SHAKHSIYYA YA IMAM ALI BIN ABI TALIB (A.S).

Shakhsiyya ya Imam Ali bin Abi Talib (a.s) ilianza kujitokeza katika kipindi cha kwanza cha Uislam, kwa kuambatana kwa karibu zaidi na Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w). Hakuachana na Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) tangu utotoni mwake mpaka mwisho wa Uhai wa Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w). Na alikuwa ni mtu aliyeshiriki na kupigana vita pamoja na Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w)  kwa wingi na mafanikio zaidi kuliko yeyote katika Maswahaba. Amepigana na washirikina na makafiri na wanafiki, na akawa ni Shujaa kati ya Mashujaa wakubwa. Alikuwa ni kiumbe bora zaidi kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake siku ya Ahzaab, ambapo Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) alisema: "Kwa hakika nitampa bendera kesho mtu anayempenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na anapendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake." Kama alivyomsifu kwa imani thabiti siku ya KHANDAQ, Imam Ali bin Abi Talib (a.s) alipotekea kupambana na Amr bin Abd - Wudd Al-aamiry, Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alisema: "Pambano la Ali na Amr bin Abd - Wudd siku ya KHANDAQ ni bora zaidi kuliko 'amali zote za Umma wangu mpaka siku ya Kiyama, bila shaka imani yote imepambana na shiriki yote."

Imepokewa kuwa: Usiku alitoka Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kutoka Makka kwenda Madina, alimwamuru Ali bin Ab Talib (a.s) kulala kitandani kwake. Malaika Jibril (a.s) alisimam kichwani kwake, na Malaika Mikaeli akasimama miguuni, kisha Malaika Jibril (a.s) akasema: Hongera, nani aliye mfano wako ewe Ibn Abi Talib? Mwenyezi Mungu anajifakhiri kwa Malaika kwa ajili yako, na akasoma: "Na miongoni mwa watu kuna ambaye huiuza nafsi yake kwa ajili ya kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma juu ya waja." (Qur'an: 2:207)