MUSLIMU BIN AKIL, BALOZI WAKE HUSSEIN (A.S).


 
 1-Yaillah ya Kayyumu, twakushukuru Manani,
Muhammad Msalimu, na watu wake nyumbani
 Abbasi na Muslimu, Mola awape amani
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

2- Najua mnayohamu, kusikiya ya Hussein,
Namtaja Muslim, binamu, yake Hussein
Shujaa mwana Hashimu, mrithi wa Adinani
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

3- Kaondoka Muslim, kundi moja na Hussein,
Kuepuka udhalimu, wa Yazidi maluuni
Mpenda kumwaga damu, ya wana wa Adinani
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

4- Huko Makka Muslimu, akatumwa na Hussein,
Katikati ya Swaumu, ya mwezi wa Ramadhani
Akapeleka salamu, za ujio wa Hussein
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

5- Irakki wanalaumu, kuchelewa kwa Hussein,
Waambie Waislamu, nakuja niko njiani
Kuja huko ni muhimu, ili kuinusuru dini
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

6- Nakujua Muslimu, unanipenda jamani,
Usijali tutadumu, pamoja huko peponi
Tusipokutana humu, ni mapenzi ya Manani
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

7- Kapokewa Muslimu, kwa salama na amani,
Kaziagiza salamu, kwa ndugu yake Hussein
Yazidi mwaga damu, kapeleka wahaini
Husein na Muslimu, watakutana peponi.

8- Wakatishwa wanadamu, wamgeuke Hussein,
Na nduguye Muslimu, sasa yuko Mashakani
Kavamiwa Muslimu, kule kule ugenini
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

9- Akamtuma Muslimu, kushitaki kwa Hussein,
Usije tena Imamu, mwenzio ni hatarini
Tusife wote Imamu, bora ishia njiani
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

10- Vitoto vya Muslimu, vyarejea kwa Hussein
Kavituma Muslimu, asije tena Hussein,
Baba ana hali ngumu, kule kule ugenini
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

11- Watoto yawalazimu, na njaa matumboni,
Kuwakwepa madhalimu, wasiwakute njiani
Mchana yawalazimu kujificha vichakani
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

12- Giza likija na zamu, ya kutembea njiani,
Mama wa kiislamu, kuwaona mitaani
Watoto wenye nidhamu, mbona wapo mashakani
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

13- Mama wa kiislamu, kawachukua nyumbani,
Mume wake ni dhalimu, vile vile hayawani
Mama ikamlazimu, akawaficha nyumbani
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

14- Watoto wa Muslimu, wakakamatwa jamani,
Kwa kamba iliyo ngumu, wakafungwa miguuni
Baba mwenye roho ngumu, hana huruma jamani
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

15- Kisha akamwaga damu, akawachija jamani,
Mkewe kamlaumu, kamfyeka mikononi
Vichwa vyao marehemu, kavipeleka mjini
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

16- Turudi kwa Muslimu, akiwa kule mjini,
Mji hajaufahamu, ahaha vichochoroni
Hana ndugu Muslimu, rafiki wala jirani
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

17- Kama tunavyofahamu, uvamiwe ugenini,
Wenyeji kila sehemu, wanakutenga jamani
Hadi anatoka damu, mtetezi hamuoni
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

18- Kawaambia Muslimu, nawaomba niacheni,
Nirejee kwa Imamu, msiniuwe jamani
Kwani nishafahamu, hamumtaki Hussein
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

19- Kiu ya kumwaga damu, iliwajaa vichwani,
Kwa silaha zenye sumu, kashambuliwa mwilini
Mwili wamwagika damu, kwa kuinusuru dini
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

20- Kazimia Muslimu, alipoanguka chini,
Kabebwa na madhalimu, hadi juu kipaani
Akaachiwa Muslimu, kichwa kikaruka chini
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

21- Yailahi ya kayyumu, imetujaa huzuni,
Nimefikia sehemu, nasononeka moyoni
Beti hii yalazimu, nisimamishe jamani
Hussein na Muslimu, watakutana peponi.

Mtunzi wa Shairi: Juma S. Magambilwa