Rais Mahmoud Ahmadinejad
wa Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran amewataka Waislamu kote duniani kuungana na kuzima njama za
maadui. Rais Ahmadinejad ameyasema hayo leo, katika sherehe za kumalizika kwa
mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya vikosi vya majeshi ya nchi za
Kiislamu, yaliyofanyika mjini hapa Tehran kwa mnasaba wa kuwadia uzawa wa
Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) na wiki ya Umoja.
Akizungumzia udharura wa kuimarishwa umoja
kati ya Waislamu wote duniani Rais Mahmoud Ahmadinejad amesema kuwa, kuibua migongano
na mizozo kati ya Waislamu ni mbinu zinazofanywa na maadui kwa ajili ya kuzusha
mifarakano kati yao.
Amesema kuwa, maadui mara zote wamekuwa
wakifanya njama za kuanzisha mivutano ya kikabila, kikaumu na kimadhehebu na
kuongeza kuwa, pamoja na hayo Qur'ani na Mtume Muhammad ni thamani za Waislamu
wote duniani bali pia ni kwa ajili ya watu wote wakiwemo wafuasi wa dini
tofauti za mbinguni ikiwemo Uyahudi na Ukristo na walimwengu wote kwa ujumla.
Kwa upande
mwingine Rais Mahmoud Ahmadinejad amesema kuwa, moja ya sababu zinazopelekea
kuzushwa mivutano, ni kutokufahamu tafsiri halisi ya Qur'ani na kwamba, suala
hilo kwa muda mrefu limekuwa ndio chanzo cha matatizo kati ya Waislamu. Kutoka http://kiswahili.irib.ir/habari/habari/item/29304-ahmadinejad-asisitizia-mshikamano-wa-waislamu-duniani