MWALIKO WA MAJLIS YA IMAM HUSSEIN (A.S).


Bismillahir Rahmanir Rahim.

Asalaam Aleykum.
 
Uongozi wa Hawzat Al-Imam Swaadiq (a.s),Unapenda kuwaalika katika kumbukumbu ya Kifo cha Imam Hussein (a.s), Mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w),itakayofanyika Masjid Ghadiir Khum, Kigogo post, jijini Dar es Salaam, siku ya Ijumaa 16-11-2012, kwa muda wa siku kumi na mbili (12), mfululizo kuanzia saa 07:00 Mchana pia kutakuwa na Karbala project ambayo itaonyesha Ramani ya Karbala, Tamthilia ya historia ya Imam Hussein (a.s),na ugawaji wa Vipeperushi mbalimbali, kuanzia Saa 1:30 usiku hadi Saa 4:00 usiku, wazungumzaji watakuwa wafuatao: Sheikh Said Athuman, Sheikh Muhammad Abdu, Sheikh Ghawth Salm Nyambwa, Maulana Sheikh Hemed Jalala yeye atakuwa mzungumzaji wa kila siku . Waislamu wote mnakaribishwa,fikisha ujumbe kwa wengine Inshallah.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:

"Na anachokupeni Mtume basi pokeeni, na anachokukatazeni basi jiepusheni nacho."

(Qur'an: 59:7)

Kutokana na Aya hapo juu inakuwa wazi kabisa kwamba kile anachotuambia Mtume (s.a.w.w) kukifanya, lazima tukifanye, na kile anachotuambia tusikifanye, lazima tukiache.

Kitu kimoja ambacho wanachuoni wote Wakiislam wanakubaliana nacho, ni kwamba Mtume (s.a.w.w) alimpenda sana Hussein (a.s) na alitaka Waislam wote kufanya hivyo hivyo. Hadithi zinazopatikana katika vitabu vya wanachuoni wa Kishia na Masunni, hutuambia kwamba Mtume (s.a.w.w) alijua kitakachompata Imam Hussein (a.s) baadaye mikononi mwa Bani Ummaya. Kwa mfano, tunaambiwa kwamba wakati Imam Hussein (a.s) alipozaliwa, Malaika Jibril alimjulisha bwana Mtume (s.a.w.w) kwamba siku moja mtoto huyu atakuwa na atauwawa shahidi na maadui wa Uislam. Wakati Bibi Fatma aliposikia habari hizi alihuzunika sana. Alimuuliza baba yake, "Ni lini mtoto wangu Hussein atauwawa shahidi, je, nitakuwa hai?

Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) alimwambia kwamba si mimi wala si wewe atakayekuwa hai.
Imam Ali (a.s) na Imam Hassan (a.s) vile vile hawatakuwa hai. Lakini Allah ataitengeneza jumuiya moja kwa ajili ya kuweka tu hai kumbukumbu za Imam Hussein (a.s).
"Watu katika jumuiya hii" Mtume (s.a.w.w) alisema: "Watalia kwa ajili ya Hussein na Wanaume wake Mashahidi, na Wanawake watalia mpaka siku ya Hukumu kwa ajili ya Wanawake wa nyumba yetu."

Kutokana na hadithi hiyo hapo juu inakuwa wazi kwamba Bwana Mtume (s.a.w.w) alitaka kwamba, maisha na kifo cha kishahidi cha Imam Hussein (a.s) kiwe kinakumbukwa.
Wakiwa wanafuata nyayo za Bwana Mtume (s.a.w.w), na watu wa nyumbani kwake ambao walishughulika katika kuyafanya mambo yote hayo ambayo kwayo madhumuni ya kifo cha kishahidi cha Imam Hussein (a.s) kinaweza kuelezewa kwenye Ulimwengu.

TUNAMKUMBUKA VIPI IMAM HUSSEIN (A.S).?

Kwa mara nyingine tena, tunatazama maisha ya Bwana Mtume (s.a.w.w) ili kuona ni vipi alivyowakumbuka vipenzi vyake, na kwa hiyo tunafanya hivyo kwa Imam Hussein (a.s) na mashahidi wengine.

Baada ya vita vya Uhud wale ambao wamewapoteza wapenzi wao walijikusanya katika nyumba zao na wakaanza kuwalilia. Mtume (s.a.w.w) alihuzunika sana,kwani Ami yake Hamza aliuwawa katika vita ya Uhud lakini hakuna anayemlilia nyumbani kwake. Hivyo Masahaba wa Mtume (s.a.w.w) waliwaambia jamaa zao kwenda nyumbani kwa Hamza na kulia kwa ajili yake. Wakati Bwana Mtume (s.a.w.w) alipowaona jamaa za Masahaba wanamlilia Hamza, alifarijika sana na akawaombea Masahaba na jamaa zao maisha mema.

