MASJID MUASASA AHLUL-BAYT (A.S), TANGA BARABARA YA ISHIRINI (20), YAOMBOLEZA KIFO CHA MTUME MOHAMMAD (S.A.W.W).



"Wanaume wana fungu katika yale waliyoyaacha wazazi na jamaa waliowakaribia, na wanawake wana fungu katika yale waliyoyaacha wazazi na jamaa walio wakaribia, ikiwakidogo au kingi, (hili ni) fungu lililofaradhishwa." Qur'an 4:7

Tukio la kufishwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) mbele ya jamii ni jambo geni sana, kana kwamba katika historia ya ulimwengu tukio hili halikutokea. Ingawa tukio la kuzaliwa kwa Mtume Muhammad limepokelewa kwa nafasi kubwa isiyo kifani. Kwa hiyo, unaweza kuona hafla mbalimbali za kusherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) zikifanywa Misikitini, Madrasani, Majumbani, na katika Mazawia mbalimbali. Hili ni jambo jema sana, swali lilipo hapa ni, je, huyu afanyiwae haya yu hai mpaka sasa? Au amekwisha kufa? Ni kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w) amekwisha kufa. Sasa, tarehe ya wafat wa Mtume, Waislamu wanaichukuliaje. Inafaa ikumbukwe tarehe hiyo ya wafat tarehe ambayo Mtume Muhammad (s.a.w.w) ndiyo alioaga dunia, au haifai kuikumbuka?! Ilikuwaje! Maulamaa wa Kiislamu na Masheikh wa Twariqa katika tarehe zao za wafat hukumbukwa kwa visomo mbalimbali. Hili ni jambo jema, isipokuwa tarehe ya wafat wa Mtume Muhammad!!! Mtume (s.a.w.w) alipokaribia kufariki, kama ilivyopokewa na Ibn Abbas, alisema: “Nileteeni karatasi niwaandikie maandiko hamtapotea baada yake. Umar akasema Mtume anaweweseka. Katika riwaya nyingine, Umar akasema: “Hakika Mtume yamemzidi maradhi, na tunayo Qur’an inatutosha. Mara wakakhitilafiana (wako waliosema aletewe, na wako waliozuia) fujo likazidi. Mtume akawaambia: “Niondokeeni, na wala haipendezi kuzozana mbele yangu”.

Taz:
Sahihi Bukhari:
Kitabul Itiswami bilkitabi wasunna, babu kara hiyatil khilafi.
Kitabul mardhaa, babu qawli quumuu anni.
Kitabun Nabi ila Kisra, babu maradhin Nabiyyi.
Kitabu Jihad, babu jawazil wafdi.
Kitabu IImi, babu kitabatil IImi.
Sahihi Muslim
Kitabul Waswiyya, babu tarkil waswiyya.

Kisha Mtume aliwaambia: “Niitieni Ali, Aisha akajibu: Laiti ungemwitisha Abubakar. Hafsa (naye) akasema: Laiti ungemwitisha Umar. (kila mmoja akawita baba yake) wakakusanyika mbele ya Mtume, Alipowaona Mtume akawambia: “Ondokeni nikikuhitajini nitakuiteni”.

Taz: Tarekhut Tabari J. 3 uk. 64

Mwana Aisha anasimulia kuwa: “Mtume alipougua maradhi aliyofia, aliamrisha Abubakar asalishe watu. Abubakar alipoingia Msikitini kutaka kusalisha, mara Mtume (s.a.w) akahisi woga, akatoka akiburuza miguu yake na huku ameshikiliwa na watu wawili (Ali na Abbas) alipoingia Msikitini, Abubakar akarudi nyuma ya safu, Mtume akakaa kuongoza swala.”

Taz: Tarekhut Tabari  J. 3 uk. 64
Almuntadham J. 2 uk. 470
Katika riwaya hii, kuna mambo matatu yanahitaji kuangaliwa kwa kina:

Abubakar ni katika Maswahaba walioamriwa na Mtume kutoka pamoja na jeshi la Usama. Kwa hiyo, amma Abubakar alikwenda na jeshi kama Mtume alivyoamrisha, na kwa hiyo hakusalisha kwa sababu hakuwapo. Amma alikuwapo, kwa hiyo alipinga amri ya Mtume ya kwenda na jeshi, na kwa hiyo Abubakar amelaaniwa. Mtume (s.a.w.w) alipougua maradhi aliyofia: “Aitiwe Ali” tu, na wala si mtu mwingine. Na wapiga kampeni walipoita kila mmoja baba yake, Mtume aliwafukuza mbele yake, “ondokeni”. Mtume (s.a.w.w) amefariki akiwa kifuani kwa Ali bin Abi Talib ndani ya chumba cha Fatima (a.s). Anasema Imam Ali (a.s) kuwa: “Niliitwa na Mtume nikakaa naye karibu, nikampakata, akawa akininong’oneza kwa muda mrefu, mpaka mate ya Mtume yakanitiririkia!! Mtume (s.a.w.w) akakata roho akiwa kifuani kwangu!!!

