AYATULLAH KERMANI: VITISHO HAVIWEZI KUIFANYA IRAN ISALIMU AMRI MBELE YA MATAKWA YA MAREKANI.


Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa mjini Tehran amesema kuwa, vitisho vya Marekani haviwezi kuifanya Iran isalimu amri mbele ya matakwa ya kutotosheka ya Washington.
Ayatullah Muhammad Ali Movahedi-Kermani amesema hayo mbele ya hadhara kubwa ya waumini waliohudhuria ibada ya Sala ya Ijumaa mjini Tehran na kuwaasa viongozi wa Marekani wajiepushe na kutoa matamshi ya vitisho dhidi ya Iran na vile vile waache kuingilia masuala ya ndani ya nchi za Mashariki ya Kati.
 

Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran ameongeza kuwa, kuendelea kutumia lugha za vitisho kutakabiliwa na radiamali kali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Movahedi-Kermani amesema kuchukuliwa dola bilioni mbili za Iran huko Marekani ni mfano hai wa uporaji wa wazi wa mali za taifa fulani na kubainisha kwamba, hatua hiyo itazifanya nchi nyingine kutokuwa na imani na Marekani kiasi cha kutokuwa tayari tena kuweka mali na fedha zao huko Marekani.
 

Amesema, katika mazungumzo ya nyuklia, Marekani iliahidi kufungamana na utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), lakini imekuwa ikifanya njama za kukwamisha mambo jambo ambalo limewathibitishia walimwengu kwamba, taifa hilo si la kuaminika.
 

Khatibu wa Sala ya Ijumaa ameashiria misaada na uungaji mkono kwa silaha na fedha wa baadhi ya nchi za Kiarabu na za Magharibi ikiwemo Saudi Arabia na Marekani kwa makundi ya kigaidi likiwemo la Daesh na kusisitiza kwamba, makundi hayo yamenunuliwa ili yafanye mauaji dhidi ya raia wa Mashariki ya Kati wakiwemo wa Iraq, Syria na Yemen na ili kwa njia hiyo mipango ya mabeberu iweze kufanikiwa. http://parstoday.com/…/iran-i7000-ayatullah_kermani_vitisho…