WAISLAMU KENYA WALAANI WENYE MISIMAMO MIKALI:


Baraza Kuu la Waislamu Kenya SUPKEM limelaani kutumiwa baadhi ya misikiti mjini Mombasa kwa vitendo ambavyo imevitaja kuwa vya uhalifu.

Katibu Mkuu wa SUPKEM Adan Wachu amewalaani vijana ambao walitimuliwa na polisi kutoka Masjid Musa Jumapili na kusema 'Uislamu si ugaidi'. Ameongeza kuwa, ‘Baraza Kuu la Waisalmu Kenya limeshtushwa na vitendo vya uhalifu na vilivyo dhidi ya Uislamu vilivyotendwa na vijana wavamizi katika Masjid Mussa Mombasa.’ Amesema, SUPKEM haifahamu vijana hao wana imani gani na hivyo inawakana kabisa. Kiongozi huyo wa Waislamu Kenya amesema si sawa kutumia sehemu za ibada kwa ajili ya vitendo vya uhalifu. Aidha amesisitiza kuwa, vitendo vinavyofanywa na vijana hao ni kinyume cha mafundisho ya Qur'ani na Mtume SAW. Wachu amesema, SUPKEM inaunga mkono maimamu na uongozi uliopo katika misikiti yote na katika taasisi za Kiislamu Kenya. Aidha ametoa wito kwa serikali kuchukua hatua kali dhidi ya vijana hao wahalifu lakini ametaka misikiti iachwe wazi. Katibu Mkuu wa SUPKEM ametoa wito kwa Waislamu wote Kenya kuungana kukabiliana na ugaidi ambao amesema hauna uhusiano wowote na Uislamu. Baadhi ya watetezi wa haki za binaadamu wanasema vijana sita waliuawa Jumapili baada ya polisi ya Kenya kuuvamia Msikiti wa Musa mjini Mombasa kufuatia ripoti kwamba kulikuwa na vitendo vilivyo kinyume cha sheria ndani ya msikiti huo uliokumbwa na utata. (irib)