HURUMA YA IMAM ALI BIN ABI TALIB (A.S).

Bismillahir Rahmanir Rahim.

 Imam Ali bin Abi Talib (a.s) amesema: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu laity nikipewa mbingu saba na vyote vilivyo chini yake eti ili tu nimwasi Mwenyezi Mungu kwa kumnyang’anya mdudu chungu punje ya shairi, sitofanya, na hakika dunia yenu hii ni dhalili kwangu kuliko jani lililomo mdomoni mwa nzige.

Taz: Nahjul Balaghah, hotuba ya 224

Imam Ali bin Abi Talib (a.s) ndiye mwenye maagizo mazuri aliyoyatuma kwa Al-Ashtar An-Nakhaiy gavana wake wa Misri na watu. Ndani ya maagizo hayo amesema: “Usiwe mnyama mkali mwenye kushambulia unayetumia fursa kwa ajili ya kuwala wao. Kwani hakika wao wako katika makundi mawili: Ima ni ndugu yako katika dini au ni kiumbe mwenzako, hivyo wape msamaha wako kama unavyopenda upewe msamaha na Mwenyezi Mungu. Wala usijute kwa msamaha wowote utakaotoa, wala usijivune kwa adhabu yoyote utakayotoa.” Kisha akamwambia: “Jizuie kujilimbikizia.”

Taz: Nahjul Balaghah, barua ya 53

Hakika ukali wa Imam Ali bin Abi Talib (a.s) katika kuzuwia kujilimbikizia ulikuwa ni sababu kubwa ambayo ilipelekea kutokea  yaliyotokea kati yake na Muawiyyah na jamaa zake, kwani hakika hawa walitaka ufalme, mali na utajiri kwa ajili ya nafsi zao huku Imam Ali bin Abi Talib (a.s) akitaka hayo yote yawe kwa ajili ya raia wote.

Huruma iliwafikia watu wote akawasamehe dhidi ya yale wanayoyatenda, hivyo watu wa Busra walimpiga vita, wakaupiga kwa mapanga uso wake na nyuso za wanae, wakamtukana na kumlaani, lakini alipowashinda hakuwauwa na akawa kawaingiza katika amani yake. Na aliusia kutendewa wema Yule mwovu muuaji wa nafsi yake Ibn Muljim.