MAREKANI YACHUKIZWA NA MAFANIKIO YA JESHI LA SYRIA.

Seneta wa chama cha upinzani cha Republicans nchini Marekani, John McCain ameelezea kuchukizwa kwake na mafanikio ya jeshi la Syria dhidi ya makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Washington na waitifaki wake.

McCain ameiambia kanali ya televisheni ya CBS kwamba serikali ya Rais Barack Obama inafaa kuingilia kati mara moja la sivyo, Rais Bashar al Assad atazima kabisa nguvu za magaidi hao na kwamba hilo litakuwa pigo kubwa kwa ikulu ya White House.

Wiki iliyopita, seneta huyo aliingia kinyemela huko Syria na kukutana na viongozi wa makundi ya waasi wenye silaha, jambo lililodhihirisha wazi uhusiano uliopo kati ya Marekani na makundi hayo ya kigaidi.

Huku hayo yakijiri, habari zinasema kuwa jeshi la Syria limeendelea na oparesheni kali za kuwasaka magaidi katika mji wa Qusayr na kwamba magaidi kadhaa wa kundi la Jabhat an-Nusra wameuawa.

Kwa upande mwingine magaidi wa Syria wamejaribu kumuua kamanda mmoja wa harakati ya Hizbullah kwa madai kwamba harakati hiyo inamsaidia Rais Bashar Asad. Watu wenye silaha wamefyatulia risasi gari la kamanda huyo ingawa hawakufanikiwa kumuua au hata kumjeruhi.