NAFASI YA MAULAMA NA WANAZUONI KATIKA KUFIKISHA UJUMBE SAHIHI WA KIISLAMU.

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujumuika nami katika kipindi kingine cha Makala ya Wiki ambacho kwa leo kitajadili umuhimu wa maulama na wanazuoni wa Kiislamu katika kuongoza umma wa Kiislamu kwa njia sahihi.

Dini ya Kiislamu ndiyo dini iliyokamilisha dini na mafundisho ya Nabii Adam, Ibrahim, Musa na Issa (as). Kwa kipindi cha historia nzima, kwa kuzingatia daraja ya akili ya mwanadamau katika kudiriki mambo, Mwenyezi Mungu aliwaarifishia wanadamu dini ya kuwaongoza hatua kwa hatua hadi kufikia zama ambazo jamii, ingeweza kuikubali dini ya mwisho na kuiendeleza katika vizazi vijavyo. Hivyo Mwenyezi Mungu akaufanya Uislamu kuwa ndiyo dira ya maisha ya mwanadamu, huku akimpa jukumu la kufikisha ujumbe huo mzito wa dini hii ya milele, Mtume wake wa Mwisho ambaye ni Mtume Muhammad (saw). Kuhusiana na suala hilo, Qur'an Tukufu inasema: "…Leo nimewakamilishia dini yenu na kuwatimizia neema yangu na nimewapendelea Uislamu kuwa dini…" Surat al-Maida aya ya 3. Wataalamu wa masuala ya dini wamekiri kwamba, dini ya Kiislamu si tu kwamba ni kioo cha ibada kwa mtu binafsi, bali pia ni ratiba kamili kwa ajili ya kumfikisha mwanadamu kwenye utukufu katika kila pande za maisha yake. Kwa mtu binafsi kijamii, kisiasa na hata katika uga wa kisheria. Aidha dini ya Kiislamu inakidhi haja ya mwanadamu katika kila zama na mahala popote sanjari na kuzingatia pia mazingira ya utekelezwaji wake. Mbali na hapo, Uislamu haujapoteza mvuto wake hata kidogo, na hii ni kwa sababu msingi wa mipango ya dini hii imejikita katika maumbile ya mwanadamu.

****************************************

Katika muda wote wa utume wake, Mtukufu Mtume wa Uislamu (saw) alikabiliwa na maudhi ya washirikina na wanafiki wa zama zake. Na katika njia hii ndefu iliyojaa milima na mabonde pindi mtukufu huyo alipokuwa akiendelea na kazi ya kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya saada ya milele ya mwanadamu, kamwe hakuogopa  hatari yoyote. Mtume alipitia mateso, mashaka na maudhi mengi kwa ajili ya kumuongoza mwanadamu Mtume na kuchelea kwamba watu hawangemwamini. Kadiri kwamba Mwenyezi Mungu alimwambia: 'Huenda labda ukajikera nafsi yako kwa kuwa hawawi Waumini.'

Hadi mwisho wa uhai wake Mtume alitekeleza vilivyo jukumu la kuwaongoza watu na kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu huku akiamuriwa na Allah kumuainisha kiongozi baada yake sanjari na kumuarifisha kwa watu ili kwa njia hiyo kusije kukatokea ukengeukaji wa watu katika suala hilo.

Baada ya kumalizika kipindi cha uongozi wa Imamu wa 11 yaani Imam Hassan al-Askari na kuanza uongozi wa Imamu wa 12, Imam Mahdi-af, mtukufu huyo kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu alitoweka mbele ya macho ya watu na kuwa kama hazina ya Mwenyezi Mungu ambaye baada ya walimwengu kufikia daraja ya ukamilifu atafanikisha haki kuishinda batili, na kusimamisha utawala wa mwisho ambao utajengeka juu ya msingi wa haki, uadilifu na usawa. Kwa mujibu wa aya na riwaya kadhaa, katika kipindi cha ghaiba yake ndefu, Imamu Mahdi ambaye ndiye kiongozi baada ya Mtume saw kwa muda huu, ni maulama ndio watakaoilinda dini ya Mwenyezi Mungu kutokana na upotevu. Hii ndio sifa ya jamii ya mwanadamu katika zama za Mitume wa Mwenyezi Mungu waliopita. Kwa ibara nyingine ni kwamba, kwa kutumia uwezo na akili yake mwanadamu katika kipindi cha ghaiba ya khalifa wa zama zake, anatakiwa kushikamana na Qur’an, suna na hadithi ili kwayo aweze kutofautisha kati ya haki na batili na kuelekea kwenye njia iliyonyooka. Mtukufu Mtume (saw) anasema: “Maulama ni taa za ardhini, ni makhalifa wa Mitume na warithi wangu na Mitume wengine.” Mwisho wa kunukuu. Hapa ndipo tunapoweza kufahamu nafasi isiyo na mbadala ya maulama na wanazuoni wa dini ya Kiislamu. Imam Hadi (as) anasema: “Lau kama baada ya ghaiba ya (Imamu) msimamizi wetu kusingekuwepo maulama ambao wanawalingania watu kwake (Imam wa zama), na kuwafundisha watu juu ya uepo wake…na kuwaokoa waja wa Mwenyezi Mungu kutokana na ibilisi na wafuasi wake, bila shaka watu wote wangekengeuka kunako dini ya Allah.” Mwisho wa kunukuu.

