Iran leo imekuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Marafiki wa Syria ambao umefanyika mjini Tehran na kuhudhuriwa na wawakilishi wa nchi 40.
Mkutano huo umefanyika chini ya anwani ya 'Sul uhisho la Kisiasa, Uthabiti wa Kieneo' kwa lengo la kuutafutia suluhisho la kisiasa mgogoro wa Syria. Kati ya waliohudhuria mkutano huo ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq Hoshyar Zebari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria Mourad Medelci, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Yossef Al-Harthi, Rais wa Zamani wa Lebanon Emile Lahoud na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Tanzania Shamsi Vuai Nahodha. Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ali Akbar Salehi ametoa pendekezo la kuundwa Kundi la Mawasiliano la Kimataifa hapa Tehran kwa lengo la kutatua mgogoro wa Syria. Amesema ukosefu wa uthabiti nchini Syria ni jambo ambalo litasababisha maafa na kupelekea kukosekana uthabiti katika eneo na dunia nzima. Salehi ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga suala la kutoa uungaji mkono wa kifedha na kisilaha kwa makundi yanayopigana dhidi ya serikali ya Syria. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na mwakilishi mkuu wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu katika kadhia ya Syria pia wametuma ujumbe katika kikao hicho. Habari kutoka http://kiswahili.irib.ir/habari/iran/item/32247-nchi-40-zashiriki-katika-kikao-cha-syria-tehran