MANENO YA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W), JUU YA USHUJAA WA IMAM ALI BIN ABI TALIB (A.S).


Bismillahir Rahmanir Rahim.

Amesema Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w).

“Kesho nitampa bendera yangu mtu anayempenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, naye anapendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, mkali katika mapambano si mwenye kukimbia, Mwenyezi Mungu amekwisha utahini moyo wake kwa imani.”

Masahaba wakaitamani (kuipata) bendera hiyo, Mtume akampa Imam Ali bin Abi Talib (a.s).

Kwa kifupi, bila shaka Maudhui ya elimu, nguvu na Ushujaa, mambo ambayo Imam Ali bin Abi Talib (a.s) amepwekeka kwayo, ni Maudhui inayofahamika kwa wote (Sunni na Shia) na ukiachilia mbali maandiko yanayojulisha kwa uwazi wa kuashiria juu ya Uimamu wa Ali bin Abi Talib (a.s), hapana shaka kwamba Qur’an haikubali Uongozi na Uimamu isipokuwa kwa mtu mwenye elimu, shujaa tena mwenye nguvu.
Mwenyezi Mungu anasema: “Basi aongozaye katika haki ndeye anayestahiki zaidi kufuatwa au (anastahiki) yule asiyeongoka isipokuwa aongozwe, basi mna nini, ni vipi mnahukumu.?” Qur’an: 10:35

Hapa inaonyesha wajibu wa kuwafuata wanachuoni (wenye elimu).
Napia amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu wajibu wa kumfuata mwenye elimu, shujaa tena mwenye nguvu:
“Wakasema, ni vipi atakuwa na Ufalme juu yetu, na hali sisi tunastahiki zaidi kupata Ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali? Akasema, Mwenyezi Mungu amemchagua juu yenu na amemzidishia wasaa wa elimu na kiwiliwili na Mwenyezi Mungu humpa Ufalme wake amtakaye, naye Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa mwenye kujua.” Qur’an: 2:247

Hapana shaka Mwenyezi Mungu Mtukufu amemzidishia Imam Ali (a.s) wasaa wa elimu kuliko Masahaba wote, akastahiki kuwa ni “Mlango wa elimu” akawa ndiye rejea pekee kwa Masahaba baada ya kufariki Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) nao Masahaba walikuwa kila wanaposhindwa kutatua mambo husema “Mas-ala haya magumu hakuna ayawezaye isipokuwa Abul-Hassan.”
Rejea: Manaqibul-Khawar-Zami Uk. 58, Ibnul-Maghazili Tarjumah ya Ali Uk. 79.

Na alimzidishia wasaa wa kiwiliwili, kwa kweli alistahiki kuwa Simba wa Mwenyezi Mungu aliye mshindi, na nguvu zake na ushujaa wake ni wenye kupigiwa mfano katika kila zama kiasi kwamba wanahistoria wamesimulia visa vingi kuwa ni miujiza, kama vile kuung’oa mlango wa Khaybar, wakati ambapo Masahaba Ishirini walishindwa hata kuutikisa. Na pia kuling’oa Sanamu kubwa la Hubal kutoka juu ya paa la Al-Kaabah na kulisogeza jiwe kubwa ambalo jeshi lote lilishindwa hata kulitikisa na mengineyo miongoni mwa riwaya mashuhuri.