Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewanasihi wanaogombea kiti cha urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wawe wakweli na watoe maelezo sahihi katika kampeni zao.
Ayatullahil Udhma S ayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo Jumatano alipokutana na wabunge nchini kwa mnasaba wa kuadhimisha kuasisiwa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani bunge la Iran. Katika hotuba yake amesema kuwa wagombea kiti cha urais wana jukumu zito wanapojitokeza katika radio na televisheni na kwamba wanapaswa kuchukua tahadhari wasitamke maneno yasiyo na ukweli wakati wakijaribu kuwavutia wananchi. Aidha amewanasihi wagombea kiti cha urais wasiharibiane majina. Kiongozi Muadhamu amesisitiza udharura wa wananchi kuwa na ujuzi, kuwa macho na uono wa mbali katika kuainisha ni mgombea yupi bora. Ameendelea kusema kuwa kwa kuzingatia kiwango cha juu cha maarifa na uono wa mbali wa watu wa Iran katika masuala ya kisiasa sambamba na vipindi vya uchaguzi katika radio na televisheni ili kuandaa mazingira ya kubainika mgombea bora zaidi, kuna uwezekano mkubwa wa kufikiwa natija nzuri katika uchaguzi. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekanusha tetesi kuwa anamuunga mkono mgombea fulani katika uchaguzi wa rais. Amesema madai kama hayo hayana ukweli kwani Kiongozi ana kura moja kama watu wengine na hakuna anayejua ni nani atakayepata kura hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi ni jambo ambalo litaandaa mazingira ya kulilinda taifa la Iran sambamba na kudhamini usalama na uwezo wake. Ameongeza kuwa kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi kutasambaratisha vitisho vya maadui. Kiongozi Muadhamu amesema kuwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umejengeka katika msingi wa ushiriki wa wananchi. Kwingineko katika nasaha zake, Ayatullah Khamenei amesisitiza udharura wa kuzingatiwa sheria, maelewano na insafu katika ushirikiano wa serikali na bunge nchini. Habari kutoka http://kiswahili.irib.ir/habari/uchaguzi-iran-1392/item/32248-kiongozi-muadhamu-awanasihi-wagombea-urais-iran