Shirika la Msamaha Duniani Amnesty International limetoa taarifa likilaani ukatili na mwenendo mbaya wa serikali ya Ethiopia dhidi ya Waislamu nchini humo.
Amnesty International imeitaka serikali ya Addis Ababa kusitisha ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Ethiopia. Taarifa Amnesty imetolewa baada ya kutiwa nguvuni idadi kubwa ya Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Idil Fitri. Ripoti zinasema kuwa, askari usalama wa Ethiopia walishambulia maandamano ya amani ya Waislamu katika siku ya Idil Fitri na kuwapiga na kuwadhalilisha kisha wakatia nguvuni idadi kadhaa miongoni mwao.
Ukandamizaji huo unafanywa na askari usalama wa serikali ya Ethiopia licha ya kwamba, Waislamu wamekuwa wakifanya maandamano na mikutano ya amani katika kipindi chote cha miezi 18 iliyopita wakitetea haki zao. Askari hao wanatumia mabavu na ukatili kusambaratisha mikutano na maandamano hayo ya amani. Jumamosi iliyopita pia polisi ya Ethiopia ilishambulia maandamano ya kambi ya upinzani katika eneo la Urumia na kuua raia kadhaa kwa kuwapiga risasi. Waislamu hao wanaandamana wakitaka kuachiwa huru wanazuoni watatu wanaoshikiliwa na vyombo vya usalama.
Wapinzani wa siasa za serikali ya Ethiopia wanadai uhuru wa kiraia, utawala wa sheria na kutekelezwa haki na uadili. Vilevile Waislamu wa nchi hiyo wamekuwa wakipinga sera za serikali ya Addis Ababa za kuingilia masuala yao ya kidini. Maelfu ya Waislamu wamekuwa wakiandamana katika miezi ya hivi karibuni wakipinga suala hilo. Hata hivyo mpambano mkali zaidi kati ya polisi ya Ethiopia na Waislamu ulishuhudiwa tarehe 12 Julai mwaka jana wakati wa mkusanyiko wa kumbukumbu ya tukio la kutiwa nguvuni makumi ya Waislamu. Julai 12 mwaka jana polisi ya Ethiopia ilivamia misikiti ya Anwar na Auliyaa na kuwatia nguvuni Waislamu waliokuwa humo. Waislamu hao wanaendelea kushikiliwa jela hadi hivi sasa. Polisi ya Ethiopia inawatuhumu kuwa walivuruga amani na kufanya vitendo vya kigaidi.
Kwa mujibu wa katiba ya Ethiopia, serikali ya nchi hiyo inalazimika kulinda haki za wafuasi wa dini zote. Hata hivyo ushahidi unaonesha kuwa, serikali ya Addis Ababa imekuwa ikiwakandamiza wafuasi wa dini ya Kiislamu na kutetea maslahi ya Kikristo. Suala hilo kumepingwa na taasisi za kimataifa za kutetea haki za binadamu. Waislamu nchini Ethiopia wanaunda asilimia 34 ya jamii ya nchi hiyo.
Ukandamizaji unaofanywa na vyombo vya usalama vya Ethiopia unaonesha kuwa, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Hailemariam Desalegn amedumisha siasa za kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Meles Zenawi. Zenawi alieneza siasa za utawala wa kifederali uliojengeka juu ya misingi ya kikabila ambao uliwapa nguvu na mamlaka makubwa viongozi wanaounga mkono sera za kibaguzi. Wakati wa utawala wake, taasisi na jumuiya mbalimbali za kimataifa ziliituhumu Ethiopia hususan kiongozi wake, Zenawi, kuwa anakandamiza na kufanya ukatili dhidi ya jamii za waliowachache wakiwemo Waethiopia wenye asili ya Kisomali wa eneo al Ogaden na wapinzani wa utawala wake. Meles Zenawi alikuwa muitifaki mkubwa wa Marekani na alihusika katika matukio mbalimbali yaliyojiri katika nchi za Sudan, Somalia na katika mapigano yaliyotokea kwenye nchi nyingine kadhaa za Kiafrika. Baada ya kiongozi huyo kufariki dunia, mashirika ya Human Rights Watchs na Amnesty International yalitoa taarifa yakielezea matumaini yao kwamba serikali ijayo itatumia vyema fursa hiyo kwa ajili ya kuboresha hali ya haki za bindamu nchini humo. Mashirika hayo pia yalitaka kufutwa sheria ya ugaidi iliyopasishwa na Meles Zenawi mwaka 2009. Habari kutoka http://kiswahili.irib.ir/