MSIMAMO WA MWANA AISHA DHIDI YA IMAM ALI BIN ABI TALIB (A.S).

Bismillah Rahmanr Rahiim.

Kwa mtafiti yeyote juu ya msimamo wa Mwana Aisha dhidi ya Imam Ali bin Abi Talib (a.s), atakuta mambo ya ajabu na ya kushangaza na hataweza kupata tafsiri yoyote kwa mambo hayo isipokuwa ni wivu na uadui dhidi ya watu wa nyumba ya Bwana Mtume (s.a.w.w).
Historia imezisajili chuki na bughudha za Mwana Aisha kwa Imam Ali bin Abi Talib (a.s), chuki ambazo hazina mfano, na zilifikia kiasi cha Mwana Aisha kushindwa hata kulitamka jina la Imam Ali bin Abi Talib (a.s) 65 na wala hataki hata kumuona, na aliposikia kuwa watu wamempa baia Imam Ali bin Abi Talib (a.s) kuwa Khalifa baada ya kuuawa Uthman akasema: "Natamani lau mbingu ingeifunika ardhi kabla hajaukalia Ukhalifa Mtoto wa Abi Talib." Hapo ndipo Mwana Aisha alipofanya kila njia kumuangamiza Imam Ali bin Abi Talib (a.s) na akaongoza jeshi kubwa ili kupambana na Imam Ali bin Abi Talib (a.s) na hatimaye zilipomfikia habari kwamba Imam Ali bin Abi Talib (a.s) amefariki alisujudu sijda ya kumshukuru Mwenyezi Mungu.
Je, kwa nini hamuwashangai pamoja nami Masunni ambao wanasimulia ndani ya vitabu vyao kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) amesema: "Ewe Ali hatakupenda isipokuwa Muumini na hatakuchukia isipokuwa mnafiki." 66 kisha wanasimulia ndani ya Sahih zao na Musnad zao na vitabu vyao vya historia kwamba bibi Aisha akimchukia Imam Ali bin Abi Talib (a.s) kiasi cha kushindwa hata kulitamka jina lake.
Basi je, huo si ushahidi unaotaka kwao juu ya hali halisi ya Mwanamke (huyu)? Kama ambavyo Bukhar anavyosimulia ndani ya Sahih yake kwamba, Mtume (s.a.w) amesema: "Fatma ni sehemu itokanayo nami, yeyote mwenye kumkasirisha (atakuwa) kanikasirisha mimi, na mwenye kunikasirisha mimi basi hakika kamkasirisha Mwenyezi Mungu. 67
Kisha Bukhar huyo huyo anasimulia kwamba, Fatma alikufa hali ya kuwa amemkasirikia Abubakr na mpaka amefariki hakumsemesha. 68 Je, huo sio ushahidi utokanao na wao (Ahlul-Sunnah) kwamba Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamemkasirikia Abubakr? Ukweli unafahamika kwa kila mwenye akili.
Ndiyo maana mimi siku zote nasema kwamba, ukweli hapana budi uonekane japokuwa watu waovu watauficha na kwa namna yoyote (ukweli utadhihiri) japokuwa watetezi wa Banu Umayyah watajaribu kuuvuruga, kwani hoja ya Mwenyzi Mungu imesimama juu ya waja wake tangu siku Qur'an iliposhuka mpaka siku ya Kiyama "Kila sifa njema anastahiki kusifiwa Mwenyezi Mungu Mola wa Walimwengu."
Imam Ahmad ibn Hambal anasimulia kwamba, "Siku moja Abubakr alikuja na kubisha hodi kwa Mtume (s.a.w.w), na kabla hajaingia alisikia sauti ya Mwana Aisha imeparama juu anamwambia Mtume (s.a.w.w), Wallahi mimi nafahamu kwamba, Ali unampenda mno kuliko mimi na baba yangu." Alikariri maneno hayo mara mbili au tatu......69
Mambo ya Mwana Aisha na chuki yake dhidi ya Imam Ali bin Abi Talib (a.s) yalifikia kiasi kwamba siku zote Mwana Aisha alikuwa akijaribu kumtenganisha Ali na Mtume (s.a.w.w) kwa njia zotezote anazoziweza.
Na amesimulia Ibn Abil-hadid kwamba, Mtume wa Mwnyezi Mungu (s.a.w) siku moja alimsindikiza Imam Ali bin Abi Talib (a.s), basi mazungumzo yao yakawa marefu, na bibi Aisha alikuwa akija nyuma yao mpaka akaingia katikati yao na akawaambia mnazungumza nini nyie mbona mmerefusha (mazungumzo)? Mtume alikasirika kutokana na (tendo) hilo. 70
Vile vile amesimulia kwamba bibi Aisha wakati fulani alimwendea Mtume (s.a.w) hali yakuwa anazungumza na Ali, akapiga kelele na akasema, "Kuna nini baina yangu mimi na wewe ewe mwana wa Abu Talib" Hakika mimi ninayo siku moja tu kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu." Mtume (s.a.w.w) alichukia sana.
Ni mara nyingi bibi Aisha amemchukiza Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kwa matendo yake yanayotokana na wivu mkali, tabia yake ngumu na maneno yake yanayoudhi.
Je, hivi ni kweli Mtume wa Mwenyezi Mungu anamridhia Muumini Mwanaume au Muumini wa kike ambaye moyo wake umejaa chuki na Bughudha dhidi ya mwana wa Ammi yake na Bwana wa kizazi chake ambaye Mtume amesema: "Anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanampenda."71
Na akasema Bwana Mtume (s.a.w.w) juu ya Imam Ali bin Abi Talib (a.s): "Yeyote mwenye kumchukia Ali basi bila shaka kanichukia mimi." 72

_____________________________
65- Sahih Bukhar J.1 Uk.162 na J.3 Uk.135 na J.5 Uk.140.
66- Sahih Muslim J.1 Uk.61, Sahih Tirmidhi J.5 Uk.306, Sunan Nassai J.8 Uk.116.
67- Sahih Bukhar J.4 Uk.210.
68- Sahih Bukhar J.5 Uk.82 na J.8 Uk.3.
69- Imam Ahmad ndani ya Musnad yake J.4 Uk.275.
70- Shar-Nahjul-Balagha ya Ibn Abil Hadi J.9 Uk.195.
71- Sahih Bukhar na Muslim katika mlango wa fadhila za Ali ibn Abi Talib J.7. Uk.130.
72- Mustadrak Al-Hakim J.3 Uk.130.