Hii ni makala inayozungumzia malengo ya kubaathiwa Mtukufu Mtume Muhammad (S.AW.W) kwa mtazamo wa Imam Khomein (MA).,
Tarehe 27 Rajab mwaka wa tembo na akiwa na umri wa miaka 40, Mtume Muhammad (S.AW.W) alikuwa juu ya kilele cha Mlima Hira akijishughulisha na ibada ndani ya pango la mlima huo, ambapo ghafla malaika Jibril alimteremkia huku akiwa amebeba wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Alikuwa amebeba ujumbe wa bishara ya utume kwa Mtume Mtukufu (S.AW.W), ambapo alianza kumsomea aya za mwanzoni za Surat Alaq zisemazo: "Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba. Amemuumba Mwanadamu katika pande la damu. Soma, na Mola wako ni Mtukufu mno. Ambaye amefunza (kuandika) kwa kalamu. Amemfunza mwanadamu asilolijua." Kwa utaratibu huo, wahyi na utume, vikawa vimeanza kwa jina la Mwenyezi Mungu na kusoma kwa kalamu, yaani mafundisho yaliyojumuisha Tawhid. Wapenzi wasikilizaji, huku tukikupeni mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa kuwadia iddi tukufu ya kubaathiwa Mtukufu Mtume Muhammad (S.AW.W), Mtume wa rehema, na tukiwa katika siku hizi za kukumbuka kufariki dunia Imam Khomein (MA), ninakuombeni mjumuike nami, ili tuweze kutupia jicho mtazamo wa shakhsia huyo wa Kiislamu kuhusiana na malengo ya kubaathiwa Mtume (S.AW.W).
Kubaathiwa kuna maana ya kusimama na kuwa tayari kwa ajili ya kutenda kazi fulani. Na siku ya 'Mab'ath ni siku ambayo, Mtume wa Uislamu Muhammad (S.AW.W), alipewa rasmi Utume. Kutumwa Mtume (S.AW.W) ulikuwa mwanzo wa kumuokoa mwandamau kutokana na shirki, kutenda vitendo vilivyo kinyume na uadilifu, ubaguzi, ujinga na ufisadi na kumuongoza kwenye tawhid, umaanawi, uadilifu na utukufu. Aidha kubaathiwa, kuliambatana na kuanza mwamko wa kimaanawi na kuleta mapinduzi katika ulimwengu wa mwanadamu mapinduzi ambayo athari zake bado zinaendelea hadi leo. Mabadiliko haya ya kiroho, yaliwaongoza wanadamu waliokuwa wakiabudu masanamu na kuwaelekeza kwenye chimbuko la maumbile na kuwaonya dhidi ya kufanya matendo machafu, huku yakiwataka wafanye matendo mema. Siku ya kubaathiwa Mtume Muhammad (S.AW.W), ulikuwa ni mwanzo wa kumuondoa mwanadamu kutoka katika giza kuelekea kwenye nuru. Ni kwa ajili hiyo ndipo Imam Khomein (MA) akaitaja siku hiyo ya kubaathiwa babu yake Mtukufu Mtume Muhammad (S.AW.W) kuwa ni siku tukufu zaidi ulimwenguni. Kwa mtazammo wa Imam Khomein, siku ya kubaathiwa Mtume wa Mwisho (S.AW.W), hailinganishwi na siku nyingine yoyote ile, wala siku za kubaathiwa Mitume wengine Watukufu wa Mwenyezi Mungu. Aidha Imam Khomein amesisitizia kuhusiana na suala hilo kwa kusema kuwa, siku ya kubaathiwa Mtume Muhammad ni siku kubwa ambayo haina mfano wake na wala hapatatokea siku nyingine kama hiyo katika mustakbali. Ni siku ya kubaathiwa Mtume aliyediriki daraja zote za kinafsi na za mbinguni, na akafahamu sheria zote za dhahiri na batini. Kwa ajili hiyo, hakuna haja ya kutumwa ujumbe au Mtume mwingine baada yake.
