RAFSANJANI AKOSOA MISIMAMO YA WAMAGHARIBI.


Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu nchini Iran amekosoa misimamo na siasa za kindumakuwili za serikali ya Marekani na Magharibi mwa ujumla. Ayatollah Akbar Hashemi Rafsanjani amesema hayo katika mazungumzo yake mjini Tehran na Javier Solana Mkuu wa zamani wa Sera za nje za Umoja wa Ulaya na kusisitiza kwamba, muamala wa kindumakuwili wa serikali ya Marekani na Bunge la nchi hiyo ni wa kutilia shaka na hauna ishara nzuri baina ya wananchi wa Iran.

Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu amesisitiza kwamba, kuna haja ya kuamiliana kiakili na masuala yote ya kisiasa na kuweko utatuzi wa kibinaadamu wenye lengo la kuyapatia ufumbuzi matatizo yaliyopo. Sheikh Rafsanjani amesisitiza kwamba, madola ya Magharibi yanapaswa kubadilisha muamala wao na Iran na kuweka kando misimamo yao ya kindumakuwili.

Javier Solana aliyekuja hapa nchini kushiriki sherehe za jana za kuapishwa Rais Hassan Rohani amesema kuwa, matokeo ya uchaguzi wa Iran yana maana kubwa kwa Wamagharibi na kuongeza kuwa, ni haki ya Wairani kushirikiana na walimwenguni na hivyo kufikia katika nafasi yao kihistoria, kiustraabu na kiutamaduni. Habari kutoka http://kiswahili.irib.ir/habari/habari/item/33817-rafsanjani-akosoa-misimamo-ya-kindumakuwili-ya-magharibi