Maulana Sheikh Hemed Jalala,
Mudir wa Hawzat Al-Imam Swaadiq (a.s), jijini Dar es Salaam anawataka Waumini wote wa Kiislam waliyopo Dar es Salaam, kushiriki Swala ya Ijumaa Masjid Ghadiir Khum, Kigogo post, Dar es Salaam, amesema kushiriki kwao katika Swala ya Ijumaa kutafanya Harakati kuwa endelevu na kujulishana mambo mbalimbali. Msikiti ni makao ya Harakati za Kiislam, kitovu cha Msikiti ni Mihrabu, na Mihrabu maana yake ni mahala pa vita na mapambano. Na Mimbari ni Kipaza sauti cha miito na ni Nara za Kiislam, kwa hiyo, hakuna mahala bora kabisa pa kuwasiliana katika kuwashajiisha Wanaharakati wa Kiislam kama Msikiti ambao ni ngome yao. Swala ya jamaa ni kiunganisho cha Waislam wa mitaa yote ya mji na vitongoji vyake, hivyo siku ya Ijumaa baada ya kukumbushwa juu ya matatizo ya kijamii, na kisiasa yanayo wakabili Waislam, na baada ya kutekeleza Faradhi ya kiibada, huondoka Msikitini wakiwa na moyo wakutekeleza kwa matendo Faradhi nyingine za Kiislam. Mwenyezi Mungu anasema: "Anayeimarisha Misikiti ya Mwenyezi Mungu ni yule tu anayemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na kusimamisha Swala na kutoa Zaka na hawamuogopi yeyote ila Mwenyezi Mungu, basi hao huenda wakawa miongoni mwa walio ongoka." (Qur'an: 9:18)