Taz: Assiiratun Nabawiyya, ya Najahu Attai J. 2 uk. 316
At-Tabaqatul kubra J.2 uk. 263
Mtume (s.a.w.w) alivyotoka akichechemea taabani, na huku ameshikiliwa na watu wawili, Abubakar akapisha mahala hapo. Ni jambo gani lililomlazimisha Mtume kutoka akiwa hali hii, ikiwa yeye ndiye aliyeamuru kusalisha Abubakar? Ni kitu gani tena kilichomsonga kusalisha watu hali amekaa kwa taabu na dhiki kubwa? Kisha Mtume (s.a.w.w) akaagiza liandaliwe jeshi kupelekwa Rom. Mtume (s.a.w.w) akamteua Usama bin Zayd, kijana wa miaka kumi na saba au kumi na nane hivi aongoze jeshi hilo. Hii ni baada ya kumaliza hafla ya tukio kubwa lililotokea Ghadiir Khom ambapo Aya za Qur’an zilitemshwa, na Tamko la Mtume kutolewa na Waislamu wakatoa Baia yao kwa Imam Ali bin Abi Talib (a.s). Mtume (s.a.w.w) akasisitiza Waislamu kujiandaa kutoka na jeshi hilo, akasema: “Andamaneni na  jeshi la Usama, Mwenyezi Mungu amlaani atakaebaki nyuma”.

Taz: Afatu As-habil hadithi Uk. 12
Almilal wannihal J. 1 uk. 20
Katika Maswahaba walioamriwa na Mtume kutoka na jeshi la Usama ni Abubakar na Umar.
Taz: At- Tabaqatul kubra J. 2 uk. 190
Tarekhul Yaaquuby J. 2 uk. 113
Tarekh Ibn Athiir J. 2 uk. 215
Almuntadhan J.2 uk. 458

Kitendo cha Mtume (s.a.w.w) cha kumtawalisha Usama bin Zayd katika jeshi hilo, kilipingwa vikali na maswahaba: “Amemtawalisha kijana mdogo juu ya Muhajirina na Ansar wakubwa wakubwa!” Baadhi ya maswahaba walisikika wakipinga. Khabari hii ikamfikia Mtume, akawatokea akiwa amefunga kitambaa kichwani, kwa maumivu makali ya kichwa aliyokuwa nayo, akawaambia: “Japokuwa mnashutumu kutawalishwa kwake (Usama) bila shaka mlikwisha shutumu kutawalishwa baba yake zamani. Na kwa hakika. Usama anafaa sana kwa uongozi, na baba yake alifaa kwa uongozi huo. Basi jiandaeni kwenda (na jeshi la) Usama, Mwenyezi Mungu amlaani atakaebaki nyuma”. Usama akatoka pamoja na kikundi kidogo cha jeshi, akapiga kambi nje ya mji wa Madina mahala paitwapo Jurf.

Taz: Siiratul Mustafa Uk. 685-686
Tarekh Ibn Athiir J. 2 uk. 215
Tarekhut Tabari J. 3 uk. 54-55

Je, ni maswahaba gani waliopinga uteuzi wa Mtume? Vipi waandishi wengi wa Tarekh wamejiziwia kutaja majina yao? Miongoni mwa maswahaba waliopinga uteuzi wa Mtume ni Abubakar bin Abi Quhafa! Alikataa kwenda na jeshi la Usama, na badala yake akaenda kwa mkewe Habiba bint Khaarija aliyoko kijijini Sunhi, (nje kidogo ya mji wa Madina) hakurudi mpaka alipojulishwa kuwa Mtume amefariki!!

