KUMTII MWENYEZI MUNGU, MTUME NA ULUL-AMRI.

Bismillahir Rahmanir Rahim.

Mwenyezi Mungu (s.w) anasema katika Suuratun Nisaa:
"Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtii Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi, na kama mkigombana katika jambo lolote basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume ikiwa mnamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya Mwisho. Hilo ni bora zaidi na ni lenye mwisho mzuri zaidi."

(Qur'an:4:59)

Katika Aya hii kuna mambo Manne ni muhimu kufafanuliwa:-

(a) Kumtii Mwenyezi Mungu.
(b) Kumtii Mtume (s.a.w.w).
(c) Kuwatii Ulul'Amri (wenye mamlaka).
(d) Mambo yote yahukumiwe nao (waliotajwa hapo juu).

(a) na (b) Kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume (s.a.w.w).

Aya zilizokuja kuamrisha atiiwe Mwenyezi Mungu na Mtume ni nyingi sana, basi hapa nitataja Aya mbili tu: Mwenyezi Mungu anasema: Waambie: "Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume na kama wakikataa, basi Mwenyezi Mungu hawapendi Makafiri." 3:32 akasema: "Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume ili mpate kurehemewa."

(Qur'an:3:132).

(c) Kuwatii Ulul'Amri.

Ulul'Amri, yaani wenye mamlaka. Watu wengi hufahamu kimakosa, kuwa mtawala wa nchi, au Sheikh ndiye Ulul'Amir. Dhana hii potovu.

Mwenyezi Mungu anasema:
"Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi." (Qur'an:4:59). Waumini wenye mamlaka hapa ni Ahlul-Bayt (a.s) na wala si muumini yeyote tu, sembuse asiyekuwa muumini au mkuu tu wa kidunia!!

Ulul'Amri ni watu wenye daraja kubwa baada ya Mtume (s.a.w.w) na imeamriwa kufuata uongozi wao, nao ndio Ahlul-Bayt (a.s).

Ni kama ifuatavyo:-

Mtume (s.a.w.w) yeye ndiye aliyewaamrisha Waislam wote kufuata uongozi wa Ahlul-Bayt (a.s), amesema Mtume (s.a.w.w) kuwa: "Mimi ninakuachieni vitukufu viwili, Qur'an na Ahul-Bayt wangu (watu wa nyumbani kwangu) na viwili hivi havitaachana mpaka vitakaponifikia katika Haudh."

Mtume (s.a.w.w) yeye ndiye aliyewaamrisha Waislam wote kuwaswalia (kuwatakia rehema) Ahlul-Bayt (a.s) katika swala zote za Faradhi na za Sunna.
Na Waislam wote popote walipo huwataja Ahlul-Bayt, ambao ndiyo Ulul'Amri katika swala zao wakiwaswalia kama swala ya Mtume (s.a.w.w) na hapa Imam Shaafii anasema:

"Enyi watu wa nyumba ya Mtume, kupendwa kwenu ni lazima kutoka kwa Mwenyezi Mungu, katika Qur'an ameteremsha, inatosha kwenu kuwa ni heshima kubwa na kwamba nyinyi, yeyote asiyewatakia rehema hana swala."

Mwenyezi Mungu anasema: "Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake humsalia Mtume, enyi mlioamini msalieni (Mtume) na muombeeni amani. 

(Qur'an: 33:56)

Iliposhuka Aya hii, Maswahaba walimuuliza Mtum: "Tutakuswalia vipi?
Mtume akawaambia, semeni: "Allahumma Swalli a'laa Muhammad wa a'alaa Aali Muhammad."

Taz: Tafsirus Saafi     J.4 Uk.201
       Tafsirul Basaair  J.32 Uk. 653-672
       Almizan fyitafsiril Qur'an J.16 Uk. 366
       Alburhan fyitafsiril Qur'an J.3 Uk. 335
       Majmaul Bayani J.4 Uk. 369
       At-Tafsirul Kaashif J.6 Uk. 237

Mtume (s.a.w.w) amesema: Msiniswalie swala iliyo katika, Maswahaba wakauliza:
Ni swala gani iliyokatika? Mtume (s.a.w.w) akajibu: Mnasema, Allahumma Swalli a'laa Muhammad, mnanyamaza, lakini semeni: Allaahumma swalli a'laa Muhammad wa a'laa Aali Muhammad."

Taz:  As'swawaaiqul Muhriqa  Uk. 146
        Yanaabiul Mawadda       J. 1 Uk. 6

Angalieni: kusema, "Swallallahu a'layhi wasallama" ni batili, unatakiwa kusema: "Swallallahu a'alayhi wa Aalihi."

Mtume (s.a.w.w) yeye ndiye aliyefananisha uongozi wa Ahlul-Bayt na meli ya Nabii Nuhu (a.s) aliposema: "Mfano wa Ahlul-Bayt wangu, ni kama meli ya Nuhu, atakayeipanda ameokoka, na atakayebaki nje yake (asipande) atazama."

Taz: Hilyatul'Awliyaa          J.4 Uk. 306
       Majmauz Zawaidi        J.9 Uk. 168
       Tarekh Bughdad         J.12 Uk. 91

Ahlul-Bayt (a.s) ni watakatifu waliotakaswa sana na Mwenyezi Mungu (s.w).
Mwenyezi Mungu (s.w) amesema:
"Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa nyumba (ya Mtume), na (anataka) kukutakaseni sanasana." 

(Qur'an: 33:33)
 

(d) Mambo yote yahukumiwe nao:-

Kwa Ulul'Amri ambao ni Ahlul-Bayt (a.s) Mwenyezi Mungu anasema:
"Na linapowafikia jambo lolote la amani au la Khofu hulitangaza, na kama wangelilipeleka kwa Mtume na kwa Ulul'Amri."

(Qur'an: 4:83).

Ama kwa Mwenyezi Mungu na Mtume ni:-

Mwenyezi Mungu amesema: " Haiwi kwa Mwanamume aliyeamini wala kwa Mwanamke aliyeamini, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapotakata shauri, wawe na Khiyari katika shauri lao na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika amepotea upotovu ulio wazi:

(Qur'an: 33:36).