Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema madola yanayoingilia masuala ya ndani ya nchi nyengine ni kikwazo kwa maendeleo na kujitawala nchi za eneo hili. Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo mbele ya hadhara ya makamanda, maafisa na askari wa jeshi la anga kwa mnasaba wa siku ya jeshi hilo na kueleza kwamba madola hayo yanayoingilia masuala ya nchi nyengine yanataka kuwafanya wananchi wa mataifa ya eneo waamini kwamba kujitawala kwao bila ya kuwa na utegemezi kuna mgongano na kupata maendeleo lakini maneno hayo ni potofu na yamebuniwa na madola hayo tu. Akibainisha maana ya kujitawala bila ya kuwa na utegemezi Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliashiria mbinu za Ukoloni Mamboleo za kuwatumia vibaraka wao badala ya kujiingiza moja kwa moja katika nchi na kufafanua kwamba katika kukabiliana na Ukoloni Mamboleo, mbali na kupambana na udikteta wa ndani unaotawala inalazimu kukabiliana pia na Ubeberu wa nje unaounga mkono udikteta huo, kwa sababu kupambana na udikteta tu na kisha kufanya muamala na Uistikbari hakutokuwa na tija yoyote. Katika sehemu nyengine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amebainisha kuwa kutokuwa na utegemezi katika kujitawala maana yake si kususa na kuwa na muamala mbaya na nchi za dunia bali ni kujiwekea ngao na ngome ya kukabiliana na ushawishi wa nchi zinazotaka kuyatumia maslahi ya mataifa mengine kwa manufaa yao. Katika hotuba yake hiyo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha pia kama ninavyomnukuu:"Viongozi wa Marekani wanawaeleza viongozi wetu kwamba hawana nia ya kutaka kuubadilisha Mfumo wa utawala; wanasema uwongo, kwani kama wataweza hawatosita hata lahadha ndogo kufanya hivyo, lakini hawana uwezo kwa sababu Mfumo wa Kiislamu umeshikamana na imani, mapenzi na irada ya wananchi wote", mwisho wa kumnukuu. Kuhusiana na imani, mapenzi na irada hiyo ya wananchi, Ayatullah Khamenei amefafanua kama ninavyomnukuu tena:"Inshallah siku ya Bahman 22 (Februari 11) mtaona jinsi wananchi wa Iran watakavyojitokeza na kupaza sauti zao kuonyesha uimara, nguvu na uwezo wa taifa lao"…/
MAZUNGUMZO YA SERIKALI NA TALIBAN PAKISTAN YALAANIWA:
Waislamu wa Kishia nchini Pakistan wamelaani vikali mazungumzo ya amani kati ya serikali ya nchi hiyo na kundi la wanamgambo linalojulikana kwa jina la Tehreek-e-Taliban Pakistan. Baraza la Umoja wa Kiislamu nchini Pakistan jana liliandaa maandamano makubwa katika mji wa Karachi kulaani mazungumzo ya serikali ya Islamabad na kundi hilo la wanamgambo linalotuhumiwa kufanya mauaji makubwa. Waandamanaji hao wameyalaani mazungumzo hayo wakisema hayatakuwa na natija na kwamba, lengo lake ni kupoteza muda. Taarifa ya Baraza la Umoja wa Kiislamu Pakistan imesema kwamba, kundi hilo linataka kununua muda ili lipate fursa ya kuendelea kuwashambulia Waislamu. Ali Hussein, mmoja wa wajumbe wa baraza hilo, ameiambia kanali ya televisheni ya Press TV kwamba, serikali ya Waziri Mkuu Nawaz Sharif inawapatia wanamgambo hao wa Tehreek-e-Taliban Pakistan fursa zaidi ya kuwaua raia wasio na hatia. Viongozi Waislamu wa madhehebu ya Kishia nchini Pakistan wameitaka serikali ya nchi hiyo iunde kamisheni ya mahakama kwa ajili ya kushughulikia vitendo vya ukatili dhidi ya raia.