Kwa hakika kubaathiwa ni bishara ya utakaso wa wanadamu wanaostahiki, na waliotakasika kutokana na machafu. Katika mtazamo wake wa awali kuhusiana na kadhia ya kubaathiwa, Imam Khomein (MA), amelitaja neno la 'tazkiya' yaani utakaso kuwa moja ya nguzo muhimu katika harakati adhimu ya kumkurubia Mwenyezi Mungu. Neno hilo pia lina maana ya kumiliki sifa njema na kurekebisha mienendo yote ile isiyo sahihi sambamba na kutokomeza sifa mbaya. Kwa hakika ‘tazkiya’ huanza kwa mja kusafisha na kutakasa dhati yake na kisha kumalizika kwa ukamilifu wa shakhsia ya mtu binafsi. Ni kwa ajili hiyo, ndipo Imam Khomein (MA) sambamba na kubainisha suala la tazkiya, kuwa lenye umuhimu wa aina yake katika malezi ya tabia njema ya watu katika jamii ya mwanadamu, akalitaja pia neno hilo kuwa moja ya malengo makubwa. Kwa mtazamo wa mtukufu huyo, tazkiya haina maana ya kubaathiwa Mtume kwa ajili ya taifa, kizazi na tabaka fulani tu la watu, wala ukomo wa historia na eneo maalumu la kijografia.
Aidha Imam Khomein (MA) amefafanua zaidi kuhusiana na utakaso wa nafsi ambao ndio lengo kuu la kutumwa na Mwenyezi Mungu, Mtume Mtukufu kwa kuashhiria aya ya 2 Surat Al-Jumua inayosema: “Yeye ndiye aliye mpeleka Mtume kwenye watu wasiojua kusoma, awasomee Aya zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri.”
Kwa mujibu wa aya hii, Mwenyezi Mungu Mtukufu, alimteua Mtume na kumpa majukumu ya kazi maalumu ambazo ni pamoja na kuteremshiwa Qur’ani na kuwasomea wanadamu Kitabu hicho Kitukufu. Qur’ani Tukufu ni mfano wa chakula kilichoandaliwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wanadamu kupitia Mtume wake (S.AW.W) ambapo kila mwanadamu ana fursa ya kunufaika nacho kadiri ya uwezo wake. Kuhusiana na suala hilo, Imam Khomein (MA) anasema: “Lengo la kubaathiwa Mtukufu Mtume (S.AW.W) lilikuwa ni kuwaandalia wanadamu karamu ya chakula kuanzia kipindi cha kuteremka Qur’ani hadi zama za mwisho. Mtume alipewa jukumu la kusoma Kitabu hicho kwa madhumuni ya kumtakasa mwanadamu na kumfundisha Kitabu hicho cha hekima. Kwa hivyo lengo la kubaathiwa Mtume na kuteremka Qur’ani lilikuwa ni kumtakasa mwanadamu na kumuondoa kwenye machafu aliokuwa amezama ndani yake." Aidha Imam Khomein anafafanua zaidi ukweli huo kwa kusema: “Ufundishaji wa Kitabu hicho na hakima ni mambo ambayo hayawezekani bila ya kuwepo utakasaji. Nuru hii ya Mwenyezi Mungu haiwezi kumulika kwenye moyo wa mtu kabla ya mtu huyo hajajiondoa katika uzio wa machafu, dimbwi la matamanio ya nafsi, dimbwi la kujiona wala kabla hajayaondoa machafu ambayo yamepenya ndani ya nafsi yake.”
Tazkiya ambayo ndio lengo kuu la kubaathiwa Mtukufu Mtume (S.AW.W), ina maana ya kuondoka katika kiza la nafsi na kupambana na matamanio na vishawishi vyote vya ndani kwa ajili ya kuingia katika anga ya usafi wa kimaanawi. Kwa mtazamo wa Imam Khomein (MA), chanzo cha tofauti na migogoro yote ambayo inashuhudiwa leo katika jamii ya mwanadamu, kinatokana na upinzani ambao unapatikana katika nafsi za wanadamu. Chanzo cha kuchupa mipaka na kuzuka tofauti kati ya wanadamu, hutokana na nafsi za wanadamu kutotosheka wala kukinai. Kwa hakika suala hilo, hupatikana katika matabaka yote ya watu, wakiwamo wafanyakazi, watu wa vijijini na hata viongozi wenye madaraka ya juu. Hakuna shaka kwamba, kukosekana utakaso wa nafsi kwa viongozi, ni jambo lenye hatari kubwa. Kuhusiana na suala hilo, mtukufu huyo anasema: “Ikiwa watu wa kawaida hawatajitakasa na wakafanya maovu, madhara ya uovu wao huwa na ukomo maalumu. Ikiwa mtu mmoja atafanya uovu sokoni au katika kijiji, inawezekana uovu huo ukawa na athari kwa kiasi fulani tu, lakini ikiwa uovu huo utafanywa na mtu ambaye amekubalika na watu, msomi ambaye watu wamekiri ujuzi wake, kwa viongozi ambao watu wamekubali uongozi wao, kwa watawala ambao watu wamekubali utawala wao, basi wakati huo nchi itakabiliwa na uharibifu. Hii ni kwa sababu mtu aliyeshika hatamu za uongozi hajatakasika.”
Sura ya kwanza iliyoshuka kwa Mtume Muhammad (S.AW.W) na kuthibitisha Utume wake ni Surat Alaq. Aya ya 7 na 8 za sura hiyo zinasema: “Si hivyo! Hakika mtu bila ya shaka huwa jeuri. Akijiona katajirika.” Kwa ajili hiyo Imam Khomein anaashiria sehemu ya pili kuhusiana na maudhui ya uasi wa mwanadamu na kusema: “Hali hiyo inawahusuza wanadamu wote, ambapo mtu hufanya uasi wakati tu anapijiona katosheka. Mtu huasi kwa kiwango cha utajiri, elimu au madaraka aliyonayo. Hivyo lengo la kubaathiwa Mtume Mtukufu, lilikuwa ni kutuokoa kutokana na uasi na kututakasa.” Mambo yanayomfanya mwanadamu ahisi kuwa anajitosheleza na kuwa si muhitajia tena na hivyo kumfanya atende uasi mwingi, ni mengi. Moja ya mambo hayo ni pamoja na elimu, madaraka, mali, uchumi na siasa.
Aidha Imam Khomein (MA) alikutaja kuondoa dhuluma, kuwa lengo jingine la kubaathiwa Mtukufu Mtume (S.AW.W). Kuhusiana na suala hilo anasema: “Sababu nyingine ya kubaathiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ilikuwa ni kuwafahamisha wanadamu njia ya kuondoa dhuluma ili kuwafanya waweze kukabiliana na nguvu kubwa za istikbari duniani. Utume pia ulikuwa na madhumuni ya kuokoa akhlaqi za wanadamu, roho za wanadamu, miili ya wanadamu na kila kitu cha mwanadamu, kutokana na dhulma. Utume pia ulikuwa na lengo laa kuwafanya wanadamu wajisafishe na kila aina ya madhambi na machafu na kuweka mahala pake nuru, waachane na dhuluma na ujinga na kuweka nuru ya elimu pahala pake na wajitenge na dhulma na ukandamizaji na kuweka pahala pake nuru ya uadilifu…. ”
Wapenzi wasikilizaji, muda uliopangiwa kipindi hiki, umefika ukingoni. Msikose kusikiliza makala mengine ya wiki katika siku na saa kama hizi. Mtayarishaji na msomaji wa kipindi hiki, kama kawaida ni mimi Sudi Jafar Shaban, hadi wakati huo, ninakuageni kwa kusema, kwa herini.