IMAM MAHDI (A.S).


Mtume Muhammad (s.a.w.w) amesema:
"Sisi Ahlul-Bayt Mwenyezi Mungu ametuchagulia Akhera dhidi ya dunia, hapana shaka watu wa nyumba yangu baada yangu watakumbana na balaa kubwa na kufukuzwa mpaka waje watu fulani toka upande wa mashariki wakiwa na bendera nyeusi, wataomba amani hawatapewa, basi watapigana na watashinda, hivyo watapewa walichokiomba lakini hawatakikubali mpaka wakitoe kwa mtu miongoni mwa watu wa nyumba yangu, basi yeye atakijaza usawa kama kilivyojazwa ujeuri." Sunan ibn Majah J.2. hadith namba 4082 na 4087

"Mahdi ni kutokana nasi Ahlul-Bayt, Mahdi ni miongoni mwa watoto wa Fatma"

Pia amesema Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kuwa:
"Katika Umma wangu atakuwepo Mahdi (atabaki) kama ni miaka midogo basi ni Saba au Tisa Umma wangu utaneemeka humo neema ambayo haukupata kuneemeka mfano wake, utajiwa na chakula chake wala hawatokuwa wanahodhi kitu, mali zitakuwa tele siku hizo, mtu atamwambia Mahdi, Ewe Mahdi! nipe, atamwambia chukua."

Rejea: Sunan ibn Majah J.2 hadith namba 4086.

Tenaameendelea kusema Mtukufu Mtume (s.a.w.w):
"Atatawala mtu toka katika watu wa nyumba yangu, jina lake linalingana na jina langu, na lau haitabaki katika dunia isipokuwa siku moja, basi Mwenyezi Mungu atairefusha siku hiyo mpaka atawale."

Rejea: Al-Ja'mius-Sahih J.9 Uk.74 - 75.

Na Al-Hafidh ndani ya Fat-Hu-Bari amesema:
"Zimeenea kwa njia ya Mutawatir Khabari zisemazo kwamba Mahdi atatokana na Umma huu, na kwamba Issa mwana wa Maryam atashuka na ataswali nyuma yake."

Rejea: Fat-Hul-Bari J.5 Uk.362.

Baadhi ya Wanachuoni wa Kisunni wanaoheshimika wanaitakidi kwamba Mahdi ni Muhammad bin Al-Hassan Al-A'skari, ambaye ni Imam wa kumi na mbili miongoni mwa Maimamu wa nyumba ya Bwana Mtume (s.a.w.w) amekwisha zaliwa na yupo hai na atadhihiri zama za mwisho na kuujaza ulimwengu uadilifu na usawa na Mwenyezi Mungu atainusuru dini yake kupitia kwake (Mahdi).