HATUA MPYA ZA KIUSALAMA ZA KUPAMBANA NS MATAKFIRI NCHINI LEBANON:
Kufuatia kujipenyeza makundi ya kigaidi ndani ya ardhi ya Lebanon na kushadidi mashambulizi ya miripuko katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, jeshi la Lebanon limetangaza kuwa limeanzisha chumba cha oparesheni maalumu za kijeshi kwa ajili ya kuzuia mashambulizo ya kigaidi nchini humo. Mamia ya raia wa Lebanon wameuawa au kujeruhiwa katika mashambulizi ya kigaidi hususan utegaji mabomu yaliyofanywa na makundi ya kigaidi ya kitakfiri wiki kadhaa zilizopita katika maeneo mbalimbali ya Lebanon ikiwa ni pamoja na huko Hermel kaskazini mashariki mwa Lebanon na Beirut mji mkuu wa nchi hiyo.
Duru za habari za Lebanon zimeripoti kuwa, katika hali ambayo vyombo vya usalama vya nchi hiyo vimetangaza uamuzi wa magaidi wa kitakfiri wanaowakufurisha Waislamu wengine wa kubadili mbinu za utekelezaji wa oparesheni zao, uongozi wa jeshi la Lebanon pia umeasisi chumba cha oparesheni maalumu za kijeshi ili kutekeleza mipango ya kiusalama lengo likiwa ni kukabiliana na makundi hayo ya kigaidi ambayo mengi miongoni mwayo yaliingia katika ardhi ya Lebanon kwenye miezi ya hivi karibuni baada ya kushindwa katika mapigano huko Syria.Vikizungumza na duru za habari za huko Lebanon,vyombo vya usalama vya nchi hiyo Alkhamisi iliyopita vilieleza kuwa magaidi wa kitakfiri wameamua kufanya mashambulizi ya kushtukiza huko Lebanon. Makundi hayo ya kigaidi sasa yamekuwa yakiwatumia wanawake kuwabebea mada za miripuko, mabomu na mikanda ya kujiripua, kwa sababu kwa kawaida wanawake huwa hawakaguliwi katika maeneo muhimu ya vituo vya upekuzi.
Jeshi la Lebanon limeimarisha hatua za kiusalama ili kuzuia mashambulizi ya makundi ya kigaidi ya kitakfiri katika hali ambayo sheikh wa kitakfiri Omar al Atrash wiki iliyopita alisema kuwa makundi hayo yamejiandaa kufanya oparesheni kubwa za uripuaji mabomu huko Lebanon.
Kundi la kigaidi la an Nusra ambalo lilikiri kuhusika katika mripuko wa kigaidi wa hivi karibuni kwenye eneo linalokaliwa na Waislamu wa Kishia la Dahiya huko kusini mwa Beirut pia limetoa taarifa likitishia kuwashambulia viongozi na vituo vya Waislamu wa Kishia hususan vya harakati ya Hizbullah kwa lengo la kile ilichokitaja kuwa eti ni katika kutetea haki za Waislamu wa Kisunni. Hii ni katika hali ambayo viongozi na shaksia wa kidini na kisiasa wa Lebanon katika siku za hivi karibuni wameashiria kuenea hatari ya ugaidi wa kitakfiri katika eneo la Mashariki ya Kati hasa huko Lebanon na kueleza kuwa hivi sasa eneo hili limegeuka na kuwa uwanja wa ugaidi na kwamba magaidi wa kitakfiri wameuweka hatarini usalama wa nchi hiyo kwa kuingia huko Lebanon kutokea Syria. Ni wazi kwamba kuendelea kwa harakati za kigaidi na kufichuliwa nafasi ya makundi yenye mfungamano na genge al Nusra katika miripuko ya hivi karibuni huko Beirut ambayo yanaungwa mkono moja kwa moja na Saudi Arabia, kumewapelekea viongozi na shakhsia mbalimbali wa nchini Lebanon kusisitiza kuwa, miripuko ya kigaidi si tu kuwa imelilenga eneo moja au kundi fulani, bali inalenga Lebanon nzima na kwa sababu hiyo wametaka kufanyika mazungumzo ya kitaifa ili kuchunguza sababu na vyanzo vinavyopelekea kushuhudiwa vitendo hivyo. Aidha wametaka kuchukuliwa hatua za lazima kwa ajili ya kukabiliana na makundi ya kigaidi ambayo yanajali tu kutekeleza matakwa ya mabwana zao bila ya kuthamini damu za watu wasio na hatia iwe ni Waislamu au Wakrtisto au Waislamu wa Kisuni au wa Kishia.
