
Yisrael Katz, Waziri wa Barabara na Uchukuzi wa utawala wa Kizayuni wa Israel ameliambia gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronot kuwa, anapinga kikamilifu kuundwa nchi yenye jina la Palestina katika mipaka ya mwaka 1967. Waziri huyo mwenye misimamo mikali ya Kizayuni ameongeza kuwa, njia pekee ya kuweza kumalizwa mgogoro uliopo, ni Israel kudhibiti usalama wa maeneo yote iliyoyotekwa tangu mwaka 1967. Amesema, ni jambo lisiloyumkinika kabisa kuundwa nchi huru ya Palestina katika mipaka ya mwaka 1967. Hii ni katika hali ambayo, viongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina wanaendelea kushikilia msimamo wao wa kuundwa nchi huru ya Palestina katika mipaka ya mwaka 1967. Viongozi hao wanaendelea kushiriki kwenye mazungumzo ya eti amani ya Mashariki ya Kati kwa tamaa kuwa kuna siku Israel itakubaliana na suala la kuundwa nchi huru ya Palestina. Hata hivyo mara kwa mara viongozi wa utawala wa Kizayuni wamekuwa wakivunja ndoto hizo za viongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa kusema wazi kuwa, ni ndoto za alinacha kudhani kwamba kuna siku watakubali kuundwe nchi huru ya Palestina kwenye mipaka ya mwaka 1967. Si hayo tu, lakini pia viongozi wa utawala wa Kizayuni wameendelea kukaidi mwito wa taasisi za kimataifa wa kuwataka wasimamishe ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. Hivi karibuni kabisa, Waziri wa Nyumba wa Israel alilitaka bunge la utawala huo liharakishe ujenzi wa vitongoji vingi zaidi vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo waliyoporwa Wapalestina. Kwa miaka mingi viongozi wa utawala wa Kizayuni wamekuwa wakipanua ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina kwa madai kuwa idadi ya Mayahudi inaongezeka, kumbe lengo lao kuu ni kufuta athari zote za Kiislamu na hata za Kikristo huko Palestina, na kulifanya eneo hilo zima kuwa na sura ya Kiyahudi. Ikumbukwe kuwa mwaka 1947, yaani mwaka mmoja kabla ya ardhi za Palestina hazijavamiwa na kukaliwa kwa mabavu na utawala pandikizi wa Kizayuni, Umoja wa Mataifa ulipasisha azimio nambari 181 la kuruhusu kuundwa nchi huru ya Palestina. Hata hivyo mwaka mmoja baadaye na kabla nchi hiyo haijaundwa, walowezi wa Kizayuni kutoka Ulaya walizivamia ardhi hizo kwa msaada wa madola ya Magharibi hasa Uingereza, wakawaua kwa umati Wapalestina, wakapora mashamba yao na kuwafukuza kwenye ardhi zao na baadaye kuzipachika jina la Israel, ardhi walizopora. Zaidi ya miaka 60 sasa imepita na tangu wakati huo hadi leo hii wananchi wa Palestina wanaendelea kukandamizwa huku wavamizi wa nchi yao wakipinga kabisa kuundwa nchi huru ya Palestina. Si hayo tu, lakini pia tangu wakati huo viongozi wa utawala wa Kizayuni wamekuwa wakifanya kila njia kuiyahudisha Palestina na kufuta kabisa athari za Uislamu za ardhi hizo. Cha kusikitisha ni kuona kuwa, hata baadhi ya Waislamu wanaiona kadhia ya Palestina kuwa ni kadhia ya Waarabu na kusahau kuwa kadhia hiyo inawahusu Waislamu, Wakristo, Mayahudi na si Wazayuni, na kila mwenye hisia za utu duniani kutokana na kuweko huko maeneo matakatifu ya kidini kama vile kibla cha kwanza cha Waislamu na maeneo walikozaliwa na kuishi Mitume wa Mwenyezi Mungu kama vile Masih Issa AS yaani Yesu (Amani ya Allah iwe juu yake na mama yake mtoharifu) na Manabii wengine wa Mwenyezi Mungu. Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia Imam Khomeini (MA) ikaitangaza Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Quds ili kuibakisha hai daima kadhia ya Palestina na kuthibitisha kuwa hiyo si kadhia inayowahusu Waarabu peke yao. Habari kutoka http://kiswahili.irib.ir/uchambuzi/item/33275-israel-yaendelea-kupinga-kuundwa-nchi-huru-ya-palestina