UHARAMU NA UHALALI WA KANZU NDEFU NA FUPI.

Bismillah Rahmanr Rahiim
 
Mawahhab (ANSWARU SUNNA) kwa kutaka kuwababaisha Waislam wasio kuwa na ujuzi wa kutosha wanasema kuwa mtu yeyote atakayevaa nguo ndefu iwe Kanzu au Suruali ataingia Motoni. Ukiingia Misikitini utawakuta watu wazima wenye akili timamu wamenunua Kanzu nzuri na Suruali na kisha wamezikata zimebaki kama Kaputula. Kwa kukazia uhalali wa imani hiyo wanaweka mbele yetu Hadithi sahihi ya Bwana Mtume (s.a.w.w) iliyopokewa na Maimamu Bukhar na Muslim ya kwamba: "Yeyote atakaye ivuta (kuburuza) nguo yake kwa kiburi Mwenyezi Mungu hatomtazama siku ya Kiyama" (Bukhar na Muslim).

Katika Hadithi nyingine Bwana Mtume (s.a.w.w) amesema tena:-
"Jiepushe na kuburuza shuka kwani ni katika kujifaharisha na hakika Mwenye Mungu hawapendi wenye kujifaharisha."
Mtu yeyote mwenye ufahamu wa kawaida tu hawezi kuelewa kuwa Bwana Mtume (s.a.w.w) kwa maneno hayo alikataza Waislam kuvaa nguo ndefu. Bali kilichokatazwa katika Hadithi hiyo ni kuvaa nguo ndefu kwa kiburi na ghururi. Katika Hadithi hiyo kuna sharti linalodhamini kupatikana uharanu wa kuvaa nguo ndefu, nalo ni pale Bwana Mtume (s.a.w.w) aliposema: "Yeyote atayevaa nguo ndefu kwa kiburi (kujionyesha)." Hii inamaanisha ya kuwa yule ambaye hakuvaa kwa ajili ya majivuno na kiburi bali ni mapenzi yake kuvaa nguo ndefu haiwezi kuwa haramu kwake kwa ushahidi usiopingika.

Bwana Mtume (s.a.w.w) alipotamka maneno haya mbele ya Masahaba wake Sayyidna Abubakr alimwambia kuwa hata yeye nguo zake zinaburuza chini na akahofia onyo hilo la Bwana Mtume (s.a.w.w) lisimkumbe naye. Hadithi ifuatayo iliyopokewa na Imam Bukhar inasema kuwa:
"Yeyote atakayeivuta (kuburuza) nguo yake kwa kujionyesha Mwenyezi Mungu hatomwangalia siku ya Kiyama. Akasema Abuka, upande mmoja wa shuka yangu unaburuza mpaka niushike, akasema Bwana Mtume (s.a.w.w) "wewe si katika wafanyao hivyo kwa kujifaharisha" (Imam Bukhar).

Wafasiri wa Hadithi wanasema kuwa maelezo ya Bwana Mtume (s.a.w.w) kwa Abubakr ambaye nguo zake zilikuwa zikiburuza chini hadi inamlazimu kuzishikilia ya kwamba yeye hahusiani na wale wanaoburuza nguo kwa kibri, yanaonyesha wazi kuwa si haramu kuvaa nguo ndefu kwa kuwa kuvaa huko si kwa kiburi. Hata hivyo ingawa haikatazwi kwa mujibu wa Hadithi hiyo sahihi, lakini si jambo linalopendeza sana kwani upo ushahidi mwengine unaoelezea aina ya nguo inayofaa kwa Mwislam ni baina ya magoti na miundi yaani fundo za chini miguuni. Nguo isizidi mafundo ya miguu kwenda chini.

DALILI ZA KIAKILI:-

Miongoni mwa tunu muhimu kabisa kwa Mwanadamu toka kwa Mwenyezi Mungu ni kujaaliwa kuwa na akili. Mtu asiyekuwa na akili hatohukumiwa na Mwenyezi Mungu. Tujadili kiakili juu ya uvaaji wa Kanzu. Kwanza kabisa Kanzu ni nguo ya asili ya Kiarabu. Kwa kuwa Bwana Mtume (s.a.w.w) alikuwa Mwarabu naye pia alivaa nguo hizo na kwetu Waislam ni Sunna kuvaa vazi hilo. Kwa vyovyoye vile sisi Waafrika hatuwezi kulijua vazi hilo kuliko Waarabu.
Katika nchi nyingi za Kiarabu kama Saudi Arabia, Imaraati, Oman, Qatar, Iraq, Kuwait, Bahrein, Libya, Algeria na nchi nyingine kadhaa za Kiislam hakuna Waislam wanaokata Kanzu zao mpaka zinabaki kama Vimini wanavyovaa baadhi ya Waislam hapa Afrika Mashariki. Tuseme nchi zote hizo Waslam na Masheikh zao hawajui kuwa Kanzu kwa mujibu wa Uislam ni lazima ikatwe ibaki kuwa nusu (kama kimini).?
Kioja kingine ni kile kufunga Swala kama wafungavyo Wakristo wanapoungama dhambi mbele ya Makasisi wao. Katika dunia ya leo ya Sayansi na Teknolojia tunaona kila siku moja kwa moja Swala ya Magharib ya Madina na Ishaa ya Makkah. Maimamu wanafunga Swala kama tufungavyo Waislam wote, wala hawapanui miguu kuziba nafasi kwa Waumini wengine na wala hatujapata kumwona Imam wala Maimamu aliyekata Kanzu kipande.

Swali:-
Je hii ina maana Mawahhab (ANSWARU SUNNA) wa hapa Afrika Mashariki ndio wajuzi zaidi kuliko Waislam wote duniani.?