ROUHANI: OIC IZUIE MAUAJI DHIDI YA WAISLAMU:
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa miongoni mwa majukumu muhimu ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ni kuimarisha umoja wa Waislamu, kuzuia machafuko na vitendo vya kuuawa Waislamu. Dakta Hassan Rouhani alisema hayo jana Jumatano alipokutana na Iyad Amin Madani, Katibu Mkuu wa jumuiya ya OIC mjini Tehran. Huku akiashiria njama zinazofanywa ili kuonesha kuwa Uislamu ni dini ya machafuko ma ukatili, Rais Rouhani amesema jumuiya ya OIC inapaswa kusahihisha mtazamo huo usio sawa na kuonesha waliwengu taswira halisi na ya upendo na huruma ya Uislamu.
Kwa upande wake Iyad Amin Madani amesisitiza ulazima wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuendelea kuunga mkono taasisi hiyo muhimu ya Kiislamu na kusema kuwa, hatua za kivitendo zinapaswa kuchukuliwa ili kuimarisha umoja katika ulimwengu wa Kiislamu na kushikamana zaidi mataifa ya Waislamu.
Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC) iliundwa mwaka 1969 kwa lengo la kuimarisha umoja baina ya nchi za Waislamu katika kukabiliana na njama za maadui na kutekeleza kivitendo matakwa ya Waislamu. Miongoni mwa matukio yaliyopelekea kuundwa jumuiya ya OIC yenye wanachama 57, ni kuchomwa moto Masjidul Aqswa, kibla cha kwanza cha Waislamu. Utendaji wa jumuiya hiyo ambayo mwaka 2011 ilibadilishwa jina na kuwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, kwa sasa unashughulisha fikra za waliowengi katika ulimwengu wa Kiislamu. Tunapoangalia utendaji wa taasisi hiyo tangu ilipoundwa hadi sasa, tunaona kuwa jumuiya hiyo muhimu na kubwa zaidi baada ya Umoja wa Mataifa, haijafanikiwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Hali ya sasa ya Quds Tukufu, kushadidi mashambulio ya Wazayuni dhidi ya Masjidul Aqswa, kutokuwa na ubunifu katika mgogoro wa Syria, mauaji ya Waislamu wa Myanmar na kuongezeka mauaji ya Waislamu katika nchi mbalimbali hasa Pakistan, Afghanistan na Iraq ambayo yanasababishwa na fikra za kiwahabi na kisalafi, yote hayo yanaonesha kuwa OIC haitatekeleza majukumu yake inavyotakiwa. Miongoni mwa malengo muhimu ya taasisi hiyo kubwa ya Kiislamu yenye wanachama kutoka mabara tofauti ni kulinda maslahi ya Uislamu duniani.
Changamoto muhimu zaidi zinazowakabili Waislamu hivi sasa ni njama zinazofanywa na Wamagharibi za kuudhihirisha Uislamu kuwa tishio, fikra ya Uwahabi, makundi ya takfiri na kutokuwepo umoja baina ya nchi za Waislamu kwa ajili ya kutatua migogoro tofauti hasa mgogoro wa Syria. Kwa msingi huo Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu inatarajiwa kusahihisha haraka iwezekanavyo fikra zisizo sahihi kuhusu Uislamu na kuwabainisha walimwengu sura halisi ya dini ya Uislamu na Mtume Mtukufu Muhammad (SAW).
Masuala kama takfiri kwa maana ya kukufurisha Waislamu wengine, mauaji na ugaidi haviwiani na mafundisho ya dini ya Uislamu lakini maadui wanawaajiri vibaraka wao wanaowatumia kuwatisha watu na kuchafua sura safi ya Uislamu katika mradi wa propaganda chafu dhidi ya dini hiyo ya Mwenyezi Mungu. Kielelezo cha mradi huo kinaonekana vyema zaidi nchini Syria. Hii leo magaidi wanaoungwa mkono na nchi za Magharibi na vibaraka wao wameilenga Syria tena kwa kutumia majina bandia ya Kiislamu ambako wanawakufurisha Waislamu na kuwaua kinyama.
Jinai zinazofanywa na magaidi nchini Syria ikiwa ni pamoja na kutafuna na kula mioyo ya wahanga wao mbele ya kamera, kuwaua kinyama wanawake na watoto na kadhalika vinaonesha kuwa, Jumuisha ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) haijatekeleza majukumu yake ipasavyo. Kama alivyosema Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, OIC inapaswa kufikisha sauti ya umoja na mshikamano wa Kiislamu kwa mataifa yote na kuzuia vitendo vyote vinavyokebehi na kuvunjia heshima itikadi za Kiislamu na kuua wafuasi wa dini hiyo.