HOTUBA YA KIONGOZI MUADHAMU KWA MNASABA WA KUMBUKUMBU YA KUBAATHIWA MTUME (S.A.W.W).

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa kustafidi na ibra na mafunzo ya mab’ath na kubaathiwa Mtume SAW kwa ajili ya kukabiliana kwa umakini na ujahili wa kisasa hii leo, ambao ni hatari zaidi na uliojizatiti zaidi kuliko ujahili wa kabla ya Uislamu. Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema hayo alipokutana na viongozi wa mfumo wa Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu hapa mjini Tehran na matabaka tofauti ya wananchi na kusisitiza kuwa, uistikbari kinara wake akiwa Marekani ndio chanzo kikuu cha kutokea ujahili wa kisasa au ujahili mambo-leo. Kiongozi Muadhamu ameashiria kuzaliwa tena hii leo ujahili uliokuwako kabla ya Uislamu na kubainisha kuwa, ujahili huu umesimama juu ya misingi miwili ambayo ni matamanio na ghadhabu na kwamba, hii leo pia walimwengu wanashuhudia hawaa na matamanio zaidi yasiyo ya kimantiki, ukatili na mauaji yasiyo na mipaka. Amesema kuwa, tofauti ya ujahili wa kabla ya Uislamu na ujahili wa kisasa ni kwamba, ujahili wa leo kwa masikitiko makubwa umejizatiti kwa silaha ya elimu na ujuzi na ni hatari zaidi. Kwa hakika kile ambacho ametahadharisha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na ujahili wa kisasa, engo na athari zake ni ukweli mchungu na wakati huo huo unakumbusha tishio kubwa na athari zake zinaweza kuzifanya nchi ndugu za Kiislamu katika mazingira ya sasa kupigana wao kwa wao kama ambavyo hilo linashuhudiwa hivi sasa huko Yemen na bila shaka hilo ni natija ya mipango ya madola makubwa ya kibeberu yakiongozwa na Marekani. Marekani na madola mengine ya kibeberu yameuchanganya ujahili huu wa kisasa na madai yao ya uongo kwa shabaha ya kutaka kufikia malengo yao machafu katika Mashariki ya Kati. Vita dhidi ya ugaidi ni miongoni mwa madai yao hayo. Katika hali ambayo sio tu kwamba, madola hayo hayakabiliani kwa dhati na ugaidi, bali yamekuwa chanzo cha kujitokeza ugaidi huo. Fauka ya hayo, madola hayo yanayodai kuwa vinara wa kupambana na ugaidi yamekuwa yakiyaunga mkono makundi hatari kabisa ya kigaidi. Kwa hakika makundi ya kigaidi kama Daesh yamekuwa yakipata mafunzo na misaada ya kifedha na kisilaha kutoka Washington. Marekani na madola mengine ambayo yenyewe ndiyo yaliyouleta ugaidi na yamekuwa yakiuunga mkono kwa hali na mali, hivyo kama yanadai kwamba, yanapambana nao kimsingi yanafuatilia maslahi yao haramu ambayo yanayapata kupitia kuanzisha vita vya niaba na kwa kuziuzia silaha nchini za Kiarabu katika eneo, zimekuwa zikinufaisha makampuni yao ya kutengeneza silaha. Hali hii imekaririwa kwa senario tofauti katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita. Moja ya sifa maalumu ya senario hii ni madai ya uongo ya Marekani kuhusiana na usalama wa Ghuba ya Uajemi, katika hali ambayo, daima eneo hili limekuwa likikabiliwa na ukosefu wa usalama pindi vinapokuweko vikosi vya kigeni. Kama alivyobainisha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kuwa, Marekani haifuatilii suala la kudhamini usalama wa Ghuba ya Uajemi, lakini kama eneo hilo litakuwa salama hapana shaka kuwa nchi zote zitanufaika na na usalama huo, na vile vile kama litakabiliwa na ukosefu wa amani basi nchi zote za eneo zitakosa usalama na amani. Kutokana na kuweko tishio la kweli katika Mashariki ya Kati, Ayatullahil Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitaka nchi za eneo hili kuwa macho na siasa za kibeberu pamoja na njama zao za kuleta adui wa kutunga na kuzifanya nchi za eneo ziogopane na kuongeza kuwa, maadui hao wanafanya njama ili adui wa kweli ambaye ni ubeberu, wanaofungamana nao pamoja na Wazayuni wasizingatiwe, na hivyo kuzigonganisha vichwa nchi za Kiislamu. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akasisitiza kuwa, kuna ulazima wa kukabiliana na siasa hizi ambazo ndio ule ujahili wa kisasa na kusimama kidete dhidi ya ujahili huo.