HADITHI YA KISHAMIYA (SHUKA).

1- Kwa jina la Mola, Karima ninatamka,
Kheri na salama kwa Hashima mzawa wa Makka,
Na watoto wake wema halikadhalika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


2- Hadithul kisaa, tukisoma kinasikika,
Watu wengi sana kila zama hawakushika,
Huo ni  msiba tunasema kwa kusikitika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


3- Kwenye Qur'an tukisoma, wazi imeweka,
Pia kwa hadithi za hashima inabainika,
Muhammadi Ali na Fatma wametwaharika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


4- Hassani Husseini waja wema wametwaharika,
Sura Ahzabu tukisoma inabainika,
Watu wa Tarehe na Hadithi wameliandika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


5- Toka kwa Jabir Answari wakuaminika,
Kasema Fatma yule mama alotwaharika,
Mtume kafika kwa Fatma kisha katamka,
Nyumabani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


6- Homa imenishika mwili wangu unatetemeka,
Ninasikitika baba yangu yalokufika,
Naomba Rabbuka akulinde na kudhoofika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


7- Baba kaniambiya, Fatma nipe lile shuka,
Ambalo latoka Yemeni, nitajifunika,
Nami kwa haraka ni kampatiya lile shuka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


8- Akajifunika nikaona,nuru inawaka,
Imeongezeka kama, mwezi uliokamilika,
Punde akafika na Hussani nikamuitika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


9- Ninaburudika kwa mwanangu, nakufarijika,
Naye katamka, manukato wapi yanatoka,
Inaaminika Babu yangu hapa amefika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


10- Kweli ana Homa, babu yako amejifunika,
Akasikitika akaenda, pale kwenye shuka,


Assalaam Aleyka babu yangu nije jifunika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


11- Tumwa kaitika nakusema umekubalika,
Hodhi kauthara ni Hassani unayeishika,
Ingiya kwenye shuka na Hassani akajifunika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


12- Nikwa madakika na mwanangu Husseini kafika,
Nikamuitika moyo wangu, ukaburudika,
Naye kataamka manukato, wapi yanatoka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


13- Inaaminika babu yangu hapa amefika,
Kweli amefika ana homa amejifunika,
Hata kaka yako na Mtume wamejifunika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


14- Naye akaenda kwa haraka pale kwenye shuka,
Assalaam Aleyka babu yangu nijejifunika,
Akamuitikia kamwambiya umekubalika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


15- Ingia haraka Emwanangu nina
uhakika,
Kupitiya kwako Umma wangu utashufaika,
Hassani Husseni na Mtume wamejifunika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


16- Ni kwa madakika baba Hussani naye kafika,
Nikamuitika kwa salaam aliyotamka,
Ali kauliza manukato wapi yanatoka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


17- Mtume wa Mungu yaonyesha hapa amefika,
Ni binamu yangu Muhammadi aliyetukuka,
Fatma naomba nieleze nipate hakika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


18- Kweli amefika ana homa amejifunika,
Na watoto wako kwa pamoja wamejifunika,
Ali kwa haraka akaenda pale kwenye shuka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


19- Assalaam Alayka kwa Mtume Ali katamka,
Ewe ndugu yangu niruhusu nijejifunika,
Tumwa kaitika akasema umekubalika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


20- Wewe ndugu yangu kwa Hashimu sote tunatoka,
Wewe utashika uongozi nikishaondoka,
Na bendera yangu ndiyo wewe unayeishika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


21- Akajumuika bwana Ali pale kwenye shuka,
Na mimi Fatma nikaenda pale kwenye shuka,
Nikasalimiya baba yangu akaniitika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


22- Nika muuliza baba yangu aliyetukuka,
Mtume wa Mungu bint yako nijejifunika,
Baba katamka E Fatma ingiya haraka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


23- Ni wewe Fatma kwenye mwili wangu unatoka,
Nilipoingiya ni watano tumekamilika,
Baba akashika ncha mbili sehemu ya shuka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


24- Baba akaomba usalama toka kwa Rabbuka,
Mkono mmoja wa kuliya juu kauweka,
Mola nakuomba watu wangu hawa kwa hakika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.

