SIDDIQ: UAMUZI WA EU DHIDI YA HIZBULLAH NI FEDHEHA.


Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa, hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuliweka tawi la kijeshi la Hizbullah ya Lebanon katika faharasa yake ya makundi ya kigaidi ni fedheha na junaha kubwa. Hujjatul Islam wal Muslimin Kadhim Siddiqi amesema hayo mbele ya hadhara ya waumini waliohudhuria ibada ya Sala ya Ijumaa mjini Tehran na kusisitiza kwamba, hatua hiyo ni aibu na fedheha kubwa kwa Umoja wa Ulaya.

Sheikh Kadhim Siddiqi amebainisha kwamba, uamuzi huo wa Umoja wa Ulaya ni kinyume cha sheria na dhidi ya maadili na kuongeza kuwa, utakuwa utangulizi wa fedheha kubwa zaidi ya umoja huo na katu haiwezi kuwa na taathira yoyote mbaya kwa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya mjini Tehran amesema, kuiweka Hizbullah katika orodha ya makundi ya kigaidi na kuuacha utawala wa Kizayuni wa Israel ambayo ni serikali ya kigaidi ni junaha na fedheha kubwa kwa Umoja wa Ulaya. Habari kutoka http://kiswahili.irib.ir/habari/habari/item/33603-siddiqi-uamuzi-wa-eu-dhidi-ya-hizbullah-ni-fedheha