'VITA IRAQ NI NJAMA DHIDI YA ULIMWENGU WA KIISLAMU'



Waziri wa Mambo ya Nje Iran Mohammad Jawad Zarif amesema, machafuko yanayoendelea hivi sasa nchini Iraq ni njama dhidi ya ulimwengu wa Kiislamu.
Zarif ameyasema hayo mjini Tehran alipokutana na Waziri wa Leba na Maendeleo wa Sudan, Ishraqa Sayyed Mahmoud.
Zarif aliongeza kuwa, mgogoro unaoendelea hivi sasa nchini Iraq unalenga kuzuia kujitokeza nguvu ya Waislamu katika nyuga za kieneo na kimataifa.
Zarif ameongeza kuwa nchi za Kiislamu zinapaswa kuwa waangalifu na kuwa na mtazamo wa kistratijia kuhusu matukio ya hivi sasa duniani kwa lengo la kuzia maadui kuwagonganisha.
Zarif amesema uhusiano wa Iran na Sudan ni mzuri na ni wa kistratijia.
Kwa upande wake Waziri wa Leba Sudan ametoa wito wa ushirikiano kati ya nchi za Kiislamu hasa Iran na Sudan ili kukabiliana na changamoto za pamoja.
Amesema hakuna kizingiti katika uhusiano wa kidugu na kirafiki baina ya nchi hizo mbili za Kiislamu na kuongeza kuwa Sudan daima itabakia kuwa muitifaki wa Iran.

RAIS WA YEMEN ASISITIZIA KUUNGWA MKONO PALESTINA.
Rais Abd Rabbuh Mansour Hadi wa Yemen amelaani vikali uchokozi na mashambulizi yanayofanywa mara kwa mara na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina na kusisitiza juu ya kuungwa mkono juhudi za wananchi wa Palestina za kukabiliana na uchokozi na chokochoko zinazofanywa na utawala huo ghasibu dhidi ya Wapalestina. Akizungumza kwa njia ya simu na Khalid Mash'al Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina 'Hamas', Rais Abd Rabbuh Mansour Hadi amesisitiza kwamba serikali na wananchi wa Yemen wanaunga mkono haki ya wananchi wa Palestina ya kuainisha mustakbali wao wa kuundwa serikali huru kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Kwenye mazungumzo hayo, Khalid Mash'al naye amezitaka nchi za Kiarabu kuchukua msimamo mmoja na madhubuti wa kuushinikiza utawala ghasibu wa Israel, ili urejeshe haki za wananchi wa Palestina. Kiongozi wa Hamas amesema kuwa, utawala wa Israel unatekeleza jinai za kivita na zilizo dhidi ya binadamu siku hadi siku na kukanyaga sheria za kimataifa. Mash'al amesema kuwa taasisi za kimataifa zinapasa kuchukua hatua za kuwafungulia mashtaka viongozi wa utawala huo ghasibu. Kiongozi wa Hamas amezitaka taasisi za kimataifa, watetezi wa haki za binadamu kote duniani kuchukua msimamo thabiti wa kukabiliana na uchokozi wa mara kwa mara wa utawala wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina.