HUZUNI SIKU YA ASHURAA.

KUVAA NGUO NYEUSI SIKU YA HUZUNI.

Wengi katika Maulamaa wetu wakubwa na Mafaqihi watukufu wameona kwamba ni Mustahabu kuvaa nguo Nyeusi katika kuomboleza kifo cha Imam Hussein (a.s). Miongoni ni mwa Mafaqihi wapo ni Sayyed Hussein Al-Qummiy na Sayyed Al-Hakim ambao walikuwa wakivaa nguo Nyeusi kwa kipindi cha miezi miwili.
Ada hii inatiwa nguvu na riwaya kutoka kwa Maimam wa nyumba ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w). Al-Barqiy anaripoti kwamba Umar bin Zaynul-Abdin alisema: “Pindi alipouliwa babu yangu Hussein (a.s) Wanawake wa Bani Hashim walivaa katika kumuomboleza nguo Nyeusi na walikuwa hawalalamiki kuhusu joto wala baridi. Na alikuwa Ali bin Hussein (a.s) akiwatengenezea chakula kwa ajili ya vikao vya kilio (Maatam).


 Siku ya Ashura ni siku ya msiba na kilio. Ni vyema kuzingatia ada na taratibu za msiba. Kwa sababu hiyo ni vizuri kuacha kula na kunywa hadi nyakati za mwisho wa mchana. Tunakumbuka watu wa nyumba tukufu ya Mtume (s.a.w.w) kwa njaa yao na kiu, namna walivyoteseka katika vita hadi walipokufa Mashahidi na hivyo kuwa hai na kuruzukiwa na Allah kama anavyosema katika Aya ya 3:169

 Kitendo cha kulia na kuomboleza kifo cha Imam Hussein (a.s), kimefanywa na mbora wa viumbe Mtume Muhammad (s.a.w.w) alimpenda Imam Hussein (a.s) na kumuenzi. Msiba huu adhimu wa Mtume (s.a.w.w) bila shaka uliwaliza Mitume waliotangulia……Imam Ali bin Abi Talib (a.s), Bibi Fatma Zahra (a.s) na Imam Hassan (a.s) wote hawa walimlilia Imam Hussein (a.s), na baada ya tukio lenyewe, Maimam wote wa nyumba ya Mtume, walimlilia mara kwa mara Imam Hussein (a.s) kwa uchungu sana.

 Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) na watu wa nyumbani kwake, Masahaba, watu wa Madina na Waislam wapenzi wa Bwana Mtume (s.a.w.w) walimlilia Imam Hussein (a.s). Watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w) waliomboleza msiba wa Imam Hussein (a.s) katika uwanja wa Karbala, Sham na waliporejea Madina waliweka msiba na kilio na kuasisi ada ya Majalisi za Imam Hussein (a.s).
Msafara wa watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w) ulielekea Karbala na kumzuru Imam Hussein (a.s). Pia baadhi ya Masahaba kama vile Jabir bin Abdillah Al-Ansariy na jamaa wa Bani Hashim walikwenda Karbala na kujumuika na msafara wa Ahlul-Bayt (a.s).