BAKWATA: LAITISHA UCHUNGUZI KUHUSU SHEIKH PONDA.



Baraza la waisilamu Tanzania limeunga mkono kauli ya Jumuiya ya taasisi za kisilamu za kuitaka serikali kuchunguza kwa kina tukio lililopelekea kupigwa risasasi kwa mhubiri wa kiisilamu Sheikh Issa Ponda. Taarifa imetolewa na kaimu mufti wa Tanzania Al Had Musa Salum.

Pamoja ya kwamba (BAKWATA) limekuwa likipingana na misimamo ya Sheikh Ponda limesema serikali ilikuwa na nafasi ya kumkamata Ponda kwa kufuata mkondo wa sheria.

Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC mjini Dar es Salaam, Baruan Muhuza, sheikh huyo ambaye amekuwa katika mivutano ya mara kwa mara na serikali ya nchi hiyo alipigwa risasi baada ya kutokea vurugu kwenye mkutano wa mawaidha ya baraza la sikukuu ya Idd el Fitr.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Alhajj Mussa Kundecha, amewaambia waandishi wa habari mjini humo kuwa endapo serikali haitachukua hatua itakayowaridhisha Waislamu, wataamua kufikiria upya mustakabali wao na serikali ya Tanzania.

Sheikh Ponda amelazwa katika hospitali ya taifa, Muhimbili, mjini Dar es Salaam akiuguza jeraha la risasi huku akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu.

Msemaji wa Jeshi la polisi nchini humo Advera Senso ameiambia BBC mjini Dar es Salaam kuwa jeshi lake kwa kushirikiana na jukwaa la haki jinai wameunda kikosi kazi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa tukio hilo huku akikana kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi na polisi.

Senso amewalaumu wafuasi wa Sheikh Ponda kwa kuwazuia askari kumkamata Sheikh huyo kwa kuwarushia mawe; hatua iliyosababisha askari hao kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya na hata hivyo wafuasi hao walifanikiwa kumtorosha kiongozi huyo wa kidini.

Taarifa za jumuiya hiyo ambayo inajulikana zaidi Tanzania kama Shura ya Maimamu zinasema kuwa Sheikh Ponda ambaye polisi wanasema walikuwa wakimtafuta kwa tuhuma za kutoa matamko ya uchochezi, alisafirishwa usiku kutoka mji wa Morogoro hadi Dar es Salaam zaidi ya kilomita 200.

Sheikh Ponda kwa sasa anatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja alichohukumiwa mapema mwaka huu baada ya kukutwa na makosa kadhaa ikiwemo uchochezi wa kuharibu mali za watu. Habari kutoka http://www.bbc.co.uk/swahili/habari/2013/08/130811_tz_sheikh_shot.shtml