TANGAZO.


"Mnajua nafasi yangu kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ukaribu wa karibu na nafasi mahsusi niliyonayo kwake. Alinilea nikiwa mtoto akinikumbatia kifuani mwake na kitandani kwake. Akinigusisha mwili wake, akininusisha harufu yake. Alikuwa akitafuna kitu kisha akinilisha, hakupata uongo wa kauli yoyote toka kwangu, wala kosa lolote la kitendo.

Nilikuwa nikimfuata kama mtoto aliyeachishwa ziwa amfuatavyo mama yake, huku kila siku akiniinua juu kwa kuniongezea sehemu ya maadili yake huku akiniamrisha kumfuata. Kila mwaka alikuwa akienda pango la Hira hakuna anayemuona isipokuwa mimi tu. Wala hakuna nyumba hata moja kipindi hicho iliyokuwa imekusanya Waislam wasiyokuwa Mtume, Khadija na mimi nikiwa watatu wao, nikiona nuru ya Whyi na Utume huku nikinusa harufu ya unabii.

Nilisikia mlio wa Shetani pindi Wahyi ulipomshukia Mtume, nikasema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ni sauti ya nani hii?"
Akajibu: "Huyu ni Shetani amekata tamaa dhidi ya kuabudiwa, hakika wewe unasikia ninayosikia na unaona nionayo wewe si nabii lakini wewe ni waziri na hakika wewe upo juu ya Kheri."

Nahjul-Balaghah, hotuba ya 192.