Msichana Mwislamu ameshambuliwa karibu na mji mkuu wa Ufaransa Paris kwa sababu tu alikuwa amevaa Hijabu ya Kiislamu. Tukio hilo linaashiria kuongezeka hujuma dhidi ya Waislamu kote Ufaransa.
Binti huyo mwenye umri wa miaka 16 anasema siku ya Jumatatu alasiri, watu wawili walimshambulia alipokuwa akiondoka katika nyumba ya rafiki yake katika eneo la Trappes karibu na Paris. Anasema watu hao walimtolea matamshi ya kibaguzi na dhidi ya Waislamu kabla ya kumshambulia kwa kisu. Ameongeza kuwa waliirarua hijabu yake na kumuangusha chini huku wakimpiga mateke.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa Manuel Valls amelaani hujuma hiyo ambayo amesema inaashiria chuki dhidi ya Waislamu. Mwezi Juni mwaka huu mwanamke Mwislamu aliharibu mimba yake katika eneo la Argenteuil mjini Paris baada ya watu wenye chuki dhidi ya Uislamu kumshambulia na wenzake na kuwavua hijabu. Takwimu zinaonyesha kuwa chuki dhidi ya Uislamu au Islamophobia zimeongezeka nchini Ufaransa kwa asilimia 60 katika miezi ya hivi karibuni. Habari kutoka http://kiswahili.irib.ir/habari/mchanganyiko/item/34030-msichana-mwislamu-ashambuliwa-ufaransa-kwa-kuvaa-hijabu