25- Ni wasiri wangu wasaidizi wauhakika,
Mwili wao ndiyo mwili wangu mimi bila shaka,
Damu yao ndiyo Damu yangu inafahamika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


26- Ninahuzunika pindi wao wakihuzunika,
Nampiga vita awapigaye hakuna shaka,
Nampa Amani yule awapaye kwa hakika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


27- Mimi ni aduwi kwa aduwi yao bila shaka,
Mimi nampenda awapendao kwa uhakika,
Kwangu wanatoka, hata mimi kwao ninatoka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


28- Mola teremsha usalama na zako baraka,
Rehema na Radhi msamaha kwako vinatoka,
Wape watu hawa hata mimi hayo nayataka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


29- Ondowa kabisa kwao hawa uchafu na Taka,
Mungu mwenye enzi kawaita enyi Malaika,
Kwenye mbingu zangu mnakaa nasema hakika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


30- Sikuumba mbingu na Ardhi zilokamilika,
Mwezi wenye Nuru wala Jua linalomulika,
Bahari mawimbi na Sayari inayozunguuka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


31- Bahari na mwenendo wa mawimbi vyote kwa hakika,
Dau zaeleya kwenye maji nakusalimika,
Ni mapenzi yangu kwa watano waliojifunika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


32- Hapo Jibril kauliza kwa Mola Rabbuka,
Ni akina nani waliopo kwenye hilo shuka,
Mola mwenye enzi kamwambiya huyu Malaika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


33- Ni watu wa Nyumba ya Mtume wamejifunika,
Na ndiyo asili ya Ujumbe uliyotukuka,
Ni watu watano shuhudiya wewe Malaika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


34- Hawo ni Fatma na babake wachini ya shuka,
Pia mume wake na wanawe wamejifunika,
Ndipo Jibril akaomba kwenda kwenye shuka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


35- Mola karuhusu Jibril endejumuika,
Akateremka kwa Mtume pale kwenye shuka,
Akamsalimu Muhammadi Assalaam Alayka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


36- Kisha katamka Jibril ndani kwenye shuka,
Salaam zatoka kwa Mwenyezi aliyetukuka,
Anakutukuza Muhammadi unaheshimika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


37- Kwa ushindi wangu ninaapa Mola katamka,
Sikuumba mbingu na Ardhi zilokamilika,
Mwezi wenye Nuru wala Jua linalomulika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


38- Bahari na mwenendo wa mawimbi vyote kwa hakika,
Dau zaeleya kwenye maji nakusalimika,
Ni mapenzi yangu kwa watano walokamilika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


39- Mtume wa Mungu sikiliza Mola atamka,
Kwa mapenzi yake kwenu nyinyi mlojifunika,
Kama siyo nyinyi vitu vyote asinge viweka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


40- Mungu karuhusu Jibril nijejifunika,
Vipi waruhusu Muhammadi nikajumuika,
Tumwa kaitika salaam yake Malaika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


41- Umekubalika Jibril, unaaminika,
Wahy wa Allah kwako wewe unahifadhika,
Ndipo Jibril kaingiya kwenye lile shuka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


42- Akamueleza baba yangu Mola katamka,
Mungu anataka awatowe uchafu na taka,
Nyumba ya Utume mtakaswe na kutwaharika,
Nyumbani kwwa Ali na Fatma kumesalimika.


43- Ali kauliza baba yangu ampe hakika,

Ni fadhila gani za kikao chetu kwenye shuka,
Zinapatikana mbele ya Mola wetu Rabbuka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.

44- Mtume kajibu ninaapa kwa Mola hakika,
Kanipa Utume na Risala ya kuaminika,
Risala ambayo wafuwasi wake huokoka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


45- Itapokumbukwa habari yetu hii hakika,
Hafla yoyote Aridhini wakikusanyika,
Na Mashia wetu na wapenzi wakajumuika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


46- Mwenyezi ashusha rehema zitamiminika,
Watahudhuriya jambo hilo hata Malaika,
Watawaombeya Maghfira yatakubalika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


47- Yataendeleya hadi pale wakitawanyika,
Ali akasema Wallahi tumekwishavuka,
Namashia wetu wamefuzu halikadhalika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


48- Kisha baba yangu Muhammadi tena katamka,
Sikiliza Ali ninaapa kwa Mola Rabbuka,
Kanipa Risala wafuwasi wake huokoka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


49- Hapa Aridhini kama watu wakikusanyika,
Katika hafla yoyote itayofanyika,
Na Mashia wetu na Wapenzi wakajumuika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


50- Kwa mwenye huzuni ni lazima itamuondoka,
Kila mwenye Ghammu hakikisha itamuondoka,
Kila mwenye haja atapewa anachokitaka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


51- Ali katamka Wallahi tumekwishavuka,
Tumebarikiwa Shia wetu halikadhalika,
Hapa duniani na Akhera nina uhakika,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


52- Kwa Mola wa Ka'ba ninaapa bila ya mashaka,
Tumeshaongoka Shia wetu wameshaongoka,
Salaam kwa Tumwa na Ahali walioongoka,
Nyumbani kwa Ali na Fatma kumesalimika.


Na: Juma S. Magambilwa