ARAQCHI: ISRAEL SI UTAWALA WA KUZUNGUMZA NAO.


Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kimsingi utawala wa Kizayuni wa Israel hauna sifa ya kufanya mazungumzo kwani muundo na historia yote ya utawala huo imesimama juu ya vita, ukandamizaji, ubeberu na kutokubali msimamo wa upande wa pili.

Sayyid Abbas Araqchi amesema hayo wakati akijibu swali kuhusu harakati za hivi karibuni za Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani katika eneo hili la Mashariki ya Kati za kutaka kuanzisha tena mazungumzo kati ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuongeza kuwa, uzoefu unaonesha kwamba utawala pandikizi wa Kizayuni kimsingi hauna sifa ya kukubali suluhu na amani kwani dhati yake ni utawala unaopenda vita.

Amma kuhusiana na makubaliano yoyote yale yanayoweza kufikiwa kwa ajili ya kufufua mazungumzo hayo ikiwa ni pamoja na makubaliano ya kubadilishana ardhi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, suala hilo si tu lina maana ya kudharau haki ya kurejea nyumbani wakimbizi wa Kipalestina, lakini pia ni sawa na kuhalalisha kufukuzwa Wapalestina katika maeneo yao huko kwenye ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Vile vile amesema inashangaza kuona mpango huo haukuashiria hata kidogo masuala ya kimsingi kama vile suala la Quds tukufu na haki ya kurejea nyumbani wakimbizi wa Kipalestina na kwamba kufanya mazungumzo na Wazayuni ni kupoteza wakati.

Vile vile amesema kuwa, mazungumzo yoyote yale hayatakuwa na faida ila yatakapozingatia mambo ya kimsingi kama vile kuacha Wazayuni kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina, kupewa haki Wapalestina kujiainishia wenyewe mambo yao, kurejea wakimbizi wa Palestina kwenye ardhi za mababu zao na kuundwa serikali kubwa na yenye nguvu ya Palestina mji mkuu wake ukiwa ni Baytul Muqaddas. Habar kutoka http://kiswahili.irib.ir/habari/iran/item/33495-araqchi-israel-si-utawala-wa-kuzungumza-nao