Imam Khomeini
amezaliwa katika mji wa Khomein mwaka 1902,
mji uliyopo umbali wa kilometa 349 kusini Magharibi mwa Tehran
mji mkuu wa Iran.
Amezaliwa katika
familia ya Wachamungu, na baba yake Ayatullah Sayyid Mustapha Al-Musawiy
alikufa shahidi akiwa mikononi mwa maafisa wa Serikali miezi sita tangu
kuzaliwa Imam Khomeini.
Ama mama yake ni bi Hajira, nay eye anatokana na familia
iliyojulikana kwa elimu na Uchamungu. Ilipofikia mwaka 1908 mama yake alifariki
dunia baada ya kuugua, hivyo Imam Khomeini akamkosa mama yake mpendwa akiwa na
umri wa miaka sita hapo akalelewa na Shangazi yake bi Swahibat mpaka
alipofikisha umri wa miaka kumi na tano ndipo Shangazi yake nae alipofariki.
Kwa hiyo Imam aliishi ndani ya tabu za uyatima tangu mtoto
mdogo, na akawa amefahamu vizuri maana ya kifo cha Shahidi, na hizi zilikuwa ni
sababu zilizotoa changamoto katika ujenzi wa utu wake.
MASOMO:-
Imam Khomeini alisoma elimu za utangulizi kama vile
utamaduni wa Kiarabu, Mantiki na Usulul-Fiqh akiwa katika mji wa Khomein, na
alipofikisha umri wa miaka kumi na tisa mwaka 1921 alikwenda Hauza ya mji wa
Arak. Baadae alielekea mji wa Qum baada ya kusoma hapo muda wa mwaka mmoja,
huko alienda kumaliza masomo yake ya mwanzo na kusoma Hisabati, Maumbo,
Falsafa, Akhlaqi na Irfani chini ya Mujitahidina na wanazuoni wakubwa wa Sheria
pia alisoma kwa Marehemu Ayatollah Al-Mirza Muhammad Ali Shah Abadi masomo ya
juu ya Irfan ya kinadharia na kimatendo muda wa miaka sita. Alipofikia umri wa
miaka ishirini na saba mwaka 1929 alianza kutoa mihadhara na masomo kwa
wanafunzi wake, hivyo akaanza kufundisha Falsafa ya Kiislam, Irafan ya
kinadharia, Fiqhi, Usulul-Fiqh na maadili ya Kiislam na aliendelea kufundisha
maudhui hizi muda wote alioishi mji wa Qum.
JIHADI NA MAPINDUZI:-
Vielelezo vilivyo vinaonyesha kuwa Imam Khomeini tangu
mwanzo wa ujana wake na kipindi chake cha masomo alikuwa akipambana na
uharibifu wa kijamii, kifikra na kimaadili, hivyo mwaka 1943 aliandika kitabu
chake kiitwacho Kashful-Asrari na kukisambaza. Kitabu hicho kilifichua waziwazi
Kashfa za Mfalme Riza Shah alizozifanya muda wa miaka ishirini na pia kilijibu
maswali na hoja za wapotevu huku kikiutete Uislam na Wanazuoni. Na humo Imam
Khomeini alitoa fikra ya kupatikana Serikali ya Kiislam na dharura ya kuwepo
mapinduzi. Imam Khomeini aliendelea kupinga utawala wa Mfalme na tarehe
22-3-1963 utawa wa Kifalme ulivamia shule ya masomo ya Kiislam ya Al-Faydhiyah
iliyopo katika mji wa Qum na kuuwa baadhi ya
wanafunzi wa masomo ya dini. Hivyo hotuba na maelezo ya Imam kuhusu tukio hili
la kusikitisha yalienea pande zote za Iran. Alasiri ya siku ya kumi ya
mfungo nne mwaka 1383 sawa na tarehe 2-6-1963, Imam Khomeini alitoa hotuba kali
ambayo alifichua njama na mahusiano ya siri kati ya utawala wa kifalme na uzayuni.
Ni usiku huohuo kikosi maalumu cha utawala wa kifalme kilizingira nyumba ya
Imam Khomeini na kumtia nguvuni kisha kumpeleka Tehran, lakini habari za Imam
Khomeini kutiwa nguvuni zilienea Iran nzima, hivyo lilipochomoza tu jua la siku
ya pili watu walijaa barabarani katika maandamano wakiwa na hasira, na
maandamano makubwa sana yalikuwa ni yale ya mji wa Qum ambayo yalipingwa kwa
nguvu zote na utawala wa kifalme hadi baadhi ya watu wakafa shahidi. Huko
Tehran mfalme alitangaza hali ya hatari, hivyo maandamano yakazuiliwa kwa nguvu
zote kuanzia siku hiyo na siku iliyofuata, na hapo Serikali ya kijeshi ya Shah
ikauwa maelfu ya watu, na mauwaji ya tarehe 5-6-1963 ndiyo yalikuwa makubwa
kiasi kwamba habari zake zilienea sana kupita kiasi na kuamsha hisia za watu wa
aina zote, hivyo kuanzia wasomi na watu wa kawaida wote ndani na nje ya Iran
walilaumu na kulaani mauwaji hayo. Baada ya Imam Khomeini kukaa gerezani miezi
kumi, utawala wa Kifalme wa Shah ulilazimika kumuachia huru, lakini Imam
Khomeini aliendelea kuupinga utawala huo huku akitoa hotuba ambazo zilikuwa
zikiweka wazi njama za Mfalme. Utawala wa Kifalme kwa kushirikiana na wanasiasa
wa Kimagharibi na Askari wa Kimarekani walipanga njama za kumuuwa, jambo ambalo
liliamsha hasira kwa kiongozi huyu wa Mapinduzi, hivyo alipozigundua tu njama
hizi aliongeza juhudi zake kwa kutuma barua na ujumbe miji yote ya Iran na
akaazimia kutoa hotuba siku ya tarehe 26-10-1964 ili kufichua njama hizi. Japokuwa
dola ilimtisha Imam kwa kila aina ya vitisho, lakini siku hiyo alipaza sauti
juu na kuishambulia Serikali. Hivyo tarehe 4-11-1964 vikosi maalumu na vile vya
mwavuli vilizingira nyumba ya Imam Khomeini na kumtia nguvuni, kisha moja kwa
moja vikampeleka uwanja wa ndege wa Tehran.