*********************************************

Hivi sasa ambapo umma wa Kiislamu unakabiliwa na tishio la wimbi la mafuriko yanayoangamiza yanayotokana na fitina na mifarakano, ni wakati mwafaka kwa mtu kufahamu falsafa na sababu ya Uislamu kusisitiza juu ya nafasi ya maulama wa  Kiislamu. Kuhusiana na suala hilo, Mtukufu Mtume Muhammad (saw) anasema: “Wakati wowote kutakapodhihiri bidaa kati ya umma wangu, ni wajibu kwa alim wa kidini kudhihirisha elimu yake, na mtu yeyote atakayeacha kufanya hivyo, basi atalaaniwa na Mwenyezi Mungu.” Mwisho wa kunukuu. Kwa kipindi chote cha karne 14 tangu kudhihiri dini ya Kiislamu, maulama na wanazuoni wamekuwa wakifanya juhudi kubwa zisizo na kifani katika kuutetea na kuupigania Uislamu halisi. Tunaposema Uislamu halisi tunamaanisha Uislamu ule ambao Mtume Muhammad (saw) aliwafundisha Waislamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na akawasisitizia kushikamana nao kwa ajili ya kuhifadhiwa Qur’an na Ahlul-Bayti wa Mtume (saw). Uislamu sahihi ndio Uislamu ambao unajitenga na mitazamo na rai za mtu binafsi na kadhalika kujibari na tafsiri zisizo za kielimu. Sio Uislamu ule ambao kwa mujibu wa Qur’an, baadhi ya watu hufuata sehemu fulani ya mafundisho yake kwa kuzingatia manufaa yao, na kupuuza sehemu nyingine ya mafundisho ya dini hii tukufu inapotokea kuwa maslahi yao yako hatarini. Tablighi ya Uislamu wa kweli ni jukumu la wanazuoni na maulama ambao wametumia umri wao katika njia ya kuifahamu dini.

Ili kuzuia watu kuangukia katika mikono ya watu ambao wanajinadi kuwa maulama wa dini ya Kiislamu, lakini katika uhalisia wa mambo wanawaelekeza watu kwenye njia iliyo kinyume na uongofu, Qur’an Tukufu, hadithi na riwaya zimeweka wazi mlango kwa ajili ya watu wanaotaka kufahamu ukweli kuhusiana na suala hili. Mtukufu Mtume (saw) anasema: “Msikae na kila mtu anayejidai kuwa alim, isipokuwa alim ambaye atakulinganieni kukutoeni katika mambo matano na kukuiteni kwenye mambo matano, (1) kukutoeni kwenye shaka na kukupelekeni kwenye yakini, (2) kukutoeni kwenye uadui na kukuiteni kwenye kupenda kheri, (3) kukutoeni kwenye kibri na kukupelekeni kwenye unyenyekevu, (4) kukutoeni kwenye ria (kujionyesha) na kukuiteni kwenye ikhlasi, (5) kukutoeni kwenye kupenda dunia na kukuiteni kwenye kutoizingatia (dunia hiyo).” Kwa ajili hiyo alimu yeyote anayepiga ngoma ya mfarakano na akawa halinganii kwenye umoja na kupenda mema sambamba na kutoonyesha ramani ya kuepukana na shaka na upotevu, kwa hakika hafai kufuatwa. Kwa kuzingatia hayo, itawezekana vipi katika madhehebu ya Kiislamu hususan Mawahabi kwa mtu anayejiona kuwa aalim, kutoa fatwa mpya kila siku za kuzusha moto wa fitina na mifarakano baina ya Waislamu, kuwa mrithi wa Mitume? Hali hiyo inamuondolea mtu shaka kuhusiana na nafasi ya wafuasi wa watu wa aina hiyo mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

