MSIMAMO WA IRAN MKABALA NA UAMUZI WA EU KUHUSU HIZBULLAH.


Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, kunyamaza kimya Umoja wa Ulaya (EU) mbele ya jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel na kulitaja tawi la kijeshi la harakati ya Hizbullah ya Lebanon kuwa ni kundi la kigaidi ni ishara ya siasa za kindumakuwili na kibaguzi za nchi za Ulaya. Ghulamhussein Dehqani amekosoa uamuzi wa hivi karibuni wa Umoja wa Ulaya wa kuliweka tawi la kijeshi la Hizbullah katika orodha ya makundi ya kigaidi na kueleza kuwa, kutolaaniwa vitendo vya ugaidi vya utawala wa Israel kwa upande mmoja na kuliweka tawi la kijeshi la Hizbullah ya Lebanon katika orodha ya makundi ya kigaidi kunaashiria muamala wa kindumakuwiki na siasa za kibaguzi za Ulaya kuhusiana na ugaidi. Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, harakati ya Hizbullah ya Lebanon ni kundi la muqawama linaloendesha mapambano dhidi ya maghasibu na sehemu ya muundo wa kijamii wa Lebanon na kwamba, uamuzi huo wa Umoja wa Ulaya utaifanya hali ya mambo ya Mashariki ya Kati kuwa tata zaidi.

Wawakilishi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran yaani bunge pia wametoa taarifa wakilaani hatua hiyo ya Umoja wa Ulaya na wameitaja Hizbullah ya Lebanon kuwa nembo ya mapambano na kusimama kidete mbele ya utawala wa Kizayuni na fahari ya Umma wa Kiislamu.

Umoja wa Ulaya baada ya majadiliano yake na wawakilishi wa umoja huo katika kikao chao huko Brussels Jumatatu wiki hii uliliweka tawi la kijeshi la Hizbullah ya Lebanon katika faharasa ya umoja huo ya makundi ya kigaidi. Umoja wa Ulaya umechukua hatua hiyo katika hali ambayo nguvu ya muqawama ya Hizbullah daima inaungwa mkono na serikali ya Lebanon na raia wa nchi hiyo, suala ambalo limemfanya Nabih Berri, spika wa Bunge la nchi hiyo autaje uamuzi huo wa Umoja wa Ulaya kuwa ni huduma ya bure kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Berri ameeleza kuwa kuliweka tawi la kijeshi la Hizbullah katika orodha ya makundi ya kigaidi kutaathiri uhusiano wa nchi za Kiarabu na Ulaya hususan Lebanon na kuifanya hali tete ya nchi hiyo kuwa ya wasiwasi zaidi.

Rais Michel Suleiman wa Lebanon pia amesema, anataraji kuwa Umoja wa Ulaya utatazama upya uamuzi wake kuhusu Hizbullah.

Hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuliweka tawi la kijeshi la harakati ya Hizbullah katika orodha ya makundi ya kigaidi katika kipindi hiki cha kukumbuka mapambano ya siku 33 ya harakati hiyo dhidi ya uchokozi wa utawala wa haramu wa Israel, kama alivyosema Spika wa Bunge la Lebanon, inaweza kuwa na maana gani nyingine ghairi ya kuwa ni idhini na mkono wa baraka wa Umoja wa Ulaya kwa Israel ili kuendeleza jinai zake?

Katika miongo kadhaa iliyopita ambapo nchi za Kiarabu za eneo la Mashariki ya Kati zimekuwa zikikaa kimya mkabala na jinai za utawala wa Kizayuni na hata viongozi wa utawala huo kuamua kuketi katika meza ya eti ya mapatano na utawala huo, Hizbullah imekuwa moja ya harakati chache zilizosimama kidete mbele ya uchokozi wa utawala wa Kizayuni kwa kutegemea nguvu ya muqawama ya Waislamu wa madhehebu ya Shia wa kusini mwa Lebanon ambao wameulazimisha utawala huo kutupilia mbali misimamo, siasa na stratejia zake za kuanzisha chokochoko dhidi ya Lebanon.

Kwa hakika uamuzi wa Umoja wa Ulaya dhidi ya Hizbullah unaakisi nguvu na ushawishi wa lobi za Kizayuni katika nchi za Ulaya na katika maamuzi yanayochukuliwa na nchi hizo kuhusu siasa za kimataifa.

Gazeti la al Mustakbal linalomilikiwa na makundi yanayoipinga harakati ya Hizbullah nchini Lebanon pia limeonesha kushangazwa mno na uamuzi huo wa Umoja wa Ulaya. Gazeti hilo limeandika kuwa, hatua hiyo ya EU itakuwa na madhara kwa maslahi ya kitaifa ya Lebanon na kwamba, imechukuliwa kuifurahisha Marekani na utawala ghasibu wa Israel. Habari kutoka http://kiswahili.irib.ir/uchambuzi/item/33572-msimamo-wa-iran-mkabala-na-uamuzi-wa-eu-kuhusu-hizbullah