Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyed Ali Khamenei leo Jumatatu ametoa hotuba
muhimu katika ufunguzi wa kikao cha ‘Maulamaa wa Kiislamu na Mwamko wa
Kiislamu’ ambapo amefafanua kwa mitazamo mbalimbali ya tukio adhimu la
Mwamko wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu ametathmini
mustakabali wa mwamko wa Kiislamu kwa mitazamo miwili muhimu. Awali amefafanua
kuhusu kile ambacho kimejiri hadi leo katika mwelekeo wa Mwamko wa Kiislamu
Kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati na taathira za tukio hilo adhimu
katika mlingano wa kijamii na kisiasa katika ulimwengu wa Kiislamu. Kiongozi
Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ameashiria taathira za muda mfupi na
hatima ya Harakati ya Mwamko wa Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amechambua
harakati ya Mwamko wa Kiislamu Kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati kwa
mitazamo mitano ambayo ni, ‘Ulazima wa kuhifadhi marejeo na nafasi ya dini’,
‘kuainisha malengo ya muda mrefu’, ‘kujiepusha na tajriba chungu ya kufurahia
ahadi za Magharibi’, ‘kuchukua tahadhari mbele ya njama za kuzusha machafuko ya
umwagaji damu na hitilafu za kimadhehebu na kikabila’, pamoja na ‘kutosahau
kadhia muhimu ya Palestina.' Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa: “Kusimama
kidete kwa mujibu wa msingi wa Uislamu’ na ‘kujitokeza wananchi katika medani’
ni sababu mbili muhimu na za msingi ambazo zitavunja njama na hila zote za
maadui.
Mwamko wa Kiislamu kama
ulivyobainishwa katika hotuba ya Kiongozi Muadhamu hivi sasa ni ukweli na
uhakika ambao unaweza kuonekana katika takribani kila eneo la ulimwengu wa
Kiislamu. Mfano wa wazi kabisa wa mwamko huo ni hamu kubwa ya Umma na hasa
vijana ya kuhuishwa tena adhama ya Uislamu na kuwekwa wazi uso mchafu, wa
kidhalimu na kiistikbari wa nchi za kibeberu.
Kwa hivyo kilicho wazi ni kuwa upeo
wa harakati adhimu ya Mwamko wa Kiislamu ni mpana sana na wenye kutia matumaini
na kutoa bishara njema za kutimia ahadi kubwa zaidi. Lakini sambamba na upeo
huu wenye matumaini vitisho navyo si vichache. Vitisho hivyo vinalenga
kuibadilisha harakati ya Mwamko wa Kiislamu kuwa machafuko na umwagaji damu wa
kikabila, kikaumu, kimadhehebu na kitaifa.
Ayatullahil Udhma Sayyed Ali
Khamenei amesema njama hizi zinatekelezwa na mashirika ya kijasusi ya nchi za
Magharibi na utawala wa Kizayuni kwa msaada wa dola za mafuta zinazohodhiwa na
watawala waliojiuza kutoka eneo la mashariki mwa Asia hadi kaskazini mwa Afrika
hasa watawala wa nchi za Kiarabu. Amesema njama hizo zinafanikishwa vyema na
fedha ambazo zingetumiwa kuboresha maisha ya viumbe vya Allah, zinatumika
katika vitisho, kukufurishana, ugaidi, kutega mabomu na kumwaga damu ya
Waislamu sambamba na kueneza moto wa chuki za muda mrefu.
Kiongozi Muadhamu amesema yanayojiri
Bahrain ni mfano wa njama hizo. Amesisitiza kuwa, akthari ya watu nchini humo
wamedhulumiwa kwa miaka mingi na wamenyimwa haki ya kupiga kura na haki
nyinginezo za kila taifa. Amesema Wabahraini wameamka kudai haki zao
lakini kwa sababu aghalabu ya wanaodhulumiwa ni Mashia na utawala uliopo
ni wa kiimla na usiozingatia dini lakini unadai kuwa ni wa Kisunni, vyombo vya
kipropaganda vya Ulaya na Marekani na vibaraka wao wanadai harakati ya
Wabahraini ni mapambano ya Mashia na Masunni.
Ni kwa msingi huo ndio Kiongozi
Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akaitaja kuwa ya dharura nafasi ya Maulama wa
Kiislamu pamoja na kutizama kwa ustadi medani ya matukio ya kieneo. Ametoa wito
kwa Maulama watangaze misimamo yao wazi wazi na wafichue njama zote ili maadui
wasifikie malengo yao haramu. Hakuna shaka kuwa Maulama wakubwa wa Ulimwengu wa
Kiislamu wakiwemo wale wa nchi muhimu za Kiislamu kama Iran, Misri na Iraq
wamekuwa na nafasi muhimu katika harakati hii kubwa ya kihistoria ya kupinga
tawala za kiimla katika nchi za Kiislamu. Leo vile vile maulama wana nafasi
muhimu sana katika kutekeleza majukumu muhimu ya kuilinda na kuihami harakati
ya Mwamko wa Kiislamu kutokana na tufani adhimu ya fitina za maadui.
Hakuna shaka kuwa harakati ya Mwamko
wa Kiislamu imeweza kuhuisha tena Uislamu kisiasa na kijamii na kuleta mtazamo
mpya katika upeo wa maisha, serikali na matukio ya kijamii katika nchi
zilizokuwa zikitawaliwa na watawala dhalimu ambao walikuwa wakipata uungaji
mkono wa madola ya kibeberu. Harakati hii ya Mwamko wa Kiislamu bila shaka
itayatia hasara kubwa madola ya kiistikbari.
Ni kwa kuzingatia masuala hayo yote
ndio maana Ayatullah Ali Khamenei ameutaja Mwamko wa Kiislamu kuwa tukio kubwa
ambalo iwapo litabakia salama na kuendelea basi utakuwa mwanzo wa kuibuka
ustaarabu mpya wa Kiislamu katika mustakabali wa karibu. Kutoka http://kiswahili.irib.ir/uchambuzi/item/31516-hotuba-ya-kiongozi-wa-mapinduzi-ya-kiislamu-katika-kikao-cha-maulamaa-na-mwamko-wa-kiislamu