SHEIKH SIDDIQI: IRAN HAITASALIMU AMRI MBELE YA VITISHO.


Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amesema kuwa, hakuna wakati ambao taifa hili lilisalimu amri mbele ya vitisho na mabavu ya mabeberu na kwamba, katu halitafanya hivyo.

Hujjatul - Islam Walmuslimin Kadhim Siddiqi amesema hayo mbele ya hadhara ya waumini waliohudhuria ibada ya Sala ya Ijumaa mjini Tehran na kubainisha kwamba, makubaliano ya Iran na kundi la 5+1 huko Geneva ni mtihani na mbinu ya kiufundi kwa ajili ya kuwa kifua mbele na adhama ya ulimwengu wa Kiislamu. Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amesema kuwa, wananchi wa Iran wanaiunga mkono timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran na ameitaka timu hiyo ya mazungumzo kuwa makini katika mazungumzo hayo na ilinde maslahi na mistari myekundu ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hujjatul - Islam Walmuslimin Kadhim Siddiqi amezungumzia matukio ya Lebanon na kubainisha kwamba, Hizbullah ilikuwa harakati ya kwanza iliyobatilisha fikra ya kutoshindwa utawala haramu wa Israel na kuwabainisha wazi walimwengu wote miujiza ya muqawama.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa ameashiria jinai za Ariel Sharon "chinjachinja wa Sabra na Shatila" Waziri Mkuu wa zamani wa utawala ghasibu wa Israel aliyeenda jongomeo hivi karibuni na kusikitishwa mno na hatua ya Wamagharibi ya kutoa mkono wa pole kwa kifo cha mtenda jinai huyo. (irib)