi ya Mawahhabi wakufurishaji wenye kufurutu mipaka au Matakfiri.
Larijani ameyasema hayo Jumatano Tehran katika Kikao cha 11 cha Siku ya Kimataifa ya Msikiti.
Larijani pia ameilaumu vikali Marekani kwa kuendelea kuwapa silaha Magaidi wanaowakufurisha Waislamu wengine huko Syria na katika nchi zingine. Spika wa Bunge la Iran amelaani vikali makundi ya kigaidi na Uwahhabi kwa kusababisha maafa katika nchi za Kiislamu. Amesema Mawahhabi wakufurishaji wanachochea uhasama baina ya Waislamu wa Madhehebu ya Shia na Madhehebu zingine za Kiislamu. Spika wa Bunge la Iran amesema makundi ya wenye misimamo mikali yanataka kuibua mifarakano baina ya Waislamu lakini wanazuoni wa Kiislamu wanaweza kuzima njama hizo kwa kuelimisha Ummah kuhusu njama hizo na kwa kuelekeza mafundisho halisi ya Kiislamu. Kwingineko katika hotuba yake Lairjani pia aliashiria umuhimu wa Misikiti katika jamii. Alisema Katika misikiti na vituo vingi vya kidini Ulaya na Marekani imedhihirika wazi kuwa watu wengi wanataka kupata umaanawi wa hakika na hili linafanyika pamoja na kuwepo mashinikizo makubwa na propagnada dhidi ya Waislamu.