***************************************************

Tangu ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, wananchi Waislamu wa taifa hili wamepata tajriba kubwa, mojawapo ikiwa ni nafasi sahihi ya maulama katika kulinda dini na mapinduzi ya Kiislamu sanjari na kuwaepusha na kila aina ya upotevu. Katika harakati takatifu za kimapinduzi, mitetemeko ya kisiasa iliyotokana na harakati hizo na kadhalika njama za kuwachochea wananchi waachane na mapambano pamoja na dhulma na ukandamizaji, vingeweza kuandaa mazingira mazuri kwa maadui wa dini ili kuzima hisia za wananchi na hatimaye kupindisha malengo halisi ya mapinduzi hayo. Naam! Hali hii ilionekana wazi hivi karibuni huko Misri. Ni vyema kuashiria hapa kwamba katika kipindi cha harakati za mapinduzi ya Kiislamu nchini hapa, kuliibuka makundi mengi potofu huku kila kundi likijaribu kuvutia upande wake vijana ambao hawakuwa na uelewa wa mafundisho sahihi ya Uislamu. Baada ya kufikiwa mapinduzi nchini hapa, makundi hayo yakawa yanajaribu pia kuielekeza nchi kwenye vita vya ndani. Mauaji na machafuko ya ndani ya nchi na katika kipindi ambacho maadui wa nje walikuwa wameanzisha mashambulizi kwa nguvu zao zote dhidi ya taifa la Iran, ni baadhi ya mambo yaliyofanya hali ya wananchi kuwa mbaya zaidi. Makundi hayo yalikuwa yakijinadi kwa Uislamu na mapinduzi, sanjari na kuwahadaa vijana. Hata hivyo tajriba ya Iran iliyotokana na mchango wa maulama na wanazuoni wenye uelewa sahihi wa mambo ilifanikiwa kuzima njama za makundi hayo. Maulama wa Iran chini ya uongozi wa Imam Khomein (MA) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kutumia misikiti ambayo ilifanywa kuwa ngome imara kwa Waislamu, walifanya nyumba hizo za ibada kuwa vituo vya kuwaongoza vijana katika kukabiliana na itikadi potofu, hatua ambayo ilitumiwa pia na Mtume Muhammad (saw) baada ya hijra yake mjini Madina ambapo baada ya kuasisi msikiti aliufanya kuwa kituo cha kuimarisha umoja na ngome ya Uislamu.

Hivi sasa ulimwengu wa Kiislamu unapitia kipindi kigumu zaidi kati ya vipindi vyake vyote ambapo ndani yake si tu kwamba, Waislamu wanatakiwa kukabiliana na mashambulizi ya wazi ya adui kama vile Marekani na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, bali wanatakiwa pia kuwa macho na kukabiliana kwa uelewa na njama na mipango ya siri ya maadui hao yenye lengo la kuzusha mifarakano na kudhoofisha msingi wa mafundisho sahihi ya dini yao ya Uislamu. Vitendo vya kutisha vya makundi potofu na yasiyo na uelewa wa dini na yanayowahadaa vijana, yaani makundi ya kitakfiri ya Daesh, Boko Haram, Taleban, al-Qaidah, ash-Shabab nk, vinahitaji kukabiliwa na maulama wenye uelewa sahihi wa kidini katika kuuarifisha Uislamu halisi kwa vijana na Waislamu wote kwa ujumla. Tunamalizia kipindi chetu cha leo kwa hadithi ya Imam Baqir (as) inayosema: “Ikiwa maulama wataficha nasaha zao, basi watakuwa wamefanya khiyana, ikiwa mtu ataona upotevu (wa watu) na akakataa kuwaongoza, au akashindwa kufufua mioyo ya watu, basi ni kitendo cha aina gani kichafu atakuwa amekitenda!”

Wapenzi wasikilizaji kipindi chetu cha makala ya wiki kinaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar Shaban hadi wakati mwingine ninakuageni kwa kusema, kwaherini.