Taz; Tarekh Ibn Athii J. 2 uk. 218
Assaqiifa, ya Najahu Attaai Uk. 172-176

Mtume (s.a.w.w) amefariki tarehe 28 Swafar siku ya Jumatatu mwaka wa kumi Hijria. Familia ya Mtume ikakusanyika tayari kwa mipango ya maziko. Umar bin Khattb kuona hivyo, akachukua upanga akawa akizunguka huku na kule katika eneo la Msikiti na nyumba ya Mtume. Umar kwa sauti yake ya juu akawa anaonya: “Wanafiki wanasema Mtume amekufa, na hakika Mtume hakufa, atakaesema Mtume amekufa nitakata shingo yake”. Mpaka alipofika Abubakar akitokea kijijini kwake Sunhi kwa mkewe, akaingia ndani alipolazwa Mtume (s.a.w.w). Alipotoka akasoma Aya: “Na hakuwa Muhammad ila ni Mtume aliyepitiwa na Mtume kabla yake. Basi je, akifa au akiuliwa mtarudi nyuma kwa visigino vyenu? Na atakaerudi nyuma visigino vyake hatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu atawalipa wanaoshukuru”. 3:144. Umar akasema: “Wallahi, kana kwamba watu hawajui kuwa Ayah ii ilishuka kwa Mtume”. Kisha Abubakar na Umar wakaondoka kwenda kwenye ukumbi wa Bani Saaidah kwa ajili ya uchaguzi.

Taz: Tarekh Ibn Athiir J. 2 uk. 219
Tarekhut Tabari J. 3 uk. 67-69
Nurul absaar Uk. 57-59

Kumbuka, Umar anasema: “Wanafiki wasema Mtume amekufa”. Je, ni nani wanafiki? Nyumbani kwa Mtume kuna: Ali bin Abi Talib, Fatima bint Muhammad, Abbas bin Abdil Muttalib, Alfadhl bin Abbas, Qutham bin Abbas, na Usama bin Zayd. (ilipotangazwa kuwa Mtume amefariki, Usama pamoja na kikundi chake cha jeshi walirudi mjini) Hawa ndiyo waliokuwamo nyumbani kwa Mtume pamoja na mwili wa Mtume, na ndiyo waliotangaza kifo cha Mtume. Kwa mtazamo wa Umar, hawa ndiyo wanafiki, na ndiyo aliokusudia kukata shingo zao!!

Abubakar na Umar hawakuhudhuria osho wala maziko ya Mtume, walikuwa kwenye ukumbi wa Bani Saaidah wakichaguana!!

Taz: Kanzul Ummal, kitabul khilafa maal-imaara khilafatu Abibakar
Almuswannaf, ya Ibn Shayba, babul Maghaz khilafatu Abibakar

Kama ambavyo, Mwana Aisha (mkewe Mtume) hakuhudhuria osho wala maziko ya Mtume, alipotea nyumbani kwa Mtume siku mbili, mwenyewe Mwana Aisha anasimulia hapa: “Wallahi hatukuelewa maziko ya Mtume mpaka tuliposikia kelele za majembe usiku wa Jumanne (wakati wakichimba kaburi):

Taz: Al-muntadham J. 2 uk. 482
Asiiratun Nabawiyya, ya Najah Attaai J. 2 uk. 314
Assunanul Kubra J. 3 uk. 574
Tarekhut Tabari J. 3 uk. 81

Kifo cha Mtume kinatatanisha, je, amekufa kifo cha kawaida au ameuliwa kwa sumu? Anasema Mwana Aisha kuwa: “Tulimnywesha dawa Mtume wakati wa maradhi yake, na Mtume akiwazuia: “Msininyweshe”.

Taz: Tarekhut Tabari J. 3 uk. 62
Fat-hul Baary J.10 uk. 175

Waandishi wa kiislamu wanasema kuwa: “Waliohusika kumnywesha dawa hiyo kwa nguvu ni Aisha na Hafsa (wakeze Mtume) na kwamba dawa hiyo ni sumu!!

Taz: Assiiratun Nabawiyya, ya Najahu Attaai J. 2 uk. 379
Alburhan fyilafsiril Quran J. 2 uk. 117
Tafsirul ‘Ayyaashy J. 1 uk. 224
Tafsirus Saafy J. 1 uk. 389-390

Mtume (s.a.w.w) alikoshwa, kuswaliwa, kuzikwa na: Ali bin Abi Talib, Abbas bin Abdul Muttalib, Qutham bin Abbas, Alfadhlu bin Abbas, na Usama bin Zayd. Mtume (s.a.w) amezikwa siku ya Jumatatu, amepewa Utume siku ya Jumatatu, amehama Makka kwenda Madina siku ya Jumatatu, amefika Madina siku ya Jumatatu, na amefariki siku ya Jumatatu.

Taz: Almuntadham J. 2 uk. 477
Tarekhut Tabari J. 3 uk. 80