RAIS HASSAN ROHANI: IRAN INAJITAHIDI KUZUIA VITA SYRIA.


 Rais Hassan Rohani wa Iran amesema Tehran inafanya kila iwezalo kuzuia vita dhidi ya Syria huku akionya kuwa uingiliaji wa kijeshi na madola ya kigeni nchini Syria ni jambo litakalokuwa na taathira mbaya katika eneo hili.
Akizungumza mjini Tehran leo Jumanne katika Kikao cha Maimamu wa Sala ya Ijumaa, Dkt. Rohani amesema katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, serikali imetumia uwezo wake wote kuzuia vita.
Rais wa Iran ameongeza kuwa wanaopiga ngoma za vita na waitifaki wao katika eneo hili la Mashariki ya Kati ndio watakaopata hasara zaidi iwapo watu wa Syria watalazimishwa kupigana vita. Rohani amesisitiza kuwa 'Syria ina umuhimu wa kipekee kwa Iran kwa sababu ni mwanachama wa harakati ya mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.'
Rais wa Iran amesema hata Bunge la Uingereza ambayo ni muitifaki mkubwa wa Marekani limepiga kura ya kupinga vita dhidi ya Syria.
Wakati huo huo, Rais Rohani amesema kuwa hakuna mafanikio yatakayopatikana katika mazungumzo kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran iwapo nchi za Magharibi hazitaiheshimu Iran. Amesema nchi za Magharibi zinapaswa kufahamu lugha ya serikali ya Iran kuwa ni lugha ya ustaarabu unaoandamana na mapambano. Aidha amesema nchi za Magharibi zinapaswa kufahamu kuwa haziwezi kufanikiwa katika siasa zao za kulishinikiza na kuliwekea vikwazo taifa la Iran.

 Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ametahadharisha kuhusiana na shambulio tarajiwa la Marekani dhidi ya Syria. Sheikh Naim Qassim ameonya kwamba, shambulio la kijeshi la Marekani dhidi ya Syria ni hatari kubwa kwa Mashariki ya Kati na ulimwengu kwa ujumla. Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, nchi za Kiarabu ambazo zinaunga mkono kushambuliwa kijeshi Syria hazitaki kuona amani na usalama vinatawala katika Mashariki ya Kati. Sheikh Naim Qassim amesisitiza kuwa, mgogogoro wa Syria unapaswa kutatuliwa kwa njia za kisiasa. Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kwamba, kushambuliwa kijeshi Syria kutakuwa na maafa na madhara kwa wananchi wa Syria na eneo zima la Mashariki ya Kati.

Iran imesema inakaribisha pendekezo la Russia kuhusu Syria kuweka maghala yake ya kemikali chini ya usimamizi wa kimataifa.
Akizungumza leo Jumanne na waandishi habari mjini Tehran, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bi. Marziyeh Afkham amesema 'Iran inalitazama pendekezo hilo kuwa katika fremu ya kuzuia sera za kivita katika eneo hili'.
Pendekezo hilo la Russia pia limepokewa vizuri na serikali ya Syria katika kikao kilichofanyika kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov na mwenzake wa Syria Walid Muallem jana Jumatatu mjini Moscow.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amongeza kuwa, Tehran inapinga utumiaji wa silaha za kemikali katika eneo hili na kwamba inataka ziangamizwe.
Siku ya Jumatatu Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Mohammad Javad Zarif alisema kuna ushahidi wa kutosha unaoonyesha kuwa makundi ya Kitakfiri nchini Syria ndiyo yanayomikili silaha za kemikali.
Wakati huo huo Mkurugenzi wa Kanali ya Press TV Dkt. Mohammad Sarafraz amesema kuwa, mwandishi wa Press TV nchini Uturuki ameshuhudia namna Marekani inavyowaingiza Syria magaidi wa al-Qaeda kwa kutumia magari ya wagonjwa ya Shirika la Afya Duniani, WHO.
  
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia imetangaza leo kuwa, kuna ushahidi wa kutosha unaothibitisha kuwa, video ya wahanga wa mauaji ya silaha za kemikali wanaodaiwa kuuliwa na jeshi la Syria, ni ya bandia. Aidha Wizara hiyo imesisitiza kuwa wataalamu wa kimataifa wamewasilisha ushahidi wa kutosha katika duru ya 24 ya kikao cha kutetea haki za binaadamu iliyofanyika mjini Geneva, Uswisi ukionyesha kuwa video hiyo inayotumiwa na madola ya Magharibi ikiwemo Marekani kudai kwamba serikali ya Damascus ndiyo iliyohusika na shambulizi hilo huko katika mkoa wa Rif Dimashq, ni ya bandia. Katika kikao hicho, wajumbe wa kikao hicho walilaani vikali vitisho vya serikali ya Washington vya kutaka kuishambulia kijeshi Syria bila ya kibali cha Umoja wa Mataifa, na kusema kuwa, hatua hiyo inahesabiwa kuwa ni ukanyagaji ulio wazi wa sheria za kimataifa. Kwa upande mwingine Russia imetangaza kuwa hivi karibuni itawasilisha dondoo za mpango wake mpya wa kutatua kadhia ya silaha za kemikali huko nchini Syria. Leo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia Sergey Lavrov amesema kuwa, Moscow kwa kushirikiana na serikali ya Damascus, itawasilisha mpango huo ulio wazi wa kutatua kadhia hiyo na kuzikabidhi pande husika ikiwemo Marekani. Aidha Lavrov amesisitiza juu ya udharura wa kukamilishwa uchunguzi wa watafiti wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria. Amesema kuwa, wale wote waliohusika na utumiwaji wa silaha hizo, lazima waadhibiwe. Hii ni katika hali ambayo serikali ya Syria imekaribisha pendekezo la Moscow la kuziweka silaha zake za kemikali chini ya uangalizi ya Umoja wa Mataifa. Aidha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu nayo imekaribisha mpango huo wa Russia kuhusiana na kadhia ya silaha za kemikali za Syria. Hii ni katika hali ambayo Katibu Mkuu wa chama cha Demokrasia nchini Lebanon amesema kuwa, hatua ya kusitishwa mashambulizi ya Marekani nchini Syria, imetokana na uwezo wa harakati za muqawama katika eneo hili. Walid Barakat amesisistiza kuwa, lengo la Marekani la kutaka kuishambulia kijeshi nchi hiyo ya Kiarabu, ni kujaribu kusambaratisha muqawama katika eneo la Mashariki ya Kati na kwamba, uwezo mkubwa wa muqawama unaoanzia nchini Iran hadi Lebanon, umeifanya serikali ya Washington, kuogopa kuivamia kijeshi Syria. Chanzo cha habari
http://kiswahili.irib.ir/habari