Polisi ya Uganda
imesema kuwa, inawasaka watu waliomuua Sheikh wa Kishia Sheikh Abdul
Qadir Sudi Muwaya na itahakikisha inawatia mbaroni. Hayo yameelezwa na
Jenerali Kale Kayihura, Mkuu wa Polisi ya Uganda ambaye amesisitiza
kuwa, hataondoka katika Wilaya ya Mayuge hadi watu waliomuua kiongozi
huyo wa Waislamu wa Kishia watakapotiwa mbaroni. Inspekta Jenerali wa
Polisi Kale Kayihura amewahakikishia wakazi wa Wilaya ya Mayuge kwamba,
jeshi la polisi limeanzisha msako mkali la kuwatafuta watu walimuua
kiongozi huyo wa kidini. Sheikh Abdul Qadir ambaye alikuwa muasisi na
mkurugenzi wa Taasisi ya Kiislamu ya Ahlul Bait alipigwa risasi siku ya
Alkhamisi na watu wasiojulikana mbele ya nyumba yake muda mfupi tu baada
ya kutoka katika msikiti wa Buyemba. Marhumu Abdul-Qadir ambaye katika
uhai wake amewahi kufanya kazi na gazeti lililowahi kupata umashuhuri
mkubwa la Sauti ya Umma lililokuwa likichapishwa nchini Iran na
kutarjumu pia vitabu kadhaa alijipatia umashuhuri mkubwa sio katika
Wilaya yake tu ya Mayuge bali hata katika maeneo mengine ya Uganda
kutokana na harakati zake za kidini na za kimaendeleo. Akiwa kiongozi wa
Taasisi ya Kiislamu ya Ahlul Bait (ABIF) marhumu Sheikh Abdul Qadir
ambaye alifahamika zaidi kwa jina la Doktoor Abdul Qadir alisimamia
ujenzi wa misikiti 50 katika maeneo mbalimbali nchini Uganda na
kudhamini gharama za masomo kwa watoto wasio na uwezo. Marhumu Abdul
Qadir alizikwa siku ya Ijumaa katika Wilaya ya Mayuge mashariki mwa
Uganda katika mazishi yaliyohudhuriwa na maafisa mbalimbali wa serikali
na wa kiusalama akiwemo Mkuu wa jeshi la Polisi nchini Uganda. Chanzo
cha habari: http://kiswahili.irib.ir/…/45511-polisi-ya-uganda-inawasaka…