LENGO LA VITA VYA MTUTU WA BUNDUKI NA VYA KIPROPAGANDA VYA WAMAGHARIBI NA WAARABU DHIDI YA SYRIA.


Katika kipindi ambacho jeshi la Syria linaonekana kupata mafanikio makubwa kwenye vita vyake dhidi ya makundi ya kigaidi yenye silaha, inaonekana sasa kumejitokeza medani nyingine ya mapambano yenye lengo la kufunika mafanikio hayo dhidi ya magaidi. Baadhi ya nchi za Kiarabu pamoja na nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, zimeshadidisha vita vya kipropaganda kwa kutumia vyombo vyao vya habari vya kimataifa dhidi ya Rais Bashar Asad na jeshi lake. Mfano uliohai umeonekana kupitia matangazo ya jana Jumatano Agosti 21 kwenye kanali za televisheni za Al-Jazeera ya Qatar na Al-Arabiya ya Saudi Arabia ambazo zimetangaza kwamba jeshi la Syria lilitumia silaha za kemikali dhidi ya raia wasio na hatia kwenye eneo la al-Ghouta lililoko mkoani Rif Dimashq, kusini mwa nchi hiyo. Kanali hizo zimedai kwamba makumi ya watu waliuawa kwenye shambulizi hilo. Weledi wa mambo wanaamini kwamba, vita hivyo vipya vya kipropaganda dhidi ya serikali ya Rais Bashar Asad vinalenga kuvuruga uchunguzi wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaochunguza matumizi ya silaha za sumu nchini Syria.  Wataalamu hao wa UN waliwasili Syria Jumapili iliyopita mjini Damascus na kazi yao kubwa ni kuchunguza madai ya kutumiwa silaha za kemikali katika nchi hiyo ya Kiarabu. Hii ni katika hali ambayo, Machi 19 mwaka huu, magaidi wenye silaha walitumia silaha za kemikali dhidi ya wananchi wanaomuunga mkono Rais Bashar Asad katika eneo la Khan al- Assal huko Aleppo na kusababisha maafa makubwa. Pia magaidi hao walitenda jinai nyingi dhidi ya binadamu katika eneo hilo.
Itakumbukwa kuwa, Russia iliwahi kutoa ripoti kwa Umoja wa Mataifa ikeleza kwamba magadi wa Syria wametumia silaha za kemikali na ili kuthibitisha madai hayo, Moscow ilitoa nyaraka zinazofafanua suala hilo. Ni kutokana na kufichuliwa jinai hiyo ya magaidi wa Syria ya kutumia silaha za sumu dhidi ya raia na wanajeshi wa serikali na hatua ya Damascus ya kuwakaribisha wataalamu wa Umoja wa Mataifa ili kuchunguza kadhia hiyo, ndio maana nchi za Kiarabu na zile za Magharibi zikashadidisha vita vya kipropaganda dhidi ya Rais Assad na jeshi lake. Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imekanusha madai yaliyotolewa na kanali za Al-Jazeera na Al-Arabiya kwamba jeshi la serikali lilitumia silaha za kemikali na kusisitiza kwamba propaganda hizo hazitafaulu wala kuathiri mafanikio ya jeshi kwenye vita vyake dhidi ya ugaidi. Taarifa ya Wizara ya mambo ya Nje ya Syria imesema kuwa, serikali imekubali kwa maandishi kushirikiana kikamilifu na wachunguzi wa UN na wakati huohuo imelaani magaidi kwa kutumia silaha za sumu na hivyo kusababisha maafa na uharibifu mkubwa. Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria pia imesisitiza kuwa iko tayari kushiriki kwenye kongamano la kimataifa la Geneva 2 ili kuzungumzia mgogoro unaoikumba nchi hiyo na kuutafutia ufumbuzi wa amani. Hata hivyo taarifa ya wizara hiyo imeelezea masikitiko yake kwa kile ilichosema ni njama za Saudia na Qatar na mabwana wao wa Magharibi za kuvuruga kila juhudi zinazofanywa kwa lengo la kuutatua mgogoro huo kwa njia za kidiplomasia. 
Magaidi wa Syria wanaendelea kupokea misaada ya silaha na fedha kutoka kwa baadhi ya nchi za Kiarabu zikiwemo Qatar na Saudi Arabia pamoja na nchi za Magharibi, na kwa mantiki hiyo, hatua yoyote inayoweza kupelekea kuanikwa hadharani jinai zao inaweza kutoa pigo kwa wafadhili wao na kuzima njama zao za kuipindua serikali halali ya Damascus. Hivyo basi, juhudi zote zinafanywa kuhakikisha hilo halifanyiki. Habari kutoka http://kiswahili.irib.ir/uchambuzi/item/34192-lengo-la-vita-vya-mtutu-wa-bunduki-na-vya-kipropaganda-vya-wamagharibi-na-waarabu-dhidi-ya-syria