EU YAKOSOLEWA KWA KUIWEKA HIZBULLAH KATIKA ORODHA YA MAIDI.


Shakhsia mbalimbali diniani wameendelea kuonesha upinzani wao mkubwa dhidi ya uamuzi wa Umoja wa Ulaya (EU) wa kuiweka harakati ya Hizbullah katika orodha yake ya makundi ya kigaidi.

Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa suala muhimu kwa harakati hiyo ni kwamba inaungwa mkono na wananchi wa Lebanon, mataifa ya Kiarabu na ulimwengu wa Kiislamu.

Sayyid Hassan Nasrullah ambaye alikuwa akijibu hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuiweka Hizbullah katika orodha yake ya makundi ya kigaidi, alisema jana jioni katika karamu ya futari iliyotayarishwa na Kamati ya Ulinzi ya Muqawama wa Kiislamu mjini Beirut kwamba, wanamapambano wa Hizbullah wamebadili kanuni za mapigano, wakabatilisha mipango ya adui na kukomboa mateka na ardhi za Lebanon zilizokuwa katika makucha ya Wazayuni na wataendelea kuwa mwiba katika jicho za Israel.

Sayyid Nasrullah amesema Hizbullah haikushangazwa na hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuiweka katika orodha yake ya makundi ya kigaidi, kwani uamuzi huo ulikuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu, na kwamba jambo la kushangaza ni kuchelewa uamuzi huo.

Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema Umoja wa Ulaya (EU) unatumikia maslahi ya Israel na kwamba, umoja huo umetwishwa maamuzi hayo kwa sababu yanapingana na thamani za nchi za Ulaya. Amesema wale wanaodhani kwamba Hizbullah ambayo ilitoa kipigo kikali kwa wavamizi wa Kizayuni hususan katika vita vya siku 33 hapo mwaka 2006 itasalimu amri mbele ya uamuzi huo usio na thamani yoyote, ama wanaota au ni majahili.

Mwishoni mwa hotuba yake, Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza tena kuwa, harakati hiyo ya mapambano itaendelea kuwepo na itashinda kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu.

Radiamali kali ya fikra za waliowengi nchini Lebanon, katika nchi za Kiarabu na ulimwengu wa Kiislamu dhidi ya uamuzi huo wa Umoja wa Ulaya imeonesha kuwa, watu hao hawakuathiriwa na propaganda chafu za utawala wa Kizayuni wa Israel na witifaki wake. Si hayo tu, bali hatua hiyo ya Umoja wa Ulaya itazidisha chuki na hasira za waliowengi katika Mashariki ya Kati na kwenye Umma wa Kiislamu dhidi ya umoja huo.

Hapana shaka kuwa, kufeli kwa utawala wa Kizayuni na mafanikio ya mara kwa mara ya Hizbullah yameutia wasiwasi mkubwa utawala ghasibu wa Israel na waitifaki wake wa Kimagharibi.

Katika hali kama hiyo Israel na nchi hizo za Ulaya zimeamua kuchukua hatua kama hizo za kuiweka Hizbullah katika makundi eti ya kigaidi ili kuficha kushidwa kwa utawala huo haramu kwa upande mmoja, na kulipiza kisasi dhidi ya wanamapambano wa Hizbullah katika upande wa pili. Hii ni pamoja na kuwa, kwa hatua hiyo, Umoja wa Ulaya unataka kuzipotosha fikra za walimwengu kuhusu sura na hakika ya kigaidi ya Israel na kuhusu misaada yake kwa makundi mbalimbali ya kigaidi ya Mashariki ya Kati hususan huko Syria.

Alaa Kulli hal, Hizbullah imethibitisha kuwa, daima umekuwa ngome imara mbele ya chokochoko zote za utawala ghasibu wa Israel na vitimbi vya nchi za Magharibi ambazo zimetambua kuwa, wanamapambano wa Hizbullah ni kisiki kikubwa kinachokwamisha malengo yao machafu katika eneo hili. Habari kutoka http://kiswahili.irib.ir/uchambuzi/item/33574-eu-yakosolewa-kwa-kuiweka-hizbullah-katika-orodha-ya-maidi