Kutikana na makubaliano ya mwanzo alipelekwa Ankara
kisha Borisia Uturuki ili awe chini ya ulinzi mkali wa vikosi vya Usalama vya Iran
na Uturuki, na wamzuie asifanye harakati zozote za kisiasa na Kijamii.
KUFARIKI:-
Hakika Imam Khomeini ambaye alikaribia umri wa miaka tisini
hakuwahi hata sekunde moja kupuuza jambo lolote katika mikakati ya kuinua jamii
ya Kiislam, hivyo alikuwa kiongozi wa kisiasa mwenye changamoto na harakati
nyingi ulimwenguni. Kila siku alikuwa akisoma na kufuatilia kwa karibu habari
na ripoti muhimu magazeti na kutoka majarida mbalimbali ya habari, huku
akisikiliza habari kupitia vituo vya redio na luninga vya Iran na bila
kusahau uchambuzi wa habari kupitia vyombo vya habari vya nje. Alikuwa akiamini
dharura ya kuwepo mipango, ratiba na udhibiti wa nafsi katika maisha, hivyo
alikuwa akitenga muda maalumu usiku na mchana kwa ajili ya ibada, dua, na
kisomo cha Qur’an. Alikuwa akishiriki mazoezi ya kutembea huku akimtaja
Mwenyezi Mungu na kufikiria mustakbali, kiasi kwamba alifanya kufikiria
mustakbali ni sehemu ya ratiba yake ya kila siku. Pamoja na kuwa na kazi nyingi
na mikutano ya mara kwa mara na viongozi wa utawala wa Kiislam lakini suala la
kukutana na watu wa kawaida alilipa umuhimu wa pekee, hivyo aliendelea na
ratiba yake ya kila wiki ya kukutana na familia za mashahidi hadi siku za
mwisho za maisha yake.Miaka mingi Imam Khomeini alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa
wa moyo, hivyo mwaka 1979 alipelekwa hospitali ya moyo Tehran kwa ajili ya
matibabu, lakini sababu hasa iliyokuwa chanzo cha kifo chake ni ugonjwa
uliyopatikana kwenye mfumo wa chakula hivyo alilazimika kufanyiwa upasuaji.
Imam alifariki dunia saa nne na dakika ishirini jumamosi usiku sawa na tarehe
3-6-1989, ikiwa ni baada ya kukaa hospitali muda wa siku kumi. Ilipofika tarehe
tano mwezi wa sita uliwekwa mwili wake uliyotakasika kwenye kiwanja kikubwa cha
kusalia cha jiji la Tehran
ili Umma wa Wairani uweze kumuaga. Kisha mwili wake uliyotakasika ulisindikizwa
na msafara wa watu zaidi ya milioni kumi wakiwa wamevaa na kujifunika mavazi
meusi huku wakimwaga machozi na kutoa sauti ya kuishiwa nguvu kutokana na
hasara waliyoipata ya kuondokewa na mtu mkubwa na kiongozi shupavu. Wawakilishi
wa vyombo vya habari walishindwa kuuelezea vilivyo au kuutolea picha halisi
msafa huo wa mazishi, kwani ulikuwa ni msafara wenye urefu wa kilometa kumi na
saba. Lakini wawakilishi wa vyombo vya habari vya kimagharibi bila hiyari yao wakaelezea msafara
huo wa mazishi kwa kusema: “Ulikuwa wa kipekee kwa ukubwa, na ni msafara ambao
haujawahi kupatikana mfano wake ulimwenguni.” Wakati huohuo wawakilishi wa
vyombo vingine vya habari kulikuwepo na waliripoti idadi ya washindikizaji wa
jeneza hilo kwa
kusema: “Walikuwa watu zaidi ya milioni kumi na saba. Mwili wake mtakatifu
ulizikwa pembezoni mwa makaburi ya mashahidi wa mapinduzi ya Kiislam, kwenye
moja ya kona za makaburi ya Zahraa mjini Tehran.
Maombolezo yalienea kona zote za Iran na kwa Waislam wengine wote
ulimwenguni kwa muda wa siku Arobaini huku sehemu zote zikiwa zimeenea bendera
nyeusi na vikao vya maombolezo kwa kupoteza mtetezi wa heshima ya Uislam. Na
sasa kaburi lake limekuwa ni sehemu na kituo cha Ziara
kwa kila siku kutembelewa na Waislam na watu huru kutoka
kona zote za dunia.
kona zote za dunia.