Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema umoja na mshikamano wa wananchi wa mataifa ndicho kitu muhimu cha kuwezesha kukabiliana na njama zinazoukabili Ulimwengu wa Kiislamu. Ayatullah Khamenei aliyasema hayo jana katika hotuba za Sala ya Idil Fitri na katika mkutano na viongozi wa Mfumo, mabalozi wa nchi za Kiislamu walioko Tehran na wananchi wa matabaka mbalimbali nchini. Katika kubainisha matukio yaliyojiri karibuni katika nchi za Kiislamu na njama za maadui za kushadidisha hitilafu baina ya Waislamu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema "kumwamini Mwenyezi Mungu" na kushikamana na "kalima ya umoja" ndivyo vitu viwili vyenye kutoa nguvu za muqawama na kuweza kusimama imara mataifa ya Kiislamu ili kukabiliana na mishale yenye sumu ya kueneza hitilafu.
Akiwahutubu moja kwa moja viongozi, wenye vipawa vya kisiasa na shakhsia wa juu wa kidini, Ayatullah Khamenei alisema:"Tilieni mkazo kadiri mwezavyo suala la kuimarisha imani, umoja na mshikamano wa wananchi; na natamani laiti viongozi wa kisiasa na wa kiutamaduni wa nchi za Kiislamu waliotingwa na matatizo na matukio yanayojiri wangelilipa umuhimu maradufu suala hili."
Baada ya kutokea mapinduzi ya wananchi katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kuangushwa tawala vibaraka za vikaragosi wa madola ya kibeberu, njama chafu za maadui wa Ulimwengu wa Kiislamu zilizotekelezwa kwa kutumia mbinu ya kuchochea hitilafu zilianza rasmi. Yanayojiri nchini Misri leo hii, na kwa kiwango fulani huko Tunisia ni mifano hai ya njama ya ukolezaji moto wa hitilafu unaofanywa na maadui katika nchi za mstari wa mbele katika Mwamko wa Kiislamu.
Mapinduzi ya Misri, ambayo yalifikia ushindi tarehe 25 Januari mwaka 2011 na kuhitimisha zama za utawala kibaraka wa Hosni Mubarak aliyekuwa kikaragosi wa mfumo wa kibeberu, yalizitia kiwewe Marekani na Israel na kuzifanya zitumie kila mbinu ili kuyatoa mapinduzi ya wananchi wa Misri katika mkondo wake wa asili.
Mnamo tarehe 3 ya mwezi uliopita wa Julai, ukiwa umepita mwaka mmoja tu tangu mmea wa demokrasia changa uanze kuchipua nchini Misri, Muhammad Morsi, rais wa kwanza wa nchi hiyo aliyechaguliwa kwa kura za wananchi alienguliwa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi. Kuwepo kwa baadhi ya hitilafu tu baina ya makundi ya kisiasa ya Misri kulitoa fursa tosha kwa Marekani na Israel pamoja na wengineo ambao hawakuyafurahia mapinduzi ya wananchi wa Misri ya kufanikisha malengo yao. Kushtadi hitilafu za ndani na uingiliaji wa baadhi ya nchi za Magharibi na hasa Marekani pamoja na utawala haramu wa Israel katika matukio ya mwezi mmoja uliopita nchini Misri, vimeisukuma nchi hiyo hadi kwenye ukingo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Katika hali kama hiyo ikiwa wananchi wa Misri watashikamana na kalima ya umoja na kumwamini Mwenyezi Mungu Mtukufu ndipo watakapopata nguvu na uwezo wa kuzikabili njama za maadui wa nchi hiyo na kutoruhusu jamii ya demokrasia changa ya Misri irejee katika zama zilizopita na matokeo yake yakawa ni kutumbukia nchi hiyo kwenye lindi la vita vya ndani. Kama alivyoeleza Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kwamba anatiwa wasiwasi na hali ya hivi sasa ya Misri, na akasisitiza kwamba lugha ya utumiaji nguvu inayotumiwa na makundi hasimu haitokuwa na faida abadani; na endapo vitatokea vita vya ndani kitapatikana kisingizio kinachohitajika kwa ajili ya uingiliaji zaidi wa madola ya kigeni ambao utaliletea balaa kubwa taifa la Misri.
Amma kadhia ya Palestina ni maudhui nyengine muhimu iliyokuwemo kwenye hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Sala ya Idilfitri. Aliashiria kuanza tena mazungumzo baina ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na Wazayuni na kusisitiza kuwa mazungumzo hayo, kama yale yaliyopita hayatokuwa na tija nyengine ghairi ya kupokwa na kupotezwa haki za Wapalestina na kumshajiisha mvamizi kufanya ukandamizaji na jinai zaidi.
Baada ya kufanya safari mara kadhaa katika eneo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry, hatimaye alifanikiwa kuwarejesha viongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwenye meza ya mazungumzo ya mapatano yanayokidhi maslahi ya Washington na Tel Aviv. Duru mpya ya mazungumzo ya mapatano imefanyika huku jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni uliokuwa ukipigiwa kelele ukiwa ungali unaendelea. Kusitishwa ujenzi huo, kuachiwa huru Wapalestina wanaoshikiliwa kwa muda mrefu sasa kwenye magereza ya kuogofya ya utawala wa Kizayuni, kurejea wakimbizi wa Kipalestina kwenye ardhi yao ya asili na kutambuliwa Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa kudumu wa Palestina yalikuwa miongoni mwa masharti yaliyotolewa na Mahmoud Abbas kwa ajili ya kurudi tena kwenye meza ya mazungumzo. Hata hivyo duru mpya ya mazungumzo hayo imeanza tena pasina kuzingatiwa hata moja kati ya masharti hayo huku tajiriba ikionyesha kuwa Marekani haijawahi katu kuanzisha harakati ya mazungumzo kwa manufaa ya Wapalestina. Ni kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba katika mazungumzo ya mapatano, Marekani imejionyesha dhahiri shahiri kuwa iko upande wa maghasibu wa Kizayuni, na bila ya shaka kinachopangwa na kusimamiwa na Waistikbari kitakuwa na madhara tu kwa Wapalestina. Habari kutoka http://kiswahili.irib.ir/uchambuzi/item/33930-mtazamo-wa-kiongozi-muadhamu-kuhusiana-na-yanayojiri-misri-na-palestina