Bismillahir Rahmanir Rahim.
Fatima
Az-Zahrau (a.s) aliishi ndani ya misukosuko ya kufikisha ujumbe tangu utotoni
mwake, akawekewa nikwazo yeye, baba yake, mama yake na Bani Hashim wengine
katika bonde maarufu ilihali wakati vikwazo vinaanza alikuwa na umri wa miaka
miwili tu.
Vilipoondolewa
tu vikwazo baada ya miaka mitatu migumu akakumbana na msukosuko mwengine wa
kufiwa na Mama yake kisha kufariki ami yake huku akiwa mwanzoni mwa mwaka wake
wa Sita, hivyo akabakia kama kifuta machozi cha baba yake akimliwaza wakati wa
upweke huku akimsaidia dhidi ya majeuri na mabeberu ya kikurayshi. Mtukufu
Mtume (s.a.w.w) akahama kuelekea Madina yeye pamoja na Bint yake Fatima huku
wakiambatana na mtoto wa ami yake Ali (a.s), akiwa na umri wa miaka minane,
hivyo akabakia na baba yake mpaka alipokutanishwa na mtoto wa ami yake, Ali bin
Abi Talib (a.s), hapo ikaanzishwa nyumba Tukufu ndani ya Uislam kwani Fatima
alikuwa ni Mwanamke safi wa kuendeleza kizazi kitukufu cha Bwana Mtume
(s.a.w.w) na Kheri nyingi waliyopewa kizazi kitukufu cha Bwana Mtume Muhammad
(s.a.w.w).
Fatima
Az-Zahrau alitoa mfano bora wa Mke na Mama ndani ya kipindi kigumu cha historia
ya Uislam, kipindi ambacho Uislam ulikuwa unataka kuweka njia ya kudumu ya
utukufu wa juu lakini ndani ya Mazingira ya Kijahiliya na mila za Kikabila
zinazokataa Uwanadamu wa Wanawake huku zikimhesabu Mwanamke kuwa ni Aibu. Hivyo
ikawajibika kwa Fatima kutumia mwenendo wake binafsi na wa kijamii ili kuwa
mfano halisi wa kivitendo unaojenga mjengo hali wa mafunzo na hadhi ya ujumbe
wa Mwenyezi Mungu. Fatima Az-Zahrau ameuthibitishia ulimwengu wa Wanadamu kuwa
yeye ni Mwanadamu timilifu ambaye ameweza kuwa alama ya uwezo wa juu wa
Mwenyezi Mungu na Muujiza wake wa ajabu, hivyo ni kutokana na hadhi, heshima na
Tukufu aliokuwa nao. Fatima Az-Zahrau Al-Batul alimzalia Ali bin Abi Talib
(a.s) watoto wawili watukufu wa kiume nao ni mabwana wa Vijana wa Peponi na
watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu: Hassan na Hussein Maimam watukufu, pia
alimzalia Mabinti wawili watukufu: Zaynabu mkubwa na Ummu Kulthum wapiganaji
wawili wenye Subira.
Fatima
Az-Zahrau alimporomosha mwanae wa tano Muhsin baada ya kifo cha baba yake
kutokana na matukuo ya Uadui dhidi ya nyumba yake, nyumba ya utume na Uimam,
hapo zikatimia habari za Qur’an iliposema: “Hakika sisi tumekupa kheri nyingi.
Basi swali kwa ajili ya Mola wako na uchinje. Hakika Adui yako atakuwa mkiwa.”
Hivyo yeye
Fatima Az-Zahrau ndio kheri nyingi ya Utume ambayo Mwenyezi Mungu alimpa Mtume
wake (s.a.w.w), isipokuwa Mtume (s.a.w.w) alikuwa anahitaji wenye kujitolea
atakaowatoa kwa ajili ya mti wake wenye kustawi ili kuwazima Maadui zake ambao
tangu mwanzo walisimama kidete kuuwa Uislam na alama zake.