KUKOMBOLEWA KIKAMILIFU MJI WA KISTRATIJIA WA AL-QUSAYR NA JESHI LA SYRIA.

Hatimaye baada ya siku kadhaa za mapigano makali jeshi la Syria jana lilifanikiwa kuukomboa mji wa kistratijia wa al Qusayr ulioko kwenye mkoa wa Homs kutoka kwenye udhibiti wa makundi ya kigaidi yaliyoko nchini humo. Kwa mujibu wa duru za habari sambamba na kusonga mbele kwa kasi majeshi ya Syria makundi ya kigaidi yameukimbia mji huo. Mji wa al Qusayr wenye wakaazi wapatao elfu 25 ulikuwa ukitumiwa na magaidi kama kituo kikuu cha kupitishia silaha kimagendo kutokea Lebanon na vilevile ulikuwa ngome yao ya mashambulizi dhidi ya harakati za jeshi la Syria kutokea mji mkuu Damascus kuelekea pwani ya magharibi mwa nchi hiyo. Kwa kuzingatia umuhimu wa mji huo magaidi wanaotoka mataifa kadhaa na wanaozatitiwa kwa silaha na madola ya Magharibi walizichoma moto nyumba; na kwa kutumia aina mbalimbali za silaha walikuwa wakiwatumia watu kama ngao dhidi ya mashambulizi ili kuvizuia vikosi vya jeshi la Syria visiweze kusonga mbele.
 

Tangu mwezi Machi mwaka 2011 na kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani, Uingereza, Qatar, Uturuki, Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel, makundi ya kigaidi yameanzisha machafuko katika baadhi ya miji ya Syria kwa lengo la kuudhoofisha mhimili wa muqawama na kuiangusha serikali ya nchi hiyo; na yakajaribu kufanya kila njia za hujuma na mauaji ya kinyama ya raia ili kuandaa mazingira kwa madola ya kigeni ya kuingilia kijeshi nchini Syria.
 

Katika uga wa siasa za kimataifa, AlexeiBorodavkin, mwakilishi wa kudumu wa Russia katika makao ya Umoja wa Mataifa huko Geneva amelikosoa azimio lililotolewa na Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo dhidi ya Syria na kusema kuwa ni la kisiasa. Aidha amelikosoa azimio hilo kwa kutoashiria athari haribifu za kiuchumi ilizopata Syria na maafa ya kibinadamu yaliyotokea nchini humo.AlexeiBorodavkin ameongeza kuwa ni jambo la kushangaza kwamba wajumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa hawakuwafanya mawasiliano yoyote na jamaa na manusura wa watu waliouliwa katika jinai dhidi ya binadamu zilizofanywa na makundi ya upinzani na ya kigaidi nchini Syria katika maeneo ya Khan Asal-Qusayr, Homs na Aleppo. Mwakilishi wa kudumu wa Russia katika makao ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva amesema matumaini yake ni kwamba, katika ripoti yake ijayo kuhusu Syria, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa litafanya tathmini yakinifu na inayowiyana na uhalisia wa mambo kuhusiana na matukio ya nchi hiyo.
 

Wakati huo huo utawala wa Kizayuni wa Israel, Marekani na Uingereza zimekiri kuwa mpango wa kuiangusha serikali ya Syria umegonga mwamba. Toleo la siku ya Jumanne la gazeti la al Manar limeandika kuwa vyombo vya usalama vya Israel na vilevile vyombo vya intelijinsia vya Marekani na Uingereza vinaitakidi kwamba serikali ya Syria imeshaivuka awamu ya kuweza kuangushwa. Tangu mwaka 2011 Syria imetumbukia kwenye lindi la mgogoro wa umwagaji damu ulioanzishwa na madola ya Magharibi na baadhi ya nchi za eneo; na hivyo kukombolewa mji muhimu wa al Qusayr unahesabiwa kuwa ni ushindi wa kistratijia kwa jeshi la nchi hiyo.