KIONGOZI MUADHAMU: HATUNA IMANI NA MAREKANI.



Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesifu hatua ya vijana waumini na mashujaa wa Vyuo Vikuu vya Iran ambao tarehe 13 Aban mwaka 1358 Hijria Shamsia sawa na tarehe 4 Novemba 1979 waliuteka ubalozi wa Marekani hapa mjini Tehran na kufichua uhakika wa mambo maovu yaliyokuwa yakifanyika kwenye ubalozi huo ambao kwa hakika lilikuwa ni pango la kijasusi na kuwatangazia walimwengu uovu mkubwa wa Marekani.

Ayatullahil Udhma Khamenei, amesema hayo leo asubuhi wakati wa maadhimisho ya siku hiyo ambayo huadhimishwa kila mwaka na ambayo hapa Iran inajulikana kwa jina la Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari. Amesema hayo mbele ya maelfu ya wanachuo na wanafunzi wadaraja mbalimbali za masomo na kuongeza kuwa, siku ya tarehe 4 Novemba 1979, wananchi wa Iran waliupachika jina la pango la kijasusi ubalozi wa Marekani wa mjini Tehran na leo hii, baada ya kupita zaidi ya miongo mitatu, balozi za Marekani katika nchi za Ulaya ambazo ni marafiki na waitifaki wa karibu wa Marekani, nazo zimekuwa mapango ya kijasusi na jambo hilo linathibitisha kuwa, vijana wa Iran walikuwa mbele ya takwimu ya historia zaidi ya miaka 30 iliyopita.

Ayatullahil Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, serikali ya Marekani ni serikali ya kibeberu ambayo inajipa haki ya kuingilia masuala ya ndani ya mataifa yote ya dunia. Ameongeza kuwa, kwa mapinduzi yake matukufu, taifa la Iran limesimama kikwelikweli kupambana na ubeberu wa uistikbari wa Marekani na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia, wananchi wa Iran walikata kikamilifu mzizi wa mabeberu na wala hawakuwa kama watu wa nchi nyingine, walioacha njiani mapambano yao na mwishowe wakapata madhara.

Vile vile amesisitiza kuwa, kuwalegezea kamba mabeberu hakuna faida yoyote kwa nchi na kwa taifa lolote lile na kuongeza kwamba, miamala ya kibeberu ya Marekani imeyafanya mataifa mengine duniani kutoiamini hata kidogo nchi hiyo, kama ambavyo pia uzoefu umethibitisha kuwa taifa na serikali yoyote inayoiamini Marekani mwisho wake hupata pigo hata kama ni miongoni mwa marafiki wa Marekani.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha nukta muhimu na ya kimsingi kuhusu masuala yanayoendelea hivi sasa baina ya Iran na Marekani na sambamba na kuwaunga mkono vilivyo viongozi wa Iran wanaofanya bidii za kila upande amekumbusha kuwa, historia ya vitendo vya Marekani vinaonesha kuwa, kadhia ya nyuklia inatumiwa kama kisingizio tu na nchi hiyo ili kuendelea uadui wake dhidi ya Iran.

Vile vile amesema, tangu zamani tulisema, hivi sasa pia tunasema na katika siku za usoni aidha tutasema kwamba, utawala wa Kizayuni ni utawala usio wa kisheria, bali ni mwana wa haramu. Chanzo cha habari: http://kiswahili.irib.ir/habari/kiongozi/item/35810-kiongozi-muadhamu-hatuna-imani-na-marekani