Mwenyezi
Mungu (s.w.t) anasema: “Kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu,
umekuwa laini kwao. Lau ungekuwa mkali mwenye moyo mgumu, bila shaka
wangelikukimbia. Basi wasamehe na uwaombee maghfira na ushauriane nao katika
mambo. Utakapoazimia, basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu
anawapenda wamtegemeao.” (Surat al-Imraan: 159)
Ikiwa
unyenyekevu unatakiwa kwa kila mmoja wetu, basi Wanachuoni wa kidini wanafaa
zaidi na wanastahiki zaidi kuwa na tabia hii njema, kutokana na kusoma kwao
mafunzo ya Uislamu, na kujishughulisha kwao na ulinganiaji na uongozaji, na kwa
nafasi ya kidini waliyonayo katika macho ya watu, ambapo mtazamo wa watu wengi
kuhusu dini hupata kupitia mwonekano wao na mwenendo wao. Na kwa unyenyekevu na
tabia yao njema wanaipa dini sura nzuri na mwonekano mzuri unaovutia nafsi za
watu kwenye dini. Wanachuoni wakiwa wamepatwa na maradhi ya majivuno na
kujikweza, watafeli katika jaribio la kuvutia nyoyo za watu, na watatoa mfano
mbaya wa hali ya dini katika jamii.