Katika wakati mwengine, Bwana Mtume (s.a.w.w) aliposikia habari za kifo cha binamu yake Jaa'far katika vita vya Muta, alikwenda mwenyewe nyumbani kwa Jaa'far na kutoa habari hizi, mjane wa Jaa'far, Asma bint Umays alianza kulia. Mtume (s.a.w.w) hakumnyamazisha, alimuacha alie.

Tena wakati mtoto wake Ibrahim alipokufa akiwa bado mtoto, Bwana Mtume (s.a.w.w) alihuzunika sana, na alilia sana kwa ajili ya mtoto wake.

Kwa hiyo kukusanyika na kulia kwa ajili ya waliokufa ni "SUNNA" ya Bwana Mtume (s.a.w.w). Si kwamba Mtume (s.a.w.w) aliwahimiza Waislam wengine kufanya hivyo, bali yeye mwenyewe alijihusisha, na kushiriki katika mikusanyiko hiyo kama ilivyokuwa katika vifo vya wapenzi wake waliotajwa hapo juu.

Hivyo, Maimamu watukufu wa nyumba ya Bwana Mtume (s.a.w.w) waliwashauri Waislam kufanya Mikutano (Majlis) kwa jina la Imam Hussein (a.s).

Imam Jaa'far As-Sadiq (a.s) Imam wa sita, na Imam Ali Ridha (a.s) Imam wa nane, wao walipata fursa ya kutayarisha mikutano kwa ajili ya Maombolezo ya Imam Hussein (a.s). Katika mikutano hiyo wahubiri waliitwa kutoa maelezo juu ya shida alizopata Imam Hussein (a.s) na Masahaba zake kabla na baada ya kuja kwao Karbala. Kwenye mkutano mmoja kama huo Imam Jaa'far As-Sadiq (a.s) aliwashauri Masahaba zake kulia kwa ajili ya Imam Hussein (a.s) katika namna ile ile ambayo Bibi Fatma (a.s) anamlilia huko Peponi. Masahaba wakamuuliza ni vipi Bibi Fatma anavyomlilia mtoto wake? Imam Jaa'far Sadiq (a.s) akasema: "Analia kwa sauti kubwa kama vile Mama anavyolia kwa kifo cha mtoto wake wa miaka kumi na nane (18).

Imam Ali bin Hussein (a.s) (Mashuhuri kwa jina la Zainul Abidiin) alilia kwa ajili ya mashahid wa Karbala kwa muda wa zaidi ya miaka thelathini.
Inasemekana kwamba alimshauri sahaba wake mmoja kufanya Majlis ya kumkumbuka Imam Hussein (a.s) kabla ya sherehe ya ndoa ya kijana wake au bint yake; na ni baada ya hilo tu, ndipo Zainul Abidiin angehudhuria ndoa hiyo.

Kwa mujibu wa Allamah Majlis, baada ya kurudi kutoka gereza la Damaskasi, Imam Zainul Abidiin (a.s) alikuwa mara kwa mara akifanya majlisnyumbani kwake kwa ajili ya maombolezo ya Imam Hussein (a.s). Baada ya maombolezi, chakula kiliandaliwa kwa jina la Imam Hussein (a.s) kwa wale waliohudhuria majlis hizo.

Hakika, kitendo cha mtu kulia kwa ajili ya wapenzi wake kimesifiwa sana katika Qur'an yenyewe. Wakati Mtume Yakub (a.s) alipotenganishwa na mtoto wake Yusufu (a.s), Mtume Yakub (a.s) alilia sana kwa ajili ya mtoto wake, "Mpaka macho yake yakawa meupe (kipofu)." Kama kulia nikitendo kibaya, Allah (s.w.t) angesema wakati anaelezea kitendo hiki katika Qur'an. Badala yake, Allah (s.w.t) alimsifia Mtume Yakub na kumuona yeye kama mtu mwenye Subira: "Na akajitenga nao na akasema: "Oh huzuni wangu juu ya Yusufu! na macho yake yakawa meupe kwa huzuni, Na alikuwa mwenye subira."

(Qur'an: 12:84)

Kwa hiyo njia moja ya kumkumbuka Imam Hussein (a.s) ni kufanya Majlis mara kwa mara kiasi inavyowezekana. Majlis huandaliwa hususani katika miezi ya Muharram (mfungo nne) na Safar